Sep 05, 2017 08:00 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (79)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia moja ya tabia njema katika Uislamu nayo ni kumtakia au kuwatakia watu wengine kheri. Tulisema kuwa, katika utamaduni wa Kiislamu suala la kumtakia mtu au watu wengine kheri lina daraja ya juu na jambo hili linahesabiwa kuwa miongoni mwa misingi ya dini.

Tulikunukulieni hadithi ya Bwana Mtume saw amenukuliwa akisema inayosema: Daraja ya juu kabisa Siku ya Kiyama ni ya wale watu ambao hapa duniani walikuwa wakiwatakia kheri watu wengine. Aidha tulibainisha kwamba, endapo utakianaji kheri utazingatiwa na kutekelezwa kikamilifu katika matabaka yote ya jamii, basi suala hilo litakuwa na nafasi muhimu na kubwa katika kuwaongoza watu na jamii ambayo watu wake wanakiana kheri hugeuka na kuwa bustani yenye maua ya thamani ambayo yamejaa huba na upendo wa hali ya juu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 79 ya mfululizo huu kitazungumzia moja ya sifa na tabia ambayo ambayo inahesabiwa kuwa miongoni mwa maradhi ya kimaadili na kiakhlaqi nayo ni tamaa. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki ambapo tutabainisha maana ya tamaa na kukunukulieni baadhi ya hadithi kutoka kwa Bwana Mtume saw na Ahlul Baiti wake watoharifu as kuhusiana na maudhui hii. Karibuni.

*******

Tamaa maana yake ni mtu kukusanya zaidi ya mahitaji yake na kutohisi kutosheka na kile alichonacho. Sifa hii mbaya ya kimaadili, chimbuko lake ni mtu kupenda dunia kupita kiasi. Tamaa ni miongoni mwa tabia na sifa ambazo mawalii na viongozi wa dini wa Mwenyezi Mungu walizitahadharisha; hii ni kutokana na kuwa ni miongoni mwa sifa mbaya ambazo zinamtoa mtu katika njia nyoofu na kumfanya awe mwenye kupenda mambo kupita kiasi yaani asiyekinaika na wakati huo huo kumfanya mhusika kuwa mwenye tamaa na dunia. Licha ya kuwa Mwenyezi Mungu amewaruzuku na kuwapatia wanadamu neema nyingi na tofauti tofauti; lakini watu wenye tamaa daima huwa hawatosheki na siku zote huhangaika huku na kule wakitafuta kujiongezea na kushibisha tamaa yao. Endapo watu wa namna hii watapatiwa dunia yote na vilivyomo, bado kiu yao ya tamaa haitakatika na wataendelea kuhangaika ili wajiongezee mambo zaidi ambayo ni makubwa kuliko hayo waliyopatiwa. Hii ni katika hali ambayo, watu hawa si wenye kushukuru neema za Mwenyezi Mungu na katu hawasalimu amri mbele ya amri za Mola Muumba.

Imam Jaafar Swadiq as anakutambua mwisho wa kutaka makuu na tamaa ni kifo peke yake. Imam Swadiq as amenukuliwa akisema: Ewe mwanadamu! Kuwa makini tumbo lako lisiwe bahari miongni mwa bahari au korongo miongoni mwa makorongo ambayo hayajazwi isipokuwa kwa udongo.

Moja ya madhara ya sifa mbaya ya tamaa ni kwamba, humfanya mtu mwenye tamaa kutokuwa radhi na Mwenyezi Mungu, yaani ni mwenye kunung'unika na Mwenyezi Mungu na kutoridhika na yale aliyopatiwa na Mola Muumba. Hii ni kutokana na kuwa, mtu huyu huwa haridhiki na riziki aliyopatiwa na Mwenyezi Mungu na hutaka zaidi ya alichopatiwa. Hali hii ya mtu mwenye tamaa ya kutoridhika na alichoruzukiwa na Allah chimbuko lake ni kutoamini hekima ya Mwenyezi Mungu au inatokana na kutokuwa na uhakika na ahadi za Mwenyezi Mungu.

 

Imam Ali bin Abi Twalib anasema katika barua yake kwa Malik al-Shtar gavana wake wa Misri kwamba: Usishauriane na watu wa aina tatu. Usimhusishe katika ushauri mtu bakhili kwani atakuzuia kutenda jambo jema kwa kuwa anaogopa umasikini. Usishauriane vpia na mtu mwoga kwani atadhoofisha ari yako ya kutenda mambo. Kadhalika usishauriane na mtu mwenye tamaa, kwani tamaa na dhulma vitajionyesha vizuri mbele ya macho yako. Kwa hakika ubaklhili, uoga na tama ni ghariza tofauti ambazo chimbuko lake ni kuwa na dhana mbaya na Mwenyezi Mungu. Nahaj al balagha 53.

