Hadithi ya Uongofu (86)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kama mnakumbuka, kipindi chetu cha juma lililopita kilijadili maudhui ya sadaka.
Tulisema kuwa, sadaka haiishi katika kutoa fedha na mali tu, bali hata kutenda wema na hisani, kumtembelea mgonjwa, kuitikia salamu, kutoa jiwe na miba katika njia wanayopita watu, kumuonyesha mtu njia na kadhalika ni mambo ambayo kwa mujibu wa Bwana Mtume saw yanahesabiwa kuwa ni kutoa sadaka katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 86 ya mfululizo huu kitazungumzia baadhi ya masharti ya kutoa sadaka. Kuweni nami hadi mwisgo wa kipindi hiki.
*******
Katika Aya za Qur’ani Tukufu na hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maasumina (as) kumebainishwa masharti na adabu za kutoa sadaka. Moja ya adabu za kutoa sadaka ambayo imetangulizwa mbele ya adabu na masharti mengine ni kwamba, sadaka inayotolewa inapaswa kuwa ni katika mali ya halali. Huu ni msingi muhimu wa kutoa sadaka ambao umechukuliwa kutoka katika aya ya 267 ya Surat al-Baqarah ambayo inasema:
Enyi mlio amini! Toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma, na katika vile tulivyo kutoleeni katika ardhi…
Mtume saw anaihesabu sadaka inayotolewa kutoka katika mali ya halali kwamba, ni yenye kukubaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu SWT. Mbora huyo wa viumbe amenukuliwa akisema kuwa:
Mtu ambaye ameichukua mali ya Muumini kwa dhulma na ghasbi, matendo yake mema na amali zake njema anazozifanya hazitiwi katika fungu la mambo yake mema, hadi pale atakapotubu na kurejesha mali aliyoighusubu kwa mwenyewe.
Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, mtu ambaye anatoa sadaka kutoka katika mali yake aliyoipata kwa njia za halali, Mwenyezi Mungu humpatia ujira mnono na mkubwa. Katika Qur’ani Tukufu, Mwenyezi Mungu ametaja aina mbili za sadaka. Mosi sadaka inayotolewa kwa siri na kificho na sadaka ya pili ni ile inayotolewa kidhahiri na wazi. Kila moja kati ya aina mbili hizi za sadaka ina athari na natija maalumu. Sadaka inayotolewa kwa dhahiri na wazi, lengo lake ni kuwashajiisha watu na kuwaita wajiunge katika amali hii njema na ya kupendeza. Imam Ali bin Abi Twalib as anasema: Sadaka ya dhahiri inafanya mali ya mtu kuongezeka.
Kwa hakika sadaka ya dhahiri mbali na kutoa wito kwa watu wengine wajiunge katika amali na jambo la kheri, huwa sababu na chimbuko la kuwaliwaza mafakiri na wasiojiweza. Hii ni kutokana na kuwa, watu hao hujihisi kwamba, katika jamii kuna watu wenye roho nzuri ambao wanawafikiria na hatua hiyo huwafanya wahisi kuliwazwa na kuwa na matumaini. Kiujumla ni kuwa, katika suala zima la kutoa sadaka iwe ni kwa dhahiri au kwa siri, kuna majimui ya masharti ambayo mtu anayetoa sadaka anpaswa kuyazingatia. Imam Jaafar Swadiq as anataja kanuni jumla kuhusiana na utekelezaji wa ibada mbalimbali likiwemo suala la kutoa sadaka na kusema kuwa:
Kila kitu ambacho Mwenyezi Mungu amekiwajibisha kwako, kukifanya kwa njia ya wazi ni bora kuliko kukifanya kwa siri na kwa kificho. Na kile ambacho amekifanya kuwa ni mustahabu, kukifanya kwa siri ni bora kuliko kukifanya kwa wazi na dhahiri.”Kwa mujibu wa hadithi hiyo, kutoa Zaka na Khumsi ambazo zinahesabiwa kuwa miongoni mwa sadaka za wajibu, zinapaswa kutolewa kwa wazi na sadaka ambazo ni suna na mustahabu zitolewe kwa siri kadiri inavyowezekana.
Katika hadithi nyingi kumeusiwa mno suala la kutoa sadaka kwa siri. Hii ni kutokana na kuwa, kufanya amali ya kheri kwa siri, ni mara chache kuwa na aria na hali ya kujionyesha. Aidha hatua hiyo hupelekea kuhifadhiwa heshima ya masikini na hivyo kumfanya asihisi madhila na uduni. Mmoja wa masahaba wa Imam Jaafar Swadiq as aliyejulikana kwa jina la Is’haq bin Ammar anasimulia kwamba, siku moja Imam aliniuliza, unatekeleza vipi suala la Zaka ya mali? Nikamwambia, huwapa khabari masikini waje nyumbani kwangu na kisha huwapatia haki yao. Imam Swadiq as akasema: Kitendo chako hiki kinaandaa mazingira ya waumini kuwa duni na dhalili. Ewe Is’haq chunga sana na jiepushe na amali hili. Kwani Mwenyezi Mungu SWT anasema: Mtu ambaye anamdhalilisha na kumdunisha rafiki miongoni mwa marafiki zangu, ameanzisha vita na mimi.
Katika hadithi hii tunajifunza nukta moja iliyoashiriwa nayo ni kwamba, wakati mwingine yamkini mtu fulani akawa ni muhitaji na akakubali kupokea sadaka ya dhahiri na mbele za watu, lakini kitendo hiki mbele ya macho ya watu humfanya ajihisi duni na hivyo kumfanya apate maudhi ya kiroho.
Moja ya masharti na adabu nyingine ya kutoa sadaka na kumsaidia mtu ni kwamba, jambo hilo halipaswi kuambatana na masimango na masimbulizi kwani kufanya hivyo hupelekea kubatilika sadaka hiyo. Mwenyezi Mungu anatahadharisha hilo katika aya ya 264 ya Surat al-Baqarah pale anaposema:
Enyi mlio amini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama anaye toa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyo chuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
Kimsingi ni kuwa, uzuri wa kutoa na kumsadia mtu ni kule amali hiyo kuambatana kwake na moyo mpana na maneno mazuri. Kwani kutumia maneno ya masimbulizi na masimango huzijeruhi hisia za mwombaji na mwenye kuhitaji. Hatua hiyo sio tu kwamba, huondoa athari na baraka za sadaka, bali jambo hilo linahesabiwa kuwa dhambi miongoni mwa madhambi makubwa.
Katika jamii tunazoishi kuna watu Mwenyezi Mungu amewajaali moyo wa kutoa na kusaidia watu, lakini tatizo lao kubwa ni ria au masimbulizi na masimango, hali ambayo hubatilisha amali zao hizo.
Mtume saw anasema kuhusiana na suala la sadaka kuambatana na masimango na maneno mabaya kwamba: Pepo ni haramu kwa mtu ambaye anatoa masimango na masimbulizi katika sadaka.
Katika suala la sadaka na kuwalisha watu, katu hakupaswi kuweko na hali ya kumdunisha fakiri.
Bwana mmoja alimuendea Bwana Mtume saw na kumwambia, ninataka kuwaalika na kuwalisha chakula masikini wote wa Madina. Mtume saw akamwambia: Kitendo hicho si kizuri. Kwa sababu wakati masikini hao watakapokaa katika kitanga kimoja cha chakula na kila mmoja kumuangalia mwenzake watajiona kwamba, wote ni masikini na hapo watafahamu kwamba, kitanga hicho cha chakula ni kwa ajili ya masikini na kwamba, amealikwa hapo kwa kuwa ni masikini, hali ambayo itawatia simanzi na majonzi. Bwana yule akamwambia Mtume saw, ewe mbora wa viumbe, basi niwaalike matajiri. Mtume akamwambia hapana, bali waalike masikini na matajiri kwa pamoja.
Adabu nyingine ya sadaka ni kutoa kitu kizuri kati ya unavyovimiliki. Watu wengine hukosea katika kutekeleza suna ya sadaka kwani kama ni nguo basi mtu hutoa katika zile nguo chakavu na ambazo hazitumii. Ilihali anaweza kutoa sadaka nguo nzuri na hivyo akawa ametekeleza vyema suna hii ya sadaka. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 92 ya Surat al-Imran kwamba:
Kabisa hamtafikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyo vipenda. Na kitu chochote mnacho kitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua.
Kwa msingi huo basi, uhakika wa kutoa sadaka ni pale mtu anapotoa katika mali yake anayoipenda, kwani katika Uislamu, sadaka haina maana ya kujaza tu tumbo la mwenye njaa au kumvisha asiye na nguo, bali kuilea roho ya mtoaji nalo ni jambo muhimu. Kwa hakika Uislamu unamtaka mtu atoe sadaka na kuwa na hisia ya kuguswa, ushirikiano na ukarimu pamoja na thamani nyingine za kimaadili na hivyo kupitia hayo ajilee na kukwea daraja za juu zaidi. Hili hufanikiwa kwa mtu kutoa sadaka kutoka katika mali yake kwa mkono wake mwenyewe. Imepokewa kuwa, mmoja wa maswahaba wa Mtume saw aliyekuwa na stoo kubwa ya tende aliusia kwamba, atakapokufa Mtume saw azichukue tende hizo zote za kuwapatia masikini. Baada ya kuaga duni, Mtume alitekeleza wasia wa swahaba wake. Wakati Mtume saw alipokuwa akimalizia tende ya mwisho alisema: Lau Bwana huyu angekuwa ametoa sadaka tende hii moja kwa mkono wake mwenyewe, lilikuwa ni jambo bora zaidi , kuliko mimi kuzigawa kwa masikini tende zote zilizoko katika ghala hili.
Wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu cha leo umefikia tamati. Tukutane tena wiki ijayo InshaAllah.