Alkhamisi Septemba 14, 2017
leo ni Alkhamisi 23 Dhulhija 1438 hijria sawa na Septemba 14, 2017
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita yani tarehe 23 Shahrivar mwaka 1357 Hijria Shamsia kulifanyika maandamano makubwa hapa nchini kuwaenzi mashahidi waliokuwa wameuawa na vibaraka wa Shah siku kadhaa kabla yake. Siku hiyo umati mkubwa wa watu ulimiminika katika makaburi ya Behest Zahraa mjini Tehran kuwaenzi mashahidi hao. Askari wa utawala wa Shah walikuwa na nia ya kuzuia maandamano hayo lakini umati mkubwa wa wananchi walioshiriki maandamano ulidumisha malalamiko yao dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah huko wakipiga nara za: “Iran ni nchi yetu na Khomeini na kiongozi wetu.”
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, hati ya Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ilitiwa saini na nchi za Iran, Saudia, Iraq, Kuwait na Venezuela. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na makampuni makubwa ya mafuta ya Magharibi ambayo yalikuwa yakisimamia uvumbuzi, uchimbaji na uuzaji wa bidhaa hiyo kimataifa na kuainisha bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa maslahi yao binafsi na kwa madhara ya nchi zalishaji. Licha ya kwamba awali jumuiya hiyo haikuwa na nguvu wala ushawishi wowote, lakini ilikuja kupata nguvu zaidi baada ya nchi kadhaa zikiwemo, Algeria, Libya, Nigeria, Qatar, Imarat, Gabon, Indonesia na Ecuador ambazo ni wazalisha wa mafuta kujiunga nayo.
Katika siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, moja kati ya ajali kubwa za moto ulimwenguni ilitokea katika mji mkuu wa Russia Moscow. Moto huo uliwashwa kwa makusudi. Ilikuwa imepita siku moja tu, tangu mji huo uvamiwe na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Napoleone Bonaparte, wakati mji huo ulipochomwa moto kwa amri ya mtawala wa wakati huo wa mji huo. Lengo la mtawala huyo lilikuwa ni kuyafanya majeshi ya Bonaparte yashindwe kustafidi na suhula za mjini humo katika kuendelea kubaki katika mji huo. Moto huo mkubwa uliteketeza na kuharibu kabisa robo tatu ya mji wa Moscow.
Siku kama ya leo miaka 628 iliyopita, utawala wa Othmania uliidhibiti na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Serbia. Tukio hilo lilijiri wakati wa operesheni za utawala huo za kuzitia katika miliki yake ardhi za Ulaya. Ushindi huo ulipatikana katika kipindi cha ufalme wa Sultan Murad wa kwanza Mfalme III wa utawala huo. Licha ya kuweko uasi wa wananchi wa Serbia, lakini ardhi yao iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Ufalme huo kwa karibu karne tano.
Na Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sheikh Abbas Qummi, aalimu na mpokeaji hadithi mtajika wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria katika mji mtakatifu wa Qum huko kusini mwa Tehran. Sheikh Abbas Qummi alianza kusoma elimu ya dini akiwa huko huko Qum na baadaye alielekea katika chuo kikuu cha kidini katika mji wa Najaf nchini Iraq ili kukamilisha masomo yake. Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Sheikh Abbas Qummi alipata elimu kutoka kwa maulamaa watajika wa hauza hiyo ya kielimu. Sheikh Abbas Qummi alirejea Iran baada ya muda ambapo alitumia muda wake wote kuandika vitabu na kufuatilia masuala ya kidini. Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwanazuoni huyo ni Mafatiihul Jinan na Manazilul Akherah.