Sep 05, 2017 08:18 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (82)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia na kujadili namna ya kutibu maradhi ya kimaadili ya tamaa mbaya. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 82 ya mfululizo huu, kitazungumzia moja ya maradhi mengine ya kimaadili nayo ni tabia mbaya ya ubakhili. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika chache ili kutegea sikio yale niliyokuandalieni. Karibuni.

Ubahili maana yake ni hali ya mtu kubania pesa au mali hata kwa haja zake mwenyewe. Katika lugha mwenye hali hii anajulikana kama bakhili, mchoyo, mtu mgumu au mwenye mkono wa birika. Aidha inaelezwa kuwa, maana ya ubahili ni mtu kujizuia kutumia pesa na mali yake katika mahala panapostahiki. Kwa hakika ubakhili ni miongoni mwa tabia mbaya na maradhi haribifu ya kinafsi. Dini tukufu ya Kiislamu imekokoteza na kuwataka wafuasi wake wajiepushe na tabia ya ubahili. Aidha mafundisho ya kiuchumi ya Kiislamu sambamba na kukataza ufujaji na israfu yanakemea sana tabia ya ubahili na kuwa na mkono wa birika ambayo husababisha mali na utajiri kuganda sehemu moja na kutokuwa na mzunguko sahihi katika jamii.

Katika nasaha zake za kimaadili na kiakhlaqi kwa Waislamu, Mtume saw amenukuliwa akisema: Jitengeni mbali na ubahili, ambapo waliokuwako kabla yenu waliangamia kutokana na ubahili. Ubahili wao uliwalazimisha kusema uongo, hivyo wakasema uongo.

 

Pamoja na kuwa, ubahili maana yake ni hali ya mtu kujizuia kutumia pesa au mali yake mahapa panapostahiki, lakini tukirejea katika Qur'ani tukufu tunakuta kwamba, ubakhili una maana pana zaidi ambapo unaingia hata katika masuala kama kuacha kufanya mambo na amali za kheri, jihadi na kadhalika.

Kimsingi kwa mtazamo wa Qur'ani ni kuwa, kila neema ambayo mtu amepatiwa na Mwenyezi Mungu na akawa haitumii kama inavyotakiwa, basi anahesabiwa kuwa amefanya ubahili katika neema hiyo iwe na mali na kitu kingine. Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewatunuku na kuwaruzuku wanadamu ujazi na neema nyingi katika uwanja wa kimaada na kimaanawi. Si tu kwamba, bahili hujinyima na kujizuia kutumia pesa, mali na neema aliyopatiwa na Mwenyezi Mungu, bali wakati mwingine hata huwazuia watu wengine wasinufaike na neema hiyo.

Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 180 ya Surat al-Imran:

Wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika aliyo wapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni kheri yao. Bali hiyo ni shari kwao. Watafungwa kongwa za yale waliyo yafanyia ubakhili Siku ya Kiyama. Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote myatendayo.

Katika aya hii, Mwenyezi Mungu anawaambia wale wanaofanya ubakhili katika vile alivyowapatia na kuwaruzuku Mwenyezi Mungu kwamba, wasidhani kufanya hivyo ni kheri bali ni shari kwao. Hivyo basi kwa mujibu wa aya hii, watu wanaofanya ubakhili mbali na kupata mashaka na taabu hapa duniani, Siku ya Kiyama pia watapata adhabu kali.

Hadithi ya Uongofu

 

Imam Ja'far Swadiq (as) anaelezea shida na taabu za bakhili na madhara anayopata kwa kusema:

Bakhili hufanya ubakhili kwa kile alichonacho na hata kwa kile ambacho kiko mikononi mwa watu, kiasi kwamba, kila atakachokiona kwa watu hutamani akipate iwe ni kwa nia ya halali au ya haramu. Hatosheki na alichopatiwa na wala hanufaiki nacho.

Katika maisha haya ya dunia, kuna watu wamezama katika kufikiria na kutafuta pesa na mali ya dunia kana kwamba, hawana wanachokijua bighairi ya pesa na mali. Watu wa aina hii hujitaka kwa ajili ya pesa na sio pesa kwa ajili yao. Msiba mkubwa kwa watu hawa ni kwamba, huhangaika na kutaabika kwa ajili ya kutafuta pesa na hata kuhatarisha roho, maisha na kutumia umri wao kwa ajili ya kutafuta pesa, lakini hawako tayari kutumia pesa hizo kwa ajili ya afya na saada yao.

