Sep 05, 2017 08:09 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (80)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia sifa mbaya ya kimaadili ya tamaa na uchu na tulisema kuwa, maana yake ni mtu kukusanya zaidi ya mahitaji yake na kutohisi kutosheka na kile alichonacho.

Sifa hii mbaya ya kimaadili, chimbuko lake ni mtu kupenda dunia kupita kiasi. Tulisema kuwa, tamaa ni miongoni mwa tabia na sifa ambazo mawalii na viongozi wa dini ya Mwenyezi Mungu walizitahadharisha; hii ni kutokana na kuwa ni miongoni mwa sifa mbaya ambazo zinamtoa mtu katika njia nyoofu na kumfanya awe mwenye kupenda mambo kupita kiasi yaani asiyekinaika na wakati huo huo kumfanya mhusika kuwa mwenye tamaa na dunia. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 80 kitazungumzia tamaa nzuri. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.
Neno tamaa kikawaida hutumika hutumika zaidi kwa upande wa maana mbaya na hasi na kila linapotajwa neno hili basi linalompitikia zaidi msikilizaji ni tamaa ya mali, utajiri, cheo na mambo mengine ya kimaada. Hata hivyo neno tamaa katika baadhi ya mambo hutumika kwa namna ambayo hustahiki sifa. Yaani si tu kwamba, katika baadhi ya mambo tamaa haihesabiwi kuwa ni tabia mbaya na chafu; bali huhesabiwa kuwa na fadhila. Kwa maana kwamba, kuna tamaa nzuri na mbaya na wakati mwingine neno tamaa huwa na maana ya kutamani na kuhangaika kwa ajili mtu apate kitu fulani yaani kumtamania mtu kitu fulani. Mwenyezi Mungu anaizungumzia maana hii ya tamaa katika aya ya 128 ya Surat Twaba kwa kusema:

 

Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.
Katika aya hii, Mtume SAW alikuwa akihangaika na kutaabika akitamani watu wapate hidaya na uongofu.
Hivyo kama tamaa katika masuala ya kimaada na kidunia inahesabiwa kuwa ni sifa mbaya na isiyopendeza, katika masuala ya kimaanawi na ya akhera, tabia hii inahesabiwa kuwa moja ya ukamilifu. Kwa muktadha huo inafahamika kwamba, kuwa na tamaa kwa ajili ya masuala ya kimaada na kidunia kunahesabiwa kuwa miongoni mwa tabia mbaya, lakini wakati huo huo kuwa na tamaa katika masuala ya kimaanawi na kwa ajili ya akhera, ni miongoni mwa tabia nzuri na moja ya mambo yanayomkamilisha muumini. Kuhusiana na jambo hili Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema:
Wewe ni mwenye tamaa kwa ajili ya kupata kile ambacho kimekadiriwa kwako yaani riziki, basi kuwa na tamaa pia katika kufanya kile ambacho kimewajibishwa kwako.
Katika hadithi hii Imam Ali anataka kuashiria nukta moja muhimu sana nayo ni kwamba, kama ambavyo sisi wanadamu tunatamani kupata masuala ya kimaada na riziki ambayo Allah amekwishayakadiria kwa ajili yetu, basi tuwe na tamaa pia katika kuyafanya mambo ya wajibu ambayo Mola Muumba ameyawajibisha kwetu.
Ukweli ni kuwa, tamaa inagawanyika katika sehemu mbili: Tamaa mbaya inayochukiwa na ambayo ipo katika masuala ya kidunia na kimaada. Na nyingine ni tamaa nzuri na inayopendwa ambayo yenyewe iko zaidi katika masuala ya kimaanawi na kiakhera. Kama tulivyotangulia kusema tamaa ambayo ni kwa ajili ya kujipatia mali za dunia, uongozi, jaha na cheo inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa tabia mbaya. Lakini tamaa kwa ajili ya watu wengine, kuumia moyo na kuguswa na jambo la mtu na kuwa na mapenzi makubwa ya kutoa msaada wa kifedha kwa watu wengine na kukidhi haja za waumini, kuwafanya wapate faida, kutatua matatito ya wengine na kuwaongoza na kuwaokoa, zote hizo ni miongoni mwa aina za tamaa ambazo ni nzuri na zenye kupendwa katika mafundisho ya Kiislamu. Aina hii ya tamaa si tu kwamba, haichukiwi na kukemewa na mafundisho ya Kiislamu, bali inahesabiwa kuwa moja ya tabia nzuri za kimaadili.
Imam Ali bin Mussa al-Ridha AS kama alivyokuwa babu yake yaani Mtume saw, naye alikuwa mstari wa mbele katika kuwaongoza na kuwaokoa watu, alikuwa daima akiwashajiisha wafuasi na watu wake wa karibu juu ya kujipamba na sifa ya tamaa nzuri. Alikuwa akisema: 
Kuweni wenye tamaa ya kukidhi haja na shida za Waumini, kuwafurahisha na kuwaondolea mambo mabaya na yanayochukiza.
Katika hadithi hii Imam Ridha AS anawataka watu wawe ni wenye tamaa na shauku, lakini sio tamaa ya kukusanya na kujilimbikizia mali na utajiri kwa ajili yao, la hasha, bali ni tamaa ya kuwasaidia waumini na kuwaondolea shari ya waja wa Mwenyezi Mungu.

