Nov 21, 2017 06:46 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (92)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia suala la dhulma na tuliashiria jinsi mafundisho ya Kiislamu yalivyokataza kudhulumu na kuwataka watu waipinge na kuikataa dhulma vyovyote iwavyo.

Tuliona pia jinsi dhulma ilivyogawanyika katika sehemu kadhaa. Aidha tulisema kwamba, katika mafundisho ya Kiislamu mbali na dhulma kukatazwa na watu kutakiwa wajiepushe na kutenda dhulma, wanapaswa pia kutomsaidia dhalimu na wala kutoridhia dhulma. Tulisisitiza kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu anayetenda dhulma, anayemsaidia na anayeridhia dhulma wote watatu ni washirika. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 92 ya mfululizo huu kitajadi maudhui ya msamaha na kusamehe katika Uislamu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

******

Moja ya sifa njema za kimaadili na zinazopendwa katika Uislamu ni kusamehe makosa ya wengine. Kusamehe, sifa ambayo muumini anapaswa kujipamba nayo ni moja ya ukamilifu wa kibinadamu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 40 ya Surat Shuura:

Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe, na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.

Mtume saw anakutambua kusamehe kuwa ni alama ya ukubwa, izza na heshima. Mbora huyo wa viumbe amenukuliwa akisema kuwa: Hongera ziwe kwenu kutokana na kusamehe! Kusamehe huongeza izza ya mja. Basi sameheaneni ili Mwenyezi Mungu akupeni izza na heshima.

Muhammad Rasulullah

 

Katika maisha tunayoishi kuna wakati hujitokeza ugomvi na vinyongo baina ya watu. Endapo hali hii ya vinyongo itaendelea, huyafanya mahuasiano ya watu kuwa baridi na kwa muktadha huo kutawala hali ya mifarakano na vitendo visivyo laiki katika jamii.  Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana kuna haja ya kutumia mantiki na njia sahihi kwa ajili ya kumaliza hitilafu na hali ya kupishana iliyojitokeza baina ya watu wawili au kundi fulani na kundi jingine katika jamii; na hivyo kutotoa nafasi kwa vinyongo kutawala, hali ambayo bila shaka haina mwisho mwema kati ya mahusiano ya mtu na mtu au watu fulani na kundi la pili. Moja ya njia za kuondoa hilo ni kusamehe. Kuvumilia makosa na hali ya kuteleza ya watu wengine, ni hatua njema ambayo huondoa vinyongo, chuki na uadui, na hata kuwafanya maadui kuwa marafiki.

Katika kisa cha Nabii Yusuf as na nduguze tunaona jinsi ndugu zake walivyomfanyia husuda, uadui na mambo mabaya kabisa hata wakafikia kumuuza kwa thamani duni kama inavyoashiria aya ya 20 ya Surat Yusuf: Na wakamuuza kwa thamani duni, kwa akali ya pesa. Wala hawakuwa na haja naye.

Vitendo vya ndugu zake Yusuf vilifikia kumuudhi pia baba yao yaani Nabii Yaaqub as. Lakini mwisho wa siku, wao ndio walioumbuka na kujihisi duni na wakosa mbele ya Yusuf ambapo walisema: Wakasema: Wallahi! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha wewe kuliko sisi, na hakika sisi tulikuwa wenye kukosa.

Hata hivyo Nabii Yusuf as hakuwa tayari kuona hali ya tahayari na kuumbuka ya ndugu zake inaendelea, hasa baada ya kuwa yeye amepata ushindi. Nabii Yusuf as hata hakutoa mwanya kwa ndugu zake waingiwe na dhana kwamba, huenda akalipiza kisasi kwa ubaya waliomfanyia. Bila kupoteza muda aliwapatia amani na utulivu na akasema:

Akasema: Leo hapana lawama juu yenu.

Kwa muktadha huo Nabii Yusuf as sio tu kwamba, hakuweka kinyongo au kulipiza kisasi kwa ubaya wa ndugu zake, bali alifanya kila awezalo ili wasihisi unyonge na hakuruhusu hali ya kutahayari iliyowapata iendelee. Aidha sio tu kwamba, aliwaonyesha kuwa, amewasamehe bali aliwahakikishia kwamba, makossa yao yamesamehewa na Mwenyezoi Mungu pia. Aya ya 92 ya Surat Yusuf inaashiria jambo hilo kwa kusema: Akasema: Leo hapana lawama juu yenu. Mwenyezi Mungu atakusameheni, naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanao rehemu.

Hivyo basi kwa hatua yake hiyo, Nabii Yusuf as alionyesha upana wa kifua alichonacho na kusamehe kwake. Watu wenye tabia za vinyongo na kuweka ubaya ndani ya vifua vyao kwa miaka na miaka na hata pengine kufa na vinyongo vyao kutokana na kutokuwa tayari kusamehe kosa alilotendewa na ndugu yake, wanapaswa kujifunza kupitia kisa cha Nabii Yusuf as na jinsi