Aidha Mtume saw amenukuliwa akimwambia Imam Ali AS kwamba: "Usishauriane na mtu mwoga, kwani ni mgumu kutekeleza haja na shida yako; na pia usishauriane na bakhili kwani hawezi kukuacha ufikie malengo yake. Kadhalika usishauriane na mtu mwenye tamaa nyingi, kwani yeye naye vitendo vibaya atakuonyesha kuwa ni vizuri na bora. Ewe Ali! Tambua kwamba, kwa hakika woga, ubakhili na tamaa ni vitu vyenye maumbile mamoja ambavyo vyote chimbuko lake ni kuwa na dhana mbaya juu ya Mwenyezi Mungu.

Abu Dhar al-Ghiffari mmoja wa masahaba wa Bwana Mtume saw ananukuu kutoka kwa Bwana Mtume saw ya kwamba, siku moja mbora huyo wa viumbe aliniambia: Ewe Abu Dhar je unapenda kuingia peponi? Nikamwambia, ndio ewe Mtume wa Allah. Akasema: Basi punguza tamaa na matarajio yako, daima kumbuka kifo na mauti na muonee haya Mwenyezi Mungu. Katika sehemu moja Imam Ali bin Abi Twalib as anazungumzia dunia kwa kusema:

'Mtu anayeiashiki dunia moyo wake hugubikwa na mambo matatu: Huzuni isiyoisha, tamaa ya kudumu na matarajio ya mambo asiyoweka kuyapata".

Kwa hakika mtu mwenye tamaa ana dhana mbaya na ahadi za Mwenyezi Mungu na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana hujishughulisha na kujikusanyia mali kwa tamaa na kadiri atakavyopatiwa bado hatisheki bali ni mwenye kuhitajia na kutaka. Chimbuko la hilo ni imani na itikadi dhaifu aliyonayo na vilevile kutokuwa na yakini mtu mwenye tamaa.  Endapo hali hii itaendelea na kuimarika katika nafsi ya mtu, hupelekea hata kukufuru na kumlalamikia Mwenyezi Mungu.

Imam Jaafar al Sadiq

 

Imam Swadiq as amenukuliwa akisema kuwa: Nguzo za kufru ni vitu vitatu, tamaa, kiburi na husuda. Ama tamaa ni pale Adam as alipokatazwa kula tunda na mti uliopigwa marufuku peponi, lakini tamaa yake ililamzimisha akala tunda kutoka katika mti ule. Kuhusiana na kiburi, ni pale Iblisi alipoamrishwa na Mwenyezi Mungu amsujudie Adam as; lakini kutokana na kiburio alichokuwa nacho alikataa kutii amri ay Allah iliyomtaka amsujudie Adam. Ama husuda, ni ile iliyomfanya mmoja wa watoto wa Nabii Adam yaani Qabil amuuue ndugu yake yaani Habil, na tambueni kwamba, vitu hivi vitatu ni chimbuko la mzizi wa kila kosa na dhambi."

Kwa hakika tamaa ni miongoni mwa tabia ambazo humpokonya mwanadamu uhuru na hivyo kumfanya mtumwa wa tamaa na matakwa yake. Kama mnavyojua thamani ya mwanadamu ni katika uhuru, hadhi na heshima yake. Hii ni kutokana na kuwa, mtu mwenye izza na heshima hujizuia kufanya matendo mabaya, machafu na yasiyo na thamani. Endapo nafsi itakuwa haina izza na uhuru, hakuna kitu kitakachoizuia kutumbukia Kartika dhambi na maasi. Mtu mwenye tamaa huwa tayari hata kuuza uhuru na heshima yake kwa sababu tu apate kitu na starehe ndogfo ya dunia.

Katika jamii zetu tunazoishi tumeona jinsdi baadhi ya watu wenye tamaa wanavyokubalia kuuuza kwa bei rahisi thamani yao na izza yao ya bei ghali kwa sababu ya kitu kidogo ambacho kama angeweza kuizuia nafsi na kuishikilia na akaweka kando tamaa na uchu asingegeuka na kuwa mtumwa na mtu dhalili. Imekuja katika hadithi kwamba: Siku moja Imam Ali as alitakiwa atoe maana ya tamaa. Akasema katika maneno machache tu kwamba: Tamaa ni kutaka kitu kidogo mkabala wa kupoteza kitu kikubwa na chenye thamani.

Aidha katika sehemu nyingine Imam Ali AS anasema: Uchu na tamaa humpunguzia mtu thamani na hadhi yake na wakati huo huo riziki yake haiongezeki. Wakati mwingine mtu anadhani kwamba, tamaa ni jambo ambalo humkumba mtu akiwa katika zaman a rika la ujana tu na kwamba, atakapozeeka na tamaa itamalizika. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa, kadiri zama zinavyopita, mtu mwenye tamaa huzdi kumbwa na tamaa na uchu weake huongezeka. Mtume saw amenukuliwa akisema: Mwana wa Adamu anazeeka lakini sifa mbili hubakia kuwa na ujana, tamaa na uchu wa mali na tamaa ya umri.