 

Dini tukufu ya Kiislamu, licha ya kuwa inakataza mtu kuwa na tamaa katika maisha ya dunia, lakini katika masuala kama kujifunza na kutafuta elimu inatilia mkazo mno jambo hili. Hii ni kutokana na kuwa, dini hii inatambua kuwa, kutosheka na ulicho nacho katika uwanja huu ni moja ya sababu za kuzorota kielimu na kubakia nyuma kimaendeleo. Katika hadithi mashuhuri iliyopokelewa kutoka kwa Bwana Mtume saw, mbora huyo wa viumbe anasema kuwa:
“Kutafuta elimu ni faradhi (lazima) kwa kila Mwislamu Mwanamume na Mwislamu mwanamke". 
Aidha kuna hadithi nyingi zinazoonyesha kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda wanaotafuta elimu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana kuwa na tamaa kwa ajili ya kutafuta elimu na kujifunza, ambako ni kule kudumu katika hali ya kutafuta elimu, ni jambo linaloshajiishwa katika Uislamu.
Katika hadithi moja ya thamani iliyonukuliwa kutoka kwa Imam Jafar Swadiq as, mjukuu huyo wa Bwana Mtume saw anazungumzia na kubainisha umuhimu wa kuwa na tamaa katika kutafuta elimu na kwamba, hizo ni katika ishara za muumini. Anasema: 
Muumini ana nguvu katika dini yake na ni mwenye tamaa katika kufahamu dini.
Moja ya masuala mengine ambayo ni misdaqi na mfano wa tamaa nzuri na yenye kusifiwa ni mtu kuwa na tamaa na shauku katika kufanya amali za kheri na zinazotakiwa na Mwenyezi Mungu. Tamaa katika masuala haya ni stahiki na yenye kupendeza. Katika dini tukufu ya Kiislamu tamaa hii ya kufanya amali ya kheri ina umuhimu kiasi kwamba, Mtume saw anaitaja kuwa ni katika ishara za toba na kurejea kwa Mwenyezi Mungu. Anasema:  Ishara za mwenye kutubu ni nne: Amali yenye ikhlasi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kuacha kufanya batili, kufungamana na haki na kuwa na tamaa ya kufanya mambo ya kheri.
Kwa msingi huo kama tamaa itakuwa katika mstari wa malengo aali na ya juu ya kiutu na kibinadamu, sio tu kwamba, ni jambo zuri na la kupendeza, bali huwa ni katika sifa maalumu za waja wa Mwenyezi Mungu. Mtu ambaye anaweka mguu na kufanya harakati katika njia ya Mwenyezi Mungu na kupata elimu na maarifa kwa akili yake tena kwa njia sahihi, hupata kasi ya kufanya mambo ya kheri na huwa mstari wa mbele katika hili. Kuwa na kasi, kuwapita na kuwatangulia watu wengine katika kufanya mambo ya kheri katika njia kuu nyoofu ya uongofu, sio tu kwamba, ni jambo la kupendeza bali ni wajibu kufanya hivyo. Kila mtu anapaswa kufanya hima na idili ili awe mstari wa mbele katika taqwa na uchaji Mungu na hivyo kuwa kiigizo na ruwaza njema kwa wengine.
Imam Muhammad Baqir AS anaitambua tamaa kwa ajili ya ushindani salama kuwa ni jambo linalojuzu.
Anasema:
Hakuna tamaa nzuri kama kushindana kwa ajili ya kufikia daraja za juu.
Wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi hiki nao naona unanipa mkono hivyo sina budi kukomea hapa kwa leo. Tukutane tena wiki ijayo, Inshallah.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.