Hadithi ya Uongofu (84)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo Wapenzi Wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Katika kipindi chetu kilichopita tulizungumzia moja ya tabia nzuri ya kimaadili nayo ni ukarimu, Tulisema kuwa, ukarimu ni moja ya sifa za Mwenyezi Mungu.
Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 84 ya mfululizo huu kitaendelea na mada hii ya ukarimu na kuzungumzia athari za kufanya ukarimu au jamala na hisani na baadhi ya faida anazopata yule aliyejipamba kwa sifa ya ukarimu. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache ili mtegee sikio kile kilichokuandalieni kwa leo, hii ikiwa ni sehemu ya 84 ya mfululizo huu. Karibuni.
*******
Kwa hakika dini tukufu ya Kiislamu imelipa umuhimu mkubwa na wa hali ya juu, suala la kujipamba na sifa nzuri za kimaadili na kiakhlaqi kama kusaidia watu, kuwana ukarimu, kufanya juhudi kwa ajili ya kutatua matatizo ya wengine na kukidhi hawaiji na shida za watu. Hata katika jamii ambayo ina wakarimu, huba na mapenzi hushuhudiwa miongoni mwa wanajamii hao.
Ukarimu ni katika sifa za Mwenyezi Mungu na mtu mkarimu ni dhihirisho la tabia za Mwenyezi Mungu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana mtu mkarimu yuko karibu zaidi na Mwenyezi Mungu. Tukirejea mafundisho ya Kiislamu tunapata ni namna gani ukarimu ulivyo na fadhila kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, kiasi kwamba, baadhi ya hadhithi zinaeleza kwamba, mtu mkarimu yupo karibu na Mwenyezi Mungu, yupo karibu na kheri, yupo karibu na pepo na yupo karibu na watu. Aidha hadithi hizo zinaeleza kuwa, mkarimu yupo mbali na moto wa Jahanamu.
Kadhalika hadithi hiyo zinasema, bakhili yupo mbali na Mwenyezi Mungu, yupo mbali na kheri, yupo mbali na pepo, yupo mbali na watu, yupo karibu na moto wa Jahanamu. Katika upande mwingine, hadithi hizo zinamfadhilisha mtu mjinga lakini mkarimu, mbele ya mtu anayemuabudu Mwenyezi Mungu lakini ni bakhili. Baadhi ya hadithi zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume saw zinasema kuwa, "Jahili mkarimu anapendwa zaidi na Mwenyezi Mungu kuliko mtu anayemuabudu Allah lakini ni bakhili.
Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa, mtu mkarimu yupo karibu na Mwenyezi Mungu, na watu na pepo.
Kwa hakika mtu mkarimu huhesabu mali na miliki alizonazo kwamba, zimetokana na huba na mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwake na ni kutokana na kuwa na mtazamo huo ndio maana huwa yuko tayari kutoa kwa urahisi na kuwasidia watu wengine. Mkarimu anatambua kwamba, mali zake alizonazo ni kutoka kwa Mwenyezi Mungu na anahesabu hali ya kutoa, kufanya wema na hisani pamoja na ukarimu kwamba, ni mapenzi na tawfiki ya Allah kwa mja wake. Katika kubainisha umuhimu na thamani ya ukarimu, Imam Ja'far Swadiq (as) anasema: Ukarimu ni katika tabia za Manabii na nguzo ya imani. Hakuna mtu mwenye imani isipokuwa ni mwenye na ukarimu na hakuna mkarimu isipokuwa ni mwenye yakini na hima ya juu…
Kwa hakika miongoni mwa faida za kufanya wema na ukarimu ni mtu kujumuishwa katika rehma zisizo na kikomo za Mwenyezi Mungu.
Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa, Siku ya Kiyama ataletwa Bwana mmoja na kisha kuulizwa sema hoja ulizonazo:
Atasema: Mwenyezi Mungu umeniumba, ukaniongoza, ukanipatia riziki na mimi daima nilikuwa ni mwenye huruma kwa viumbe wako, niliwafanyia hisani na ukarimu, ili leo unijumuishe katika rehma Zako na unifanyie wepesi. Mwenyezi Mungu Mtukufu atasema: Mja wangu anasema kweli. Muingizeni peponi.
Aidha Imam Jaafar Swadiq (as) amenukuliwa akimwambia mmoja wa masahaba zake: Je unataka nikujulishe jambo ambalo kupitia kwake utajikurubisha na Mwenyezi Mungu na pepo, na kuwa mbali na moto wa Jahanamu: Sahaba yule wa Imam Swadiq (as) akasema: Ndio! Imam Swadiq (as) akasema: Hongera kwa kufanya ukarimu.
Kwa hakika mtu ambaye ni mkarimu na ambaye anatunguliza mbele suala la kutoa alichonacho katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi Mola Muweza humfanyia wepesi mja huyo katika mambo yake na kumjaalia uwezo wa kustahamili matatizo na misukosuko. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 5 hadi ya 10 za Surat Layl:
Ama mwenye kutoa na akamchamngu. Na akaliwafiki lilio jema. Tutamsahilishia yawe mepesi. Na ama mwenye kufanya ubakhili, na asiwe na haja ya wenzake. Na akakanusha lilio jema, Tutamsahilishia yawe mazito!
Kwa mujibu wa Aya hizi Mwenyezi Mungu anawajumuisha katika rehma na taufiki Yake wakarimu na watu wanaotoa mali na walivyoruzikiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu na huwafanya waendelee kwa wepesi kubakia katika njia ya taa ya Mwenyezi Mungu na kutoa katika njia Yake.
Na Wakati huo huo, wanaofanya ubakhili na kukanusha yaliyo mema Allah huya fanya mambo yao kuwa magumu.
Ukarimu ni pambo la tabia na hulka ya mwanadamu na ni kama ua lenye harufu nzuri ambalo humvutia kila mtu.
Imam Ali (as) anasema kuhusiana na hilo kwamba: Ukarimu huleta huba na mapenzi na ni pambo la tabia (tabia njema).
Kutokana na umuhimu wa ukarimu katika jamii, Bwana Mtume saw ametilia mkazo na kuusisitizia mno umma wake.
Mtume saw anasema:
Fumbieni macho dhambi na kuteleza kwa mtu mkarimu, kwani kila mara anapoleteza na kukosea, Mwenyezi Mungu hushika mkono wake na kumuokoa. Aidha kuna hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume saw na Ahlul-Baiti wake watoharifu (as) zinaoonyesha na kubainisha ni kwa jinsi gani ukarimu huleta huba na mapenzi na kuwafanya watu kuwapenda wakarimu.
Miongoni mwa athari nyingine za kujipamba na sifa njema ya ukarimu na kufanyia watu hisani na wema ni kuokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu au kwa uchache watu wakarimu hupunguziwa adhabu.
Imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume saw kwamba, siku moja alimwambia mtoto wa Haatam Twai aliyejulikana kwa jina la Udey kwamba, baba yako ameondolewa adhabu kali ya moto wa Jahanamu kwa sababu ya sifa nzuri ya ukarimu aliyokuwanayo.
Aidha vile vile ukarimu huwa chimbuko na sababu ya mtu kupata uongofu. Inasimuliwa kwamba, siku moja watu kutoka Yemen walimuendelea Bwana Mtume saw. Miongoni mwao alikuwepo Bwana mmoja ambaye alikuwa mzungumzaji sana. Alisema maneno mbele ya Bwana Mtume saw ambayo yalimuudhi na kumkasirisha mbora huyo wa viumbe.
Katika hali hiyo, Malaika Jibril alimshukia Mtume saw na kumwambia kwamba, Mwenyezi Mungu anakutumia salamu na kukwambia kwamba, Bwana huyu ni miongoni watu wakarimu! Baada ya kusikia maneno hayo, ghadhabu na hasira za Mtume zilishuka, akanyanyua kichwa chake na kusema: Lau kama si Malaika Jibril kunijulisha kwamba, wewe ni katika wakarimu na wenye kuwafanyia hisani watu wengine, basi ningekufukuza kutoka hapa na kukufanya ibra kwa wengine. Bwana yule akauliza, je Mola wako anawapenda watu wakarimu? Mtume akajibu kwa kusema, ndio, Bwana yule akasema: Ninashuhudia kwamba, hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah, na ninashuhudia kwamba wewe Muhammad ni mjumbe wake na Mtume wake.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.