Nov 21, 2017 02:48 UTC
  • Jumanne 21 Novemba, 2017

Leo ni Jumanne tarehe Pili Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na tarehe 21 Novemba mwaka 2017.

Katika siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza na kuiainisha siku hii ya tarehe 21 Novemba kuwa Siku ya Kimataifa ya Televisheni. Lengo la Umoja wa Mataifa la kuianisha siku hii lilikuwa ni kuweko mabadilishano ya vipindi vya runinga hususan vipindi vinavyotayarishwa kwa lengo la kueneza amani, ustawi wa kijamii, kiuchumi na kuimarisha masuala ya kiutamaduni ya jamii. 

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, Butros Butros Ghali alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa sita wa Umoja wa Mataifa. Butros Ghali alizaliwa mwaka 1922 katika familia ya Kikristo katika mji mkuu wa Misri Cairo. Baada ya kumaliza masomo yake Butros Butros Ghali alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Siasa cha Cairo. Mwanadiplomasia huyo ndiye aliyemshawishi na kumshajiisha Anwar Sadat Rais wa zamani wa Misri kutia saini mkataba wa Camp David mwaka 1978 na katika kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel.

Butros Butros Ghali

Miaka 234 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Novemba mwaka 1783, kwa mara ya kwanza katika historia ya jitihada za mwanadamu za kupaa angani, puto lilitumwa angani. Puto hilo lilikuwa limepandwa na watu wawili mmoja akiwa mwanafizikia wa Ufaransa aliyejulikana kwa jina la Pilatre De Rozier. Tangu alipokuwa masomoni De Rozier alikuwa akifikiria kutengeneza wenzo wa kupaa angani na kwa kutengeneza puto hilo mwanafizikia huyo akawa amefanikiwa kuruka angani.

De Rozier

Siku kama ya leo miaka 809 iliyopita, aliaga dunia Ibn Athir Jazari, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na mpokezi mkubwa wa hadithi. Ibn Athir alizaliwa mwaka 555 Hijria huko Iraq na kujifunza taaluma mbalimbali. Alipata umashuhuri katika masuala ya lugha na fasihi ya Kiarabu. Kitabu maarufu zaidi cha Ibn Athir ni al Kamil fi Tarikh. Kitabu kingine cha mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ni Usdul Ghabah Fi Ma'rifatis Sahabah ambacho kinaeleza wasifu wa masahaba 7500 wa Mtume Muhammad (saw).

 

Tags