Ijumaa tarehe 6 Oktoba, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 15 Muharram 1439 Hijria sawa na Oktoba 6, 2017.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri aliuawa na maafisa kadhaa wa kundi moja la wanamapambano wa Kiislamu wa Misri lililojulikana kwa jina la al Jihad. Sadat aliuawa kwa sababu ya kutia saini makubaliano maovu ya Camp David mwaka 1978 na utawala wa Kizayuni wa Israel na akatambua rasmi utawala huo ghasibu na haramu. Kwa kitendo hicho Anwar Sadat alisaliti malengo ya Waislamu na Waarabu. Hatua hiyo ya Anwar Sadat ilipelekea kutengwa Misri miongoni mwa nchi za Kiislamu. Sababu hiyo iliyapelekea makundi ya Waislamu na wanamapambano wa Misri kumuuwa Sadat, ambaye walimuona kuwa ni msaliti mkubwa kwa kuutambua rasmi utawala wa maghasibu wanaoikalia kwa mabavu Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu wote duniani. Kiongozi wa mauaji hayo alikuwa Khalid Islambuli, aliyekuwa afisa katika jeshi la Misri.
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, vita vya nne kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel vilianza. Katika siku hiyo, jeshi la Misri lilifanya mashambulio ya kushtukiza dhidi ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu huko katika mfereji wa Suez na kufanikiwa kuingia katika jangwa la Sinai baada ya kuvunja kikosi cha ulinzi cha mstari wa mbele cha utawala wa Kizayuni . Vikosi vya Misri na Syria vililisababishia hasara kubwa jeshi la Israel katika vita hivyo ambapo ndege nyingi za utawala wa Kizayuni ziliangamizwa.
Tarehe 15 Muharram miaka 850 iliyopita alizaliwa Ali bin Mussa bin Ja'far maarufu kwa jina la Ibn Twaus, faqihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika eneo la Hillah nchini Iraq. Alipitisha kipindi cha utotoni katika mji huo na baadaye alihamia Baghdad ambako aliishi kwa kipindi cha karibu miaka 15. Ibn Twaus alipata umashuhuri mkubwa katika elimu na ucha-Mungu na ameandika vitabu vingi ambavyo ni marejeo ya taaluma za Kiislamu. Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni "Al Luhuf" ambacho ndani yake anazungumzia matukio ya Siku ya A'shura na harakati ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika medani ya Karbala, na katika uwanja huo hakina kifani.
Na miaka 1086 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Ibn Sakan mwanazuoni na mpokezi mashuhuri wa hadithi wa karne ya nne Hijiria. Alizaliwa mwaka 294 Hijiria huko Baghdad na alisafiri katika nchi mbalimbali kutafuta elimu. Ibn Sakan alikusanya hadithi nyingi katika miji mbalimbali na mwishowe akaweka maskani yake nchini Misri. Mpokezi huyo wa hadithi ameacha athari nyingi moja wapo ni kitabu cha historia kinachohusu maswahaba wa Mtume SAW, kinachoitwa al Hurufu fi al Swahaba.
