Jumapili 29
Leo ni Jumapili tarehe tisa Swafar 1439 Hijria, sawa na tarehe 29 Oktoba, 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1402 iliyopita, kulingana na kalenda ya Hijria, aliuawa shahidi Ammar bin Yassir, sahaba mkubwa wa Mtume Muhammad (saw) na msaidizi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Ammar bin Yasir aliuawa katika vita vya Siffin vilivyojiri kati ya majeshi ya Imam Ali (as) na Muawiya bin Abi Sufian. Ammar alizaliwa miaka 57 kabla ya Hijra ya Mtukufu Mtume na wazazi wake wawili, yaani Yassir na Sumayyah, ndio waliokuwa mashahidi wa kwanza katika Uislamu. Sahaba huyu mtukufu alisimama imara dhidi ya maudhi ya makafiri na alishiriki katika vita mbalimbali pamoja na Bwana Mtume (SAW). Wakati mmoja Mtume alimwambia Ammar: "Ewe Ammar! Baada yangu kutatokea fitina, na katika hali hiyo mfuate Ali bin Abi Twalib na kundi lake, kwani Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali.
Siku kama ya leo miaka 1018 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Maskawayh, mtaalamu, mwanahistoria na mwanafikra mkubwa wa Kiislamu. Miskawayh alizaliwa mnamo mwaka 320 katika mji wa Rei ulio karibu na mji mkuu wa Iran, Tehran ya sasa. Miskawayh alikuwa mwalimu katika kila elimu ya zama zake sambamba na kufanya utafiti katika elimu ya tiba, kemia, historia na falsala. Miongoni mwa athari zilizobakia za Abu Ali Miskawayh ni pamoja na kitabu kinachoitwa "Tahdhibul-Akhlaq", "Tajaarubul-Umam" na "Jaavidaan Kherad."
Siku kama ya leo miaka 844 iliyopita yaani tarehe tisa Swafar mwaka 595, alifariki dunia Ibn Rushdi Andalusi, msomi mkubwa wa falsafa na muhadhiri mtajika wa Kiislamu. Abul-Walid Muhammad Bin Ahmad Bin Rushdi, maarufu kwa jina la Ibn Rushdu, mmoja wa wasomi wakubwa wa elimu ya falsafa wa Kiislamu katika karne ya sita Hijiria, alikuwa pia mtaalamu katika elimu za fiqhi, hadithi, fasihi, mantiki na elimu nyingine za wakati huo. Wakati akiishi Andalusia (Uhispania ya leo) alikuwa mtu wa karibu na mfalme na mmoja wa makadhi wa eneo moja la utawala wa kifalme. Ameacha vitabu vingi kikiwemo cha 'Bidaayatul-Mujtahid' 'Falsafatu Ibn Rushdi' na 'al-Kulliyaat'.
Siku kama ya leo miaka 234 iliyopita alifariki dunia Jean le Rond d'Alembert, mtaalamu wa hisabati wa Ufaransa. Rond d'Alembert alizaliwa mjini Paris tarehe 15 Novemba mwaka 1717 Miladia. Pamoja na hayo baba na mama yake walimtelekeza kando na kanisa moja la mjini Paris. Kuanzia wakati huo alilelewa na mwanamke mmoja mchuuzi wa mji huo na kuanza kumpatia mafunzo mbalimbali kama mtoto wake. Akiwa na miaka 22 aliandika makala kuhusiana na masuala ya hesabu na baada ya hapo akaanza kupata umashuhuri. Miaka kadhaa baadaye aliendeleza kazi zake za kielimu na kuwasilisha mbinu mpya ya kimahesabu ambayo ilikuwa na jibu kwa kila muamala wa Aljebra. Hata kama Jean le Rond d'Alembert alifanya juhudi kubwa kuvumbua mbinu hiyo, lakini ilikuja kuthibitishwa kwa mara ya kwanza miaka 16 baadaye akiwa amekwishafariki dunia. Msomi huyo alifariki dunia Oktoba 29 1783 Miladia akiwa na umri wa miaka 66.
Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita, mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri uliasisiwa nchini Uturuki kwa uongozi wa Rais Mustafa Kemal mashuhuri kwa jina la Ataturk. Kemal Ataturk aliiongoza kidikteta nchi hiyo kwa muda wa miaka 15 na kufanya hujuma za kufuta sheria, nembo pamoja na matukufu ya Kiislamu na wakati huo huo, kueneza utamaduni na nembo za Kimagharibi nchini humo. Hata baada ya kufariki dunia kiongozi huyo aliyekuwa na uadui na Uislamu mnamo mwaka 1938, njama hizo dhidi ya Uislamu nchini Uturuki ziliendelezwa na wafuasi wake.
Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita alifariki dunia Léon Charles Albert Calmette mgunduzi wa chanjo ya BCG. Albert Calmette alikuwa tabibu mtajika na mahiri wa Kifaransa ambaye alihitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Paris. Chanjo ya BCG hutumika kukinga maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu au TB. Kugunduliwa chanjo hiyo kumepunguza vifo vya watu wanaopatwa na ugonjwa wa TB duniani.
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, askari jeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia Peninsula ya Sinai huko Misri. Mashambulio hayo yalianza baada ya Rais wa wakati huo wa Misri Gamal Abdul Nassir kutaifisha mfereji wa Suez. Siku mbili baada ya mashambulio hayo, Uingereza na Ufaransa zilipeleka majeshi yao pembezoni mwa mfereji huo kwa lengo la kuusaidia utawala ghasibu wa Israel. Mnamo mwaka 1957 majeshi vamizi ya Ufaransa, Uingereza na utawala haramu wa Israel yaliondoka katika ardhi ya Misri kufuatia mashinikizo ya fikra za waliowengi, madola mengi ya Magharibi na upatanishi wa Umoja wa Mataifa.
Na siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, katika jinai yao nyingine, Wazayuni waliwauwa kwa umati wakazi wa kijiji cha Kafr Qasim huko Palestina na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kutangaza utawala wa kijeshi katika kijiji hicho. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni waliwauwa kwa umati wanaume, wanawake na watoto madhlumu wa Palestina wasiopungua 49 na kujeruhi makumi ya wengine katika kijiji hicho cha Kafr Qasim.