Nov 21, 2017 06:35 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (89)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami tena Salum Bendera katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichotangulia kilizungumzia maudhui ya kutoa adia na zawadi na umuhimu wa jambo hilo katika Uislamu.

Tulisema kuwa, adia au zawadi kama itatolewa kwa nia njema, safi na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi huwa na athari nyingi chanya kwa mtoa zawadi na mpokeaji wa zawadi hiyo na matokeo yake ni kupatikana furaha na buraha. Aidha tuliashiria kwa mukhtasari, falsafa na siri ya kupeana zawadi ambayo tulisema ni kujenga mapenzi na kuondosha chuki, uadui na vinyongo. Kipindi chetui cha leo ambacho ni sehemu ya 89 ya mfululizo huu kitazungumzia na kujadili suala la kukaa kimya na kutozungumza isipokuwa kwa haja na kwa dharura. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Moja ya tabia na sifa ya kimaadili inayopendeza na ambayo imetiliwa mkazo na kukokotezwa mno katika hadithi mbalimbali zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume saw na Maimamu watoharifu as ni kukaa kimya. Hata hivyo kunyamaza kunakokusudiwa hakuna maana ya kutozungumza kabisa, la hasha bali ni kunyamaza na kuzungumza pale inapolazimu na sio kuzungumza kila wakati na kuchangia kila mada na maudhui. Mtume Muhammad saw amenukuliwa akisema kuwa, wakati unapomuona Muumini amenyamaza kimya, msogelee ili akupatie hekima na elimu.

Kwa hakika ulimi ni miongoni mwa viungo muhimu mno katika mwili wa mwanadamu. Ulimi hubainisha na kueleza kile kilichomo katika akili na fikra za mtu na hata kuweka wazi shakhsia ya mhusika. Wakati mtu anapoanza kuzungumza kimsingi ni kuwa hudhirisha kile ambacho kimejificha katika fikra zake na kukitoa katika hali ya batini na kukidhihirisha. Kwa hivyo, basi kunyamaza na kuchunga ulimi usizungumze mambo yasiyo na maa husaidia mtu katika kulinda na kuhifadhi shakhsia ya mtu.

Imam Muhammad al Baqir AS

 

Imam Muhammad Baqir (as) anautambua ulimi kwamba ni miongoni mwa viungo muhimu mno katika mwili wa mwanadamuu na anasema:  Kwa hakika ulimi ni ufunguo wa mazuri na mabaya yote, hivyo ni jambo linalofaa kwa Muumini kuuchunga na kuulinda ulimi wake kama anavyochunga na kulinda mfuko wake wa dhahabu na fedha.

Kwa hakika kunyamaza humfanya mtu aokoke na kuepukana na madhambi mengi na natija ya hilo kuwa ni ufunguo wa kuingia peponi. Mmoja wa Masahaba wa Mtume saw anasimulia kwamba, siku moja Mtume saw alimwambia, je nikuonyeshe kitu ambacho kupitia kwacho Mwenyezi Mungu atakuingiza peponi? Nikamwambia, ndio ewe Mtume wa Allah. Anasema, Mtume akamtaka atoe katika njia ya Mwenyezi Mungu amsaidie aliyedhulumiwa na atoe msaada kupitia kutoa ushauri. Kisha akamwambia: Chagua kunyamaza, na zungumza pale tu unapopoona maneno yako ni mazuri.

Moja ya athari chanya za kunyamaza kimya, ni kujipamba na hali ya hadhi na heshima. Imekuja katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Ali bin Abi Twalib as ya kwamba amesema: Kukaa kimya hukuvalisha vazi la heshima na kukuondolea tatizo la kuomba msamaha.

Kwa hakika mtu ambaye anazungumza sana bila shaka huwa na makosa mengi. Makosa hayo hupunguza heshima na hadhi yake mbele ya macho ya watu na wakati huo huo kumfanya alazimke kuomba msamaha mara kwa mara.

Aidha Imam Ali bin Abi Twalib (as) amenukuliwa akisema kuwa, heshima na hadhi ya mtu huongezeka kwa kukaa kimya, mtu kuwa na insafu na uadilifu humfanya apate marafiki wengi, kwa kusamehe daraja ya mtu huongezeka, kwa unyenyekevu neema hukamilika, kwa kulipa gharama ukubwa wa mtu huthibitika, kwa kutumia mbinu za kiadilifu mtu huwashinda maadui zake na kwa kuwa na subira mbele ya jambo lisilo la hekima na busara mtu hupata wafuasi wengi.

Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as) anauhesabu ukimya na kukaa kimya kwamba ni katika alama za usomi. Anasema: Alama za usomi na ujuzi ni tatu: Kuwa na subira, elimu na ukimya.

Kwa hakika ukimya ni mlango miongoni mwa milango ya hekima ambayo inalela mahaba na ni muongozo wa mema na mambo yote mazuri.

Mwanadamu anapaswa kufikiri kwa makini kila anapotaka kusema jambo na kuyatia katika mzani maneno anayotaka kuyasema sambamba na kufikiria natija ya maneno hayo. Endapo neno analotaka kulisema halina matokeo mazuri basi anapaswa kunyamaza kimya na kutolitoa kinywani mwake.

Bwana mmoja katika zama za Mtume saw alimuendelea mbora huyo wa viumbe na kumwambia: Niambie mambo kuhusiana na Uislamu na maamrisho yake ambayo kama nitayafanyia kazi, bazi sitakuwa na haja tena ya kuwauliza watu wengine.

Muhammad SAW Mtume wa Mwenyezi Mungu

 

Mtume saw akasema: Muamini Mwenyezi Mungu na uwe imara katika imani yako. Bwana yule anasema: Nikamuuliza Mtume saw: Nijilinde na kitu gani? Mtume saw akaashiria ulimi wake. Yaani uogope ulimi wako na uudhibiti.  Kwa hakika katika maisha yetu tuyaoishi tunashuhudia katika jamii jamii jinsi neno moja lililosemwa na mtu kumhusu mtu fulani linavyoweza kuzua ugomvi, vurugu na tafrani na hata kuharibia uhusiano baina ya mtu na mtu na matokeo yake kutawala vinyongo na kuchukiana. Hii ni katika hali ambayo aliyesema neno lile laiti kama angeuzuia ulimi wake, kutotamka neno au angenyamaza kimya basi ugomvi na kuharibika uhusiano baina ya mtu na mtu au hata wanafamilia na marafiki usingetokea.

Hata hivyo madhumuni ya kunyamaza na kukaa kimya yanayokusudiwa katika hadithi zinazotaka watu wakae kimya, sio kwamba, mtu akae kimya mutlaki na kuzungumza neno katu hata kuhusiana na kudai na kupigania haki yake, haki za wengine au kutoa muongozo na ushauri. La hasha, makusudio ya kukaa kimya na kutozungumzia ni kutozungumza maneno yasiyo na maana, yasiyofaa na ambayo huenda yakawa na matokeo mabaya.

Kuna watu wakiwa na lengo l;a kujionyesha mbele za watu wengine huwa wako tayari kuzungumzia na kutoa maoni hata katika mambo ambayo hawana elimu na ujuzi na mambo hayo.

Kwa msingi huo, watu wa aina hiyo hutumbukia katika makosa. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana, mafundisho ya Uislamu yanawataka watu kutotoa maoni au kuzungumzia mambo ambayo hawana elimu nayo.

Imam Ja'afar Swadiq (as) anasema kuwa: Mtu ambaye anakaa kimya huwa amesalimika na kukosea na kuteleza.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo nalazimika kukomea hapa kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki. Tukutane tena wiki ijayo siku na wakati kama wa leo. Wassalaamu Alaykum Warahmtullahi Wabarakaatuh.....