Oct 08, 2017 23:06 UTC
  • Jumatatu tarehe 9 Oktoba, 2017

Leo ni Jumatatu tarehe 18 Muharram 1439 Hijria sawa na Oktoba 9, 2017.

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, yaani tarehe 9 Oktoba 1962, nchi ya Uganda ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kuanzia mwaka 1890 Uganda ilikuwa chini ya makampuni ya Kiingereza yaliyokuwepo Afrika Mashariki, na baada ya kupita miaka kadhaa, ikatawaliwa rasmi na Uingereza. Baada ya kutawaliwa na mkoloni Muingereza, wananchi wa Uganda walipigania uhuru na hatimaye walifanikiwa kujipatia uhuru wao mwaka 1962 katika siku kama ya leo.

Bendera ya Uganda

Miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Ernesto Che Guevara mwanamapinduzi mashuhuri wa Amerika ya Latini pamoja na wenzake kadhaa. Che Guevara alizaliwa mwaka 1928 nchini Argentina. Fikra za Che Guevara za kuanzisha mapambano dhidi ya ubepari ilizidi kupanuka baada ya kushuhudiwa umaskini na ubaguzi uliotokana na siasa za kipebari za Marekani za kuyanyonya mataifa ya Amerika ya Latini. Ernesto che Guevara alikutana na Fidel Castro huko Mexico na viongozi hao wawili ndio walioongoza mapinduzi ya Cuba hadi kupatikana ushindi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Cuba mwaka 1959, Che Guevara alielekea Bolivia na kuasisi kundi la wapiganaji wa msituni. Alianza kupambana na serikali ya nchi hiyo iliyokuwa tegemezi kwa Marekani. Lakini katika siku kama ya leo mwaka 1967, wanajeshi wa Bolivia wakisaidiwa na shirika la ujasusi la Marekani CIA waligundua maficho ya Che Guevara na kumuuwa kwa kummiminia risasi.

Ernesto che Guevara

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, Majid Abu Sharar, shakhsiya mwingine wa Palestina aliuawa na utawala haramu wa Israel nchini Italia. Abu Sharar ambaye alikuwa afisa wa kampeni wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO aliuawa na vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mosad mjini Roma, Italia. Israel imekuwa ikitumia njia ya kuwauwa kigaidi shakhsiya mbalimbali wa Palestina kama moja ya njia zake kuu za kusitisha mapambano ya ukombozi ya Wapalestina.

Majid Abu Sharar

Siku kama ya leo, miaka 146 iliyopita alizaliwa Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli, alimu mkubwa na mtaalamu wa fiqhi mjini Kabul, Afghanistan. Akiwa kijana mdogo Allamah Sardor Kabuli alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa enzi hizo kama vile, Mirza Hussein Nuri na Sayyid Swafiyyud-Din Hassan bin Hadi Kadhimi, sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwa maulama na maraajii watajika kama vile, Sayyid Hassan Sadr naHaji Sheikh Abbas Qumi, ambapo pia alipata ijaza (idhini) ya kunakili na kuandika riwaya na hadithi. Mwaka 1310 Hijiria, Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli alielekea mjini Kermanshah, Iran na kujishughulisha na ufundishaji kwa wakazi wa mji huo sanjari na kuandika vitabu kadhaa. Aidha msomi huyo alipata kusomea lugha kadhaa za dunia, kama vile Kiarabu, Kingereza, Kiebrania na Urdu. Kitabu cha ‘Tarjama ya Injili ya Barnaba’ na ‘Hadithi 40 katika fadhila za Amirul-Muuminin’ ni miongoni mwa athari za msomi huyo. Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli alifariki dunia mwaka 1372 Hijiria, akiwa na umri wa miaka 79 na kuzikwa mjini Najaf, Iraq.

Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli,

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Msomi huyo alibakia mjini Tehran hadi mwishoni mwa uhai wake na baada ya kufariki dunia akazikwa mjini Qum.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari