Oct 01, 2017 02:33 UTC
  • Jumapili, Oktoba 1, 2017

Leo ni Jumapili tarehe 10 Mfunguo Nne Muharram 1439 Hijria, mwafaka na tarehe Mosi Oktoba 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya. Kung'ara na kudumu kwa mapambano ya Imam Hussein AS, kabla ya jambo lolote lile kulitokana na sifa zake za umaanawi wa kidini na kiutu. Mtukufu huyo AS alitangaza wazi kwamba lengo lake la kuanzisha mapambano hayo lilikuwa ni kuamrisha mema na kukataza mabaya pamoja na kuhuisha mafundisho na thamani za dini ya Mtume Mtukufu (saw). Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya. Baada ya kupambana kishujaa na jeshi hilo kubwa la Yazid, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi katika siku kama ya leo.

Mchana wa siku ya Ashura, Karbala baada ya kuuawa Imam Hussein (as)

Siku kama ya leo miaka 1372 iliyopita Ubaidullah Bin Ziyad, mtawala dhalimu na fasiki wa mji wa Kufa Iraq, na aliyehusika na umwagaji damu mkubwa katika mauaji ya Karbala, aliuawa na jeshi la Mukhtar al-Thaqafi. Katika siku ya Ashura mwaka 67 Hijiria, yaani miaka sita baada ya kujiri tukio la mauaji ya Karbala na katika siku sawa na ile aliyotoa amri kwa jeshi lake kumuua Imam Hussein na wafuasi wake,  naye (Ubaidullah Bin Ziyad) aliuawa na jeshi la Mukhtar chini ya kamanda Ibrahim Bin Malik al-Ashtar, katika pwani ya mto wa 'Khadhir' karibu na mji wa Mosul. Katika vita hivyo kati ya jeshi la watu wa Sham lililokuwa likiongozwa na Ubaidullah Bin Ziyad na jeshi la Mukhtar, majeshi elfu 70 ya Sham yalishindwa vibaya na Ibahim na kupelekea Ibn Ziyad kuangamizwa.

Siku kama ya leo miaka 333 iliyopita alifariki dunia Pierre Corneille mwandishi na malenga wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 78. Pierre alipenda sana kujifunza uandishi wa tamthiliya na akafanikiwa kusonga mbele katika fani hiyo. Alifahamika kwa lakabu ya baba wa uandishi wa tamthiliya wa Ufaransa na mwasisi wa tamthiliya ya kiwango cha juu yaani (Classic Theatre).

Pierre Corneille

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, lilitolewa tangazo la kuundwa rasmi Jamhuri ya watu wa Uchina na Mao Tse Tung akateuliwa kuwa rais wa nchi hiyo. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 16, China ilikuwa chini ya ushawishi wa serikali za Ulaya. Nchi hiyo ilipigana vita mara kadhaa ili kujiondoa katika makucha ya wakoloni wa Magharibi khususan mkoloni Muingereza.

Bendera ya China

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita katika siku kama hii ya leo yaani tarehe Mosi mwezi Oktoba mwaka 1960, Nigeria ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza. Wareno waliingia Nigeria katika karne ya 15 na karne iliyofuata wakaingia Waingereza. Aidha katika karne ya 17, Nigeria ilikuwa kituo muhimu cha biashara ya utumwa. Mwishoni mwa karne ya 19, wanajeshi wa Uingereza waliikalia kwa mabavu kikamilifu ardhi ya Nigeria. Ilipofika mwaka 1914, Uingereza ikaziunganisha nchi mbili zilizokuwa chini ya himaya yake yaani Nigeria ya kaskazini na kusini na kuunda koloni la Nigeria. Nigeria inapaka na nchi za Cameroon, Chad, Niger na Benin. 

Bendera ya Nigeria

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, Siraj Munir mtafiti wa Kipakistani aliaga dunia. Siraj Munir alitoa huduma kubwa katika kueneza lugha ya Kifarsi nchini Pakistan na kuwaarifisha shakhsiya mashuhuri wa fasihi, utamaduni na falsafa wa Kiirani. Mtafiti huyo wa Kipakistani alichapisha kitabu muhimu alichokipa jina la "Wazungumzaji wa Iran". Siraj Munir ni mmoja wa waasisi wa taasisi ya lugha ya Kifarsi nchini Pakistan. 

Siraj Munir

Na siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel ziliyashambulia makao makuu ya harakati ya ukombozi wa Palestina PLO huko Tunisia. Watu wasiopungua 70 waliuawa katika mashambulizi hayo na wengine wengi kujeruhiwa. Harakati ya PLO ilihamishia makao yake makuu nchini Tunisia kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni huko Lebanon mwaka 1982. 

Palestina

Tags