Hadithi ya Uongofu (85)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na ni wasaa na wakati mwingine wa kukutana nami sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu ambacho hujadili maudhui mbalimbali za kidini, kijamii, kimaadili na kadhalika na kukunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na maudhui hizo kutoka kwa Bwana Mtume saw na Maimamu watoharifu as.
Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 85 ya mfululizo huu, kitazungumzia maudhui ya sadaka na kukunukulieni baadhi ya hadithi zinazozungumzia suna hii nzuri ya Mtume saw. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi. Karibuni.
********
Sadaka ni mtu kutoa kitu chake katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kila linapozungumziwa suala la sadaka na kutoa sadaka, basi watu wengi fikra zao hukimbilia katika pesa na mali. Hata hivyo katika mafundisho ya Kiislamu sadaka haiishii tu katika fedha na mali, bali ina maana na fasili pana na yenye wigo mpana zaidi. Maneno haya yanathibitishwa na kauli ya Mtume saw ambaye amenukuliwa akisema:
“Kila mwenye kutenda wema na hisani kwa sura yoyote ile basi huhesabiwa kuwa ametoa sadaka katika njia ya Mwenyezi Mungu.”
Tunaona katika hadithi hiyo iliyotangulia kwamba, sadaka haiishi katika kutoa fedha na mali tu, bali hata wema na hisani inahesabiwa kuwa ni kutoa sadaka katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Katika hadithi nyingine, mbora huyo wa viumbe amenukuliwa akisema kuwa: Ni jukumu la Mwislamu kutoa sadaka kila siku. Akaulizwa, Ewe Mtume wa Allah, nani mwenye uwezo wa kufanya hilo kila siku? Mtume akasema: Kumuonyesha mtu njia ni sadaka, kumtembelea mgonjwa ni kutoa sadaka, kuamrisha mema, ni sadaka, kuondoa jiwe na miba katika njia wanayopita watu ni sadaka na kujibu salamu ni sadaka.
Wapenzi wasikilizaji kupitia hadithi hiyo iliyonukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume saw katika kitabu cha Bihar al-Awar juzuu78 tunafahamu kwamba, sadaka imegawanyika katika sehemu nyingi na si sahihi kuamini kwamba, sadaka inaishia katika masuala ya kutoa fedha na mali tu katika njia ya Mwenyezi Mungu, bali hata kumtembelea mgonjwa na kumjulia hali yake ni mithili ya kutoa sadaka na hisani na wema tofauti katika jamii.
Katika kutaja aina nyingine ya sadaka, Imam Jaafar Swadiq (as) amenukuliwa akisema: Sadaka ambayo Mwenyezi Mungu anaipenda zaidi ni kuleta upatanishi baina ya watu wawili ambao uhusiano wao umeingia dosari na kuwakurubisha pamoja kila wanapotengana.
Wapenzi wasikilizaji, pamoja na hayo kama tulivyotangulia kusema ni kuwa, sadaka ambayo ni maarufu zaidi na ambayo imezoeleka baina ya wanadamu ni kutoa mali na fedha.
Miongoni mwa faida kubwa ya kutoa sadaka na kumsaidia mtu ni mhusika kupata baraka na kuongezewa katika mali aliyonayo. Yaani mtoaji sadaka na mwenye kutoa mali kwa ajili ya kuwasaidia wenye kuhitajia, hupata baraka na ongezeko katika mali na miliki alizonazo.
Aya ya 261 ya Surat al-Baqarah inazungumzia hili kusema:
Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyo chipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Mtume saw alikuwa akiwausia masahaba na Waislamu kwa ujumla kwamba, wajiongezee riziki zao kwa kutoa sadaka. Kuhusiana na hilo, Mtume saw anasema: Jiteremshieni riziki kupitia kutoa sadaka.”
Miongoni mwa faida nyingine za kutoa sadaka ni kwamba, mtu anapotekeleza suna hii nzuri hupata baraka, magumu yake huwa mepesi, huondolewa mabalaa na mitihani. Imam Jaafar Swadiq as anasema:
“Faida ya kutoa Sadaka ni kwamba inamsaidia kulipia madeni na vile vile kuongezea katika baraka.”
Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 104 ya Surat Tawba;
Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba ya waja wake, na anazikubali sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba na Mwenye kurehemu?
Aidha baadhi ya hadithi zinaonyesha kuwa, mpokeaji asili wa sadaka ni Mwenyezi Mungu.
Imam Swadiq as anasema: Mwenyezi Mungu amaesema kuwa, hakuna kitu isipokuwa nimekalifisha mtu wa kukipokea, isipokuwa sadaka ambayo ninaipokea mwenyewe. Hata mtu anayetoa sadaka ya tende moja au nusu yake, mimi huilea na kuiongezea kama vile mtu anavyomlea na kumkuza mtoto wake na Siku ya Kiyama tende hiyo moja au nusu yake itakuja ikiwa kubwa kama mlima wa Uhud au zaidi yake.
Kwa hakika hadithi hii inaonyesha adhama na umuhimu wa kutoa sadaka bila kujali ukubwa wa kile mtu anachokitoa hata kama kitakuwa ni kwa kiwango cha tende moja au nusu tende. Baadhi ya watu hudhani kwamba, ili kutoa sadaka na kumsaidia mwingine ni lazima mtu awe tajiri na mwenye mali nyingi. Aidha Imam Jaafar Swadiq as amenukuliwa akisema kuwa: Baba yangu (Imam Baqir as) alipokuwa akimpatia kitu muombaji, alikuwa akikuchukua tena baada ya kumpatia, halafu hukibusu na kisha kumrejeshea mwombaji. Hii ni kutokana na kuwa, sadaka kabla ya kufika katika mikono ya muombaji kwanza humfikia Mwenyezi Mungu.
Miongoni mwa baraka na faida nyingine za kutoa sadaka ni kuwa kinga ya balaa na matukio mabaya.
Kwa mujibu wa Mtume saw ni kuwa, sadaka huondoa balaa na ni dawa yenye kuponya. Vile vile sadaka huondoa kadhaa na ajali, na maumivu na maradhi hayaondoki isipokuwa kwa dua na sadaka.
Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Muadh bin Muslim anasema kuwa, siku moja nilikuwa kwa Imam Swadiq as kisha ikazungumziwa mauidhui ya ugonjwa na maumivu. Imam akasema, watibuni wagonjwa wenu kwa kutoa sadaka. Itakuwa vizuri kiasi gani kama kila mmoja wenu atatoa sadaka kwa kiwango cha mlo wenu mmoja. Kwa hakika Malaika wa mauti atakapoambiwa katoe roho ya mtu fulani, ataondoka na kwenda kutekeleza amri hiyo, lakini mara mja yule anapotoa sadaka na kumsaidia masikini na mwenye kuhitaji, Malaika wa mauti ataambiwa akhirisha amri ya kutoa roho ya mja huyo aliyetoa sadaka.
Kama mnavyojua kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, baadhi ya mambo ni yenye taathira kwa umri wa mwanadamu, yaani kwa maana kwamba, kwa kufanya au kujiepusha na mambo hayo, umri wa mtu hupungua au kuongezeka. Kutoa sadaka ni moja ya mambo ambayo hupelekea kuongezeka umri wa mtu na hivyo kumfanya awe na maisha marefu.
Imam Ali bin Abi Twalib as amenukuliwa akisema: Yeyote yule anayetumia kutoka mali yake katika njia ya kheri, basi Allah swt anamlipa mema humu duniani na kumwongezea katika malipo yake.”
Al Imam Ja'afar Swadiq as amenukuliwa katika Kitab ‘Uddatud-Da’i kuwa alimwuliza mtoto wake : “Je! nyumbani kuna kiasi gani kwa ajili ya matumizi?”
Naye alimjibu : “Zipo dinari arobaini tu.” Imam as alimwambia: “dinari zote hizo zitoe sadaka.”
Kwa hayo mtoto wake alimwambia Imam as: “Ewe Baba! Mbali na dinari hizi arobaini, hatutabakia na akiba yoyote.”
Imam as alimwambia: “Nakuambia kuwa zitoe dinari zote sadaka kwani ni Allah swt tu ndiye atakayetuongezea kwa hayo. Je! wewe hauelewi kuwa kila kitu kina ufunguo wake ? Na ufunguo wa riziki ni sadaka (kutolea mema).”
Kwa hayo, mtoto wake aliyekuwa akiitwa Muhammad, alizitoa sadaka dinari hizo na hazikupita siku kumi, Imam a.s. alitumiwa dinari elfu nne. Hapo Imam a.s. alimwambia mwanae : “Ewe Mwanangu! Sisi tulitoa dinari arobaini tu na Allah swt ametupa dinari elfu nne badala yake.”
Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa. Tukutane tena wiki ijayo, InshaAllah.