Sep 11, 2017 15:31 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (87)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya uongofu. Kipindi chetu cha juma lililopita kilizungumzia baadhi ya adabu na masharti ya kutoa sadaka.

Tulisema katika kipindi hicho kwamba, moja ya masharti muhimu katika kutoa sadaka ni kwamba, fedha au kitu kinachotolewa sadaka kinapaswa kuwa kinatokana na mali ya halali. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 87 ya mfululizo huu kitazungumzia moja ya suna na tabia nzuri za kutatua shida na matatizo ya watu nayo ni kukopesha au mkopo usio na riba. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.

Miongoni mwa amali njema na zinazopendwa katika Uislamu ambazo zinaweza kutatua matatizo ya mtu na kuufurahisha moyo wa mtu na wakati huo huo kumfurahisha Mwenyezi Mungu ni kumkopesha mtu au kumpa mkopo usio na riba. Suala la kukopeshana katika Uislamu lina umuhimu mkubwa kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu anaitaja hatua ya mtu kumkopesha mwenzake kwamba, ni sawa na kumkopesha Mwenyezi Mungu.

Kwa hakika kukopesha ni katika mifano ya wazi kabisa ya kutatua shida na haja za watu.

 

Kuhusiana na utukufu wa amali hii inayopendwa na Mwenyezi Mungu, Mtume saw amesema: Mtu ambaye atamkopesha ndugu yake Mwislamu, basi Mwenyezi Mungu atampatia mkabala wa kila dirihamu moja aliyoikopesha mambo mema sawa na uzito wa mlima Uhud, mlima Ridhwan na mlima Sinai na endapo atakuwa mwenye subira wakati wa kufuatilia kwa ajili ya kurejeshewa deni lake, basi Mwenyezi Mungu atampitisha katika njia ya Sirat kwa kasi kama umeme bila ya hesabu wala adhabu." Kwa hakika hadithi hii inaonesha fadhila kubwa za mtu kumkopesha ndugu yake Mwislamu ambaye ana shida na amekwama katika jambo fulani. Aidha Mtume (saw) anazungumzia kitendo cha mtu mwenye uwezo ambaye anajiwa na ndugu yake Mwislamu ili amkopeshe, lakini licha ya kuwa na uwezo wa kufanya hivyo huamua kutomtekelezea shida yake nduguye. Anasema: Mtu ambaye atajiwa na nduguye Mwislamu na hali ya kuwa ni mwenye shida, lakini licha ya kuwa na uwezo wa kumtekelezea shida hiyo akakataa kufanya hivyo, Mwenyezi Mungu humharamishia mtu huyo harufu ya pepo.

Imam Ja’afar Swadiq (as) anazungumzia fadhila za kumkopesha mtu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa kusema: Muumumini yeyote atakayemkopoesha Muumini mwenzake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kila lahadha sadaka ina thawabu, mpaka atakaporejeshewa mali yake.

Hata hivyo katika suala zima la kukopesha kuna nukta na sharti muhimu la kuzingatia nalo ni kwamba, mtu anayewakopesha watu anapaswa kufanya hivyo kwa nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Sharti jingine ni kwamba, pesa anayomkopesha mtu inapaswa kuwa inatokana na mali ya halali na anapomkopesha mtu anapaswa kufanya hivyo hali ya kuwa ni mwenye bashasha. Aidha mkopeshaji hapaswi kumkopesha mtu na wakati huo huo amali yake hiyo kuambatana na masimbulizi na masimango.

 

Kwa hakika mkopo humfanya mtu anayepokea mkopo kufanya hima na juhudi kwa ajili ya kulipa deni, ambapo hizo juhudi maradufu anazozifanya hupelekea kutokea ustawi wa kiuchumi na kuchanua vipaji katika jamii. Hata hivyo inasikitisha kwamba, katika jamii kuna watu huwa wako tayari kukopa deni wanapokuwa na shida, lakini kimsingi huwa hawana nia ya kulipa, au ulipaji wao huwa mgumu kiasi cha kupelekea mzozo na mvutano.

Mkopo na kukopesha ni miongoni mwa suna zilizotiliwa mkazo mno na Bwana Mtume saw. Kuna hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa mbora huyo wa viumbe  ambazo zinawashajiisha Waislamu juu ya kutekeleza suna hii. Aidha kuna hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume saw zinazoonyesha kwamba, Mtume saw anapenda kumkopesha mtu kuliko kutoa sadaka. Anasema: Dirihamu elfu moja kama nitaikopesha mara mbili, napenda zaidi kufanya hivyo kuliko kama nitaitoa sadaka mara moja.