Imam Ali bin Abi Twalib (as) amenukuliwa akisema katika maneno yaliyojaa hekima yanayopatikana katika Kitabu cha Bihar al-Anwar kwamba:

“Namshangaa bakhili anauvuta umasiki upande wake ilihali watu wanaukimbia, na anaupoteza utajiri ambao watu wanautafuta. Anaishi duniani kama hohehahe na fukara, na Siku ya Kiyama atahesabiwa kama tajiri na mtu mwenye uwezo.”

Kwa hakika watu ambao wana uwezo mkubwa lakini hawatoi uwezo wao huo ili watu wanufaike nao, hawa pia hukumu yao ni mithili ya bakhili na hata ghadhabu za Mwenyezi Mungu hupelekea waharamishiwe pepo. Hii ina maana kwamba, watu ambao wana uwezo wa kifedha au hata wa kielimu wanapaswa kutoa uwezo wao huo ili watu wengine wasio na uwezo huo wanufaike nao. Kufanya hivyo watakuwa wameondolewa katika kundi la mabakhili na wakati huo huo kuepukana na ghadhabu na hasira za Mwenyezi Mungu ambazo zingewaharamishia pepo.

Imam Ja'far Swadiq (as) anasema:

Kila mtu ambaye atakuwa na nyumba na muumini akawa na haja ya kuishi katika nyumba hiyo, lakini mwenye nyumba akamnyima fursa hiyo na kumrejesha, Mwenyezi Mungu husema kuhusiana na mtu huyo kwamba: Enyi Malaika wangu! Mja wangu, amemfanyia ubakhili wa nyumba na makazi mja wangu. Ninaapa kwa izza na utukufu wangu ya kwamba, katu sitamuingiza peponi mja huyu (bakhili).

Imam Ali bin Abi Twalib (as) amenukiliwa akisema kuwa:

Kila mtu ambaye atakuwa na kitu na mtu mwingine akawa ni mwenye kukihitajia lakini akafanya ubakhili na kumnyima, Mwenyezi Mungu hughadhibika.

 

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kisa kifuatacho:

Inasimuliwa kwamba, siku moja Bwana Mtume saw alikuwa akitufu katika Nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba, mara akamuona Bwana mmoja akiwa amening'nia katika al-Kaaba huku akisema: Ewe Mola, ninaapa kwa utukufu na adhama ya al-Kaaba, nisamehe dhambi zangu. Mtume saw akamuuliza Bwana yule, kwani umefanya dhambi gani? Niambie dhambi yako ni nini? Bwana yule akasema, dhambi yangu ni kubwa kiasi cha kutoweza kuitolea wasifu na maelezo. Mtume saw akamwambia: Ole wako! Dhambi yako ni kubwa kuliko maeneo ya nchi kavu? Akasema, ndio ni kubwa ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mbora wa viumbe Mtume akamuuliza: Je dhambi yako ni kubwa kuliko bahari? akajibu ndio ewe mjumbe wa Allah. Mtume akasema, hebu nieleze dhambi yako ni kubwa au Mwenyezi Mungu ni mkubwa kuliko dhambi yako? Akasema, Mwenyezi Mungu ni mkubwa na mtukufu  zaidi. Mtume akasema, Hebu nieleze, umefanya dhambi gani ambayo unaitaja kwa ukubwa kiasi hiki?  Bwana yule huku akiwa anaongea kwa masikitiko alisema; Ewe Mtume wa Allah! Mimi ni mtu tajiri, lakini kila anaponijia mtu mhitaji basi hupatwa na hali kama ambayo ameniletea moto. Kwa hakika ninaingiwa na hofu na woga mkubwa ninapowaona masikini na wahitaji. Mtume akamwamba, kaa mbali na mimi usije ukaniunguza kwa moto wako. Kisha Mtume akasema, ninaapa kwa Mola aliyeniongoza na kunipa Utume, endapo utasimama baina ya rukni na maqam na ukafanya ibada miaka elfu mbili, ukalia kiasi cha macho yako kutoa maji kama mto na maji hayo kushibisha miti, kisha ukafa katika hali ya ubakhili, basi Mwenyezi Mungu atakutupia motoni akitanguliza uso wako, je hufahamu kwamba, Allah amesema, kila ambaye atafanya ubakhili, amejifanyia ubakhili mwenyewe na kila ambaye atasalimika na ubakhili ni mkweli.

Wassalaamu Alayakum Warahmatullahi Wabakaatuh.