Jumamosi, Oktoba 7, 2017
Leo ni Jumamosi tarehe 16 Mfunguo Nne Muharram 1439 Hijria mwafaka na tarehe 7 Oktoba mwaka 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 179 iliyopita, hatimaye Abdul-Qadir al-Jazairi alitiwa mbaroni baada ya miaka 15 ya mapambano mtawalia dhidi ya Wafaransa. Miongoni mwa sababu za kushindwa Abdul-Qadir al-Jazairi ni kwamba, hakuwa na vituo vya mapambano ndani ya Algeria na maeneo yote ya ardhi ya nchi hiyo yalikuwa chini ya udhibiti wa Wafaransa. Ni kwa msingi huo ndio maana Abdul-Qadir al-Jazairi alilazimika kuendesha mapambano yake dhidi ya mkoloni Mfaransa katika maeneo ya mipaka ya nchi hiyo na Morocco. Hata hivyo, mtawala wa Morocco wakati huo ambaye naye alikuwa chini ya udhibiti wa Wafaransa alimzuia Al-Jazairi, kutumia maeneo ya mpakani ya nchi hiyo na akamtimua kutoka katika ardhi ya nchi hiyo. Abdul-Qadir al-Jazairi alifungwa jela kwa muda wa miaka 9 huko Ufaransa na baadaye aliachiliwa huru kwa sharti kwamba, asirejee nchini kwake. ***
Katika siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, Muhammad Ali Shah Qajar alitia saini kikamilisho cha Katiba. Kushadidi harakati ya kupigania Katiba nchini Iran na mapambano ya kila upande ya wananchi na viongozi wa kidini, Mozaffar ad-Din Shah Qajar alilazimika kukubaliana na matakwa ya wananchi ambapo mbali na mambo mengine alitoa amri ya kuundwa Bunge la Taifa. Awali Muhammad Ali Shah alikuwa akipoteza muda katika kusaidia kikamilisho hicho cha Katiba, lakini mashinikizo ya wananchi na wanazuoni yalimlazimisha katika siku kama ya leo alilazimika kutekeleza hilo. ***
Miaka 89 iliyopita katika siku kama ya leo, Sohrab Sepehri malenga na mchoraji wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Kashan moja ya miji ya katikati mwa Iran. Mwaka 1330 Hijiria Sepehri alitoa majimui ya kwanza ya tungo zake za mashairi zilizoitwa "Marge Rang" na akatoa tena majimui nyingine ya vitabu vinane. Aidha mbali na Sohrab Sepehri kuwa malenga mkubwa, alipendelea sana fani ya uchoraji. Miongoni mwa athari za Sepehri ni pamoja na majimui za vitabu vya mashairi viitwavyo "Zendegi Khob'ha", "Musafir" na "Aavaz Oftaab." Sohrab Sepehri alifariki dunia mwaka 1359 Hijiria na kuzikwa mahali alipozaliwa yaani mjini Kashan. ***
Katika siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, Ujerumani ya Mashariki iliasisiwa na kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia. Katika miezi ya mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Shirikisho la Umoja wa Sovieti liivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ujerumani ya Mashariki, na madola ya Magharibi yakadhibiti sehemu ya magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo baadaye Umoja wa Sovieti ulijitoa katika Baraza la Makamanda wa Waitifaki baada ya kutofautiana na madola ya Magharibi juu ya namna ya kuiendesha nchi hiyo.***
Na miaka 16 iliyopita katika siku kama ya leo, Marekani iliivamia Afghanistan. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington walihusika na tukio la Septemba 11 2001 nchini Marekani. Katika kipindi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden. Mashambulizi hayo mazito ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi. Hata hivyo pamoja na Marekani kusaidiwa na muungano wa vikosi vya kaskazini mwa Afghanistan na kufanikiwa kuuangusha utawala wa Taliban, hadi leo haijaweza kumtia mbaroni Mulla Omar na viongozi wengine wa kundi hilo la Taliban.