Mtume Muhammad saw amewasisitizia mno Waislamu juu ya suala la kutatua shida na matatizo ya watu wengine na kutopuuza matatizo ya watu. Mtume saw anasema: Mtu ambaye anapenda Mwenyezi Mungu amuondolee ghamu na huzuni, basi anapaswa kulegeza kamba wakati wa kudai deni lake au asamehe deni lake hilo kwani Mwenyezi Mungu anapenda kusaidiwa watu ambao kutokana na kutokuwa na mali huwa ni wenye huzuni na ghamu.

Mtume saw alikuwa akiwashajiisha watu wenye uwezo kuwasaidia watu wenye matatizo ya fedha na wakati huo huo, alikuwa akiwataka watu wenye shida wajizuie kadiri wanavyoweza na suala la kukopa na wajikinge na Mwenyezi Mungu kwa mizigo ya madeni yenye kuumiza.

Katika mafundisho ya Uislamu kama ambavyo watu wanashajiishwa kuwa na subira na ustahamivu wakati wa kudai madeni yao waliyowakopesha watu wengine, mwenye kudaiwa pia anausiwa kutositasita na kuzembea katika kulipa deni la watu. Mtume saw analitambua suala la mtu mwenye uwezo wa kulipa deni la watu lakini anajizuia kufanya hivyo kwamba, ni dhulma.

Hadithi sahihi kadhaa zimetoa ahadi ya kupata thawabu na malipo makubwa mno kwa mtu anayempa mkopo mwenzake, huku zikitoa indhari ya adhabu kali kwa mwenye kuacha kufanya hivyo. Kwa upande mwingine ni kwamba, kuomba mkopo bila kuwa na mahitajio wala shida, ni mambo yanayoshusha daraja na hadhi ya mtu.

Kimsingi hasa ni kwamba, kila muumini anatakiwa ajitahidi kadiri iwezekanavyo asikope na kujitwisha mzigo wa deni. Kwa sababu mdaiwa hujihisi duni mbele ya mdai na kujihisi mtu duni na dhalili kunakinzana na dhati ya heshima ya mtu aliyopewa na Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Mbali na hayo mtu mwenye deni hupoteza utulivu wa kiroho na umakini wa kifikra, na bali si hasha akashindwa kufanya kazi kwa namna nzuri na chanya  ambazo zinahitajia utulivu wa kiroho. 

 

Usaliti, kama ulivyo wizi una sura tofauti. Aina moja ya usaliti ni mtu kukopa fedha, lakini akaacha kulipa bila ya sababu kuzilipa kwa wakati. Imepokewa kuwa mtu mmoja aliyekuwa akiitwa Abu Thumamah alimwambia Imam Jawad (as): “Ninataka kwenda Makka na Madina, lakini ninadaiwa. Imam Jawad (as) akamwambia: Kwanza lipa deni lako. Chunga sana usije ukafariki dunia na ukakutana na Mwenyezi Mungu huku ukiwa bado unadaiwa. Ikiwa unaweza kulipa deni lako lakini ukaamua kufanya ziara, hiyo itahesabika kuwa ni moja ya usaliti na muumini hafanyi usalit.” Katika hadithi hii tunajifunza kuwa, kupuuza kulipa deni, kunahesabika kuwa ni usaliti. Katika hadithi nyingine Mtume Muhammad (saw) amesema: “Kumsamehe mtu Mwislamu mwenye uwezo wa kulipa deni lake, ni kuwadhulumu Waislamu wengine.”

Katika Uislamu kuna suala jingine ambalo linausiwa pia katika suala la ukopeshaji nalo ni kuwa, mtu mwenye kumdai mtu anapaswa kumpa muda zaidi mdeni wake endapo anaona kuwa, anashindwa kulipa deni kutokana na kubanwa na hali ya kimaisha.

Kwa maana kwamba, wewe ambaye umemkopesha mtu unapoona hali ya ndugu yako huyo si nzuri na anaonekana kushindwa kulipa deni kwa sasa, hupaswi kumshinikiza na kumuweka katika mazingira magumu. Bali unapaswa kuidiriki hali yake na kumpa muhula zaidi.

Wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Tukutane tena wiki ijayo, siku na wasaa kama wa leo. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.