Hadithi ya Uongofu (90)
Ni wasaa na wakati mwingine wa kuwa nanyi wapenzi wasikilizaji katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia suala la kukaa kimya na kutozungumza pamoja na faida zake. Tulisema kuwa, miongoni mwa faida za kukaa kimya na kutozungumza isipokuwa mtu anapoona kwamba, maneno yake yatakuwa na faida ni kuokoka na madhambi mengi na kwamba, hatua ya kukaa kimya ni ufunguo miongoni mwa funguo za peponi.
Katika sehemu ya 90 ya mfululizo huu juma hili tutazungumzia suala la kuhifadhi na kulinda heshima ya Muumini. Kuweni nami katika dakika hizi chache ili kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.
Moja ya mafundisho muhimu ya dini tukufu ya Kiislamu ni udharura wa kulinda na kuhifadhi heshima ya watu wengine. Jambo hili ni muhimu kiasi kwamba, hatua ya mtu kuharibu heshima ya wengine inahesabiwa kuwa miongoni mwa madhambi makubwa kabisa na Mwenyezi Mungu ameahidi kumpatia adhabu kali yule anayevuruga na kuharibu heshima ya wengine.
Imam Jaafar Swadiq (as) anazungumzia umuhimu wa jambo hili kwa kusema: Kila ambaye atasema jambo na lengo lake likawa ni kudhihirisha mabaya na kuharibu heshima ya Muumini, Mwenyezi Mungu atamuondolea Wilaya yake kwake na kumfanya shetani kuwa msimamizi wake.
Heshima maana yake ni hadhi na itibari ya mtu. Dini tukufu ya Kiislamju imetilia mkazo mno suala la kulindwa na kuhifadhiwa heshima, hadhi na shakhsia ya waumini. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana tunaona kuwa, miongoni mwa maamrisho muhimu ya Uislamu ni kulinda na kuhifadhi heshima na hadhi ya wengine ambapo mtu anapaswa kutumia kila wenzo kulinda na kuhifadhi heshima na hadhi ya Muumini.
Wakati mwingine mwanadamu anapaswa hata kusamehe mali yake kwa ajili ya kulindfa hadhi na heshima yake. Mtume Muhammad (saw) amenukuliwa akiwataka watu watuimie mali yao kulinda na kutetea hadhi na heshima yao. Kwa mujibui wa maneno hayo ya Bwana Mtume (saw) inafahamika wazi kwamba, hadhi na heshima ya mtu ni bora zaidi kuliko hata mali na utajiri wake.
Wakati mwingine mwanadamu anapaswa kujiepusha na mijadala na mivutano ambayo yumkini ikashusha hadhi na heshima yake. Hii ni kutokana na kuwa mijadala na mizozo hufungua milango ya mtu kudhalilishwa na kudunishwa. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib (as) anawausia Waislamu kwa kuwaambia: Kila ambaye anataka kulinda hadhi na heshima yake, anapaswa kujiepusha na kurushiana maneno. Aidha Imam Hassan bin Ali al-Mujtaba (as) analihesabu suala la kulinda heshima na hadhi kwamba, ni miongoni mwa ishara za hekima na busara. Anasema: Safihi na mtu asiye na hekima wala busara ni yule ambaye anatumia kijinga mali yake na mwenye kupuuza heshima na hadhi yake.
Katika dini ya Kiislamu moja ya mambo ambayo yametajwa kuwa ni sababu na chimbuko la uzima na usalama wa jamii ni kulindwa roho, mali na heshima za watu hususan waumini. Hii ni kutokana na kuwa, hadhi na heshima ya mtu ambayo ni matunda ya umri wa maisha na ambayo imepatikana kwa juhudi na tabu kubwa yumkini ikapotea na kusambaratika kwa lahadha moja na ndio maana hakuna dhambi kubwa kama ya kuharibu heshima na itibari ya Mwislamu.
Ni kwa kuzingatia uhakika na ukwedli huo ndio maana katika Uislamuu kukakatazwa na kupigwa marufuku amali na kitendo chochote ambacho kinapelekea kuharibu heshima na itibari ya muumini na hivyo kumdhalilisha na kumdunisha. Uislamu umezuia na kuklataza kwa nguvu zake zote mtu kufanya kitendo ambacho kitapelekea kumdhalilisha na kumdunisha ndugu yake muumini. Mtume (saw) amenukuliwa akisema kuwa:
Mwenyezi Mungu mtukufu amaesema kuwa, kila ambaye atamadunisha na kumdhalilisha rafiki miongoni mwa marafiki zangu ametangaza vita na mimi. Imam Muhammad al-Baqir (as)m anasema kuwa: Katika usiku ambao Bwana Mtume (saw) alifanya safari ya Miraji, alimuuliza Mwenyezi Mungu: Muumini ana thamani gani mbele yako? Alijibiwa kwa kuambiwa: Ewe Muhammad! Kila ambaye anamdhalilisha na kumvunjia heshima rafiki yangu, basi ni kana kwamba, amesimama kupambana na mimi; na mimi nitaharakisha kwenda kuwasaidia marafiki zangu.
Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Abu Basir anasimulia kutoka kwa Imam Muhammad al-Baqir (as) ya kwamba, alimuuliza: Mmoja kati ya wafuasi wetu ni masikini na mimi ninataka kumpatia yeye Zaka yangu, lakini Bwana huyu anaona haya na aibu kupokea Zaka. Je kuna ulazimja nimwambie kama Zaka hii ni ya mali? Imam akajibu Abu Basir kwa kumwambia:
Tekeleza amali ambayo Mwenyezi Mungu amekuwajibishia, lakini usimadhalilishe Muumini. Kwa upande wake Imam Ja'afar Swadiq (as) anazungumzia suala la kulindwa na kuhifadhiwa heshima na itibari ya Muumini kwa kusema: Kila ambaye katika nyinyi ataweza kukutana na Mwenyezi Mungu hali ya kuwa mikono yake haijatapakaa damu wala mali ya Waislamu na ulimi uliosalimika na kuharibu heshimu na itibari ya Waislamu basi anapaswa kufanya hivyo.
Qur'ani Tukufu imezungumzia katika aya mbalimbali suala la utukufu na umuhimu wa Kaaba, kibla cha Waislamu. Ni kwa kuzingatia hilo, ndio maana ni wajibu kuiheshimu al-Kaaba na kuivunjia heshima Nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu ni haramu na klunahesabiwa kuwa ni dhambi kubwa. Lakini tukirejea riwaya na hadithi mbalimbali tunapata kuwa, sio tu kwamba, kumheshimu Muumini na kutomvunjia heshima na itibari yake hakujaweka katika kiwango kiwango kimoja na heshima kwa al-Kaaba, bali kwa mujibu wa Imam Ja'afar as ni kuwa, heshima na itibari ya Muumini iko juu zaidi ya heshima ya Kaaba. Hivyo basi kama ambavyo ni haramu kuivunjie heshima Kaaba, kuharibu haiba na heshima ya Muumini na kumdunisha ni haramu pia.
Tunakiamilisha kipindi chetu cha juma hili kwa kuashiria nukta moja muhimu nayo ni kwamba, Mwenyezui Mungu amejuzisha suala la mtu kufanya kila awezalo kurejesha hadhji na heshima yake iliyoharibiwa na mtu au watu fulani kutokana na kutuhumiwa kwa jambo ambalo hakuulifanya.
Kisa cha Nabii Yusuf (as) cha kufungwa jela kwa tuhuma ambayo hakufanya na jinsi Mtume huyo wa Allah alivyoukataa msamaha wa mheshimiwa wa Misri wa kuachiliwa huru jela kabla ya kuhakikisha kwamba, anarejeshewa heshima na itibari yake iliyoharibiwa, ni funzo na mfano mzuri kabisa wa mtu kufanya juhudi za kupigania kurejeshewa hadhi na itibari yake.
Nabii Yusuf hakuwa tayari kuufurahia na kuukubali msamaha wa Azizi na mheshimiwa wa Misri wa kuachiliwa jela mpaka afutiwe tuhuma na kurejesherwa hadhi na itibari yake iliyoharibiwa. Kwa msingi huo, mheshimiwa wa Misri akaitisha kikao maalumu kwa ajili ya jambo hilo na baada ya Nabii Yusuf kuvuliwa tuhuma na kuurejeshewa heshima na itibari yake, akaridhia kutoka jela. Hivyo basi, Muumini anapaswa kusimama kidete na kutokubali hadhi na heshima au itibari yake iharibiwe.
Kutokana na kumalizika muda wa kipindi chetu kwa juma hili, sina budi kukomea hapa kwa leo, nikitaraji kwamba, mtajiunga nami wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Wasaalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.