Hadithi ya Uongofu (83)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo, na karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Hadithi ya Uongofu.
Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia moja ya sifa mbaya ya kimaadili ya ubakhili. Tulisema katika kipindi hicho kwamba, ubahili maana yake ni hali ya mtu kubania pesa au mali hata kwa haja zake mwenyewe. Tulibainisha kwamba, bakhili ni mtu ambaye hayuko tayri kutumia mahala pake mali, elimu yake na neema nyingine alizoruzukiwa na Mwenyezi Mungu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 83 ya mfululizo huu, kitazungumzia sifa nzuri ya ukarimu ambayo iko kinyume na ubakhili na kuelezea jinsi ubakhili ulivyokemewa katika mafundisho ya Kiislamu. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa name hadi mwisho wa dakika hizi chache kusikiliza yale niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.
Ukarimu ni moja ya sifa bora kabisa za kimaadili. Tukirejea mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu tunaona ni kwa namna gani kufanya ukarimu na hisani kulivyokokotezwa na kutiliwa mkazo. Katika baadhi ya hadithi zilizonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume saw, mbora huyo wa viumbe anaufananisha ukarimu na kuutaja kuwa moja ya miti inayopatikana peponi.
Katika vyanzo vya dini, kuna onyo na indhari kali kabisa kuhusiana na ubakhili na mkabala na hilo kumetole wasifa nyingi kuhusiana na ukarimu. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anautaja ubakhili kama ni sifa mbaya mno. Anasema: Kumtazama bakhili hupelekea roho ngumu. Aidha mkabala na ubakhili, Imam Ali bin Abi Twalib (as) ametoa sifa kemkemu nzuri na kusifia ukarimu. Amenukuliwa akisema kuwa; Ukarimu ni sifa kubwa ya Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake, Mtume saw amelinganisha ukarimu na ubakhili na kusema kuwa: Ukarimu ni mti miongoni mwa miti ya peponi ambao matawi yawe yamening’inia duniani na kila atakayechukua tawi lake basi tawi hilo litampeleka peponi; na ubakhili ni mti ambao matawi yake yamening’inia duniani na kila mtu ambaye atachukua tawi lake, basi tawi hilo humvuta na kumpeleka motoni.
Wapenzi wasikilizaji, kupitia hadithi iliyotangulia inafahamika kwamba, ukarimu una mizizi peponi na sifa hii inahesabiwa kuwa miongoni mwa sifa za watu wa peponi na wakati huo huo, ubakhili chimbuko lake ni motoni na mtu bakhili na mwenye tamaa ndani ya nafsi yake ana moto wa Jahanamu ambao unamuunguza yeye mwenyewe na wakati huo huo unaiunguza jamii pia. Aidha katika kusifia ukarimu na kukemea ubakhili Qur’ani Tukufu inasema katika aya ya 5 hadi ya 10 za Surat Layl:
Ama mwenye kutoa na akamchamngu. Na akaliwafiki lilio jema. Tutamsahilishia yawe mepesi. Na ama mwenye kufanya ubakhili, na asiwe na haja ya wenzake. Na akakanusha lilio jema, Tutamsahilishia yawe mazito!
Imekuja katika vitabu vya tafsiri kuhusiana na aya hizi kwamba:
Katika zama za Bwana Mtume saw alikuweko Bwana mmoja miongoni mwa Waislamu ambaye tawi la moja ya mitende yake lilikuwa limeinamia katika nyumba ya masikini mmoja aliyekuwa na mke na watoto. Mwenye mtende ule wakati alipokuwa akipanda juu kwa ajili ya kuchuma tende, wakati mwingine baadhi ya tende zilikuwa zikidondokea katika nyumba ya Bwana yule masikini na watoto wake walikuwa wakizichukua tende zile. Bwana mmiliki wa mtende ule alikuwa akishuka kutoka juu ya mtende na kwenda kuwanyang’ang’a watoto wale tende walizoziokota. Bwana yule alikuwa bakhili na mwenye roho ngumu kiasi kwamba, kama watoto wale walikuwa wameanza kuzila tende zile alikuwa akitia vidole katika midomo ya watoto wale ili atoe tende. Baada ya vitendo vya mmiliki mitende kukithiri, Bwana yule maskini alikwenda kumshtakia Bwana Mtume saw.
Baada ya Mtume saw kusimuliwa mkasa ule alifunga safari na kwenda kumuona mmiliki wa mitende ile. Kisha akamwambia Bwana yule, je utanipatia matawi ya mitende yako iliyoko juu ya nyumba ya fulani, ili mkabala wake upate mti katika miti ya peponi? Bwana yule akasema: Mimi nina miti mingi ya mitende na hakuna tende nzuri kama tende za mitende yangu, hivyo siko tayari kufanya muamala katika hili.
Mmoja wa masahaba wa Mtume saw ambaye alisikia maneno yale alimwambia Bwana Mtume saw: Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu, kama mimi nitakwenda na kununua mtende wa Bwana yule na kisha nikaukabidhi, je utanipatia kitu kile kile ulichomuahidi Bwana yule? Mtume saw akasema, ndio. Swahaba yule wa Bwana Mtume saw alikwenda kuonana na mmiliki wa mitende na kumueleza nia yake ya kutaka kununua mtende ule. Bwana yule baada ya kusikia ombi lake akasema: Je unajua kwamba, Muhammad saw alikuwa tayari kunipatia mti miongoni mwa miti ya peponi badala ya mtende huu na mimi nikakataa? Mnunuzi yule akasema: Je unataka kuuza mtende wako huu au la? Bwana yule bakhili akasema, siuzi, isipokuwa kama atatokea mtu na kunipatia fedha ambazo sitarajii! Bwana yule akamuuliza fedha kiasi gani? Akajibu, kwa mfano mitende arobaini!?.
Mnunuzi akapigwa na butwaa na kumwambia, unataka gharama kubwa mno kwa ajili ya mtende mmoja uliopinda. Hata hivyo mnunuzi yule baada ya kunyamaza na kutafakri kidogo juu ya kile atakachopata endapo atafanikiwa katika hili, akasema, vizuri, nitakupa mitende arobaini mkabala na mtende wako huu mmopa. Baada ya wawili hao kumaliza kazi ya kuuziana na makabiadhiano, mnunuzi yule alielekea kwa Bwana Mtume saw na kumwambia, Ewe Mtume wa Allah!! Tayari mtende ule ni mali yangu baada ya kuunua na sasa ninakukabidhi kwako. Baada ya hapo, Bwana Mtume saw alikwenda kwa Bwana yule masikini na kumwambia kwamba, kuanzia sasa mtende huu ni mali yako wewe na watoto wako.
Wapenzi wasikilizaji kupitia kisa hiki tunafahamu kwamba, ni kwa kiasi gani ubakhili humfikisha mhusika katika hatua hata ya kusahau ubinadamu na kusahau hata akhera yake. Vile vile mionghoni mwa mafunzo tunayoyapata kupitia kisa hiki ni kwamba, mkarimu hufikia malipo yake mema na bakhili hubakia katika njia ngumu nay a taabu na daima huwa na madhara ya wasiwasi na hofu ya kupungukiwa na alichonacho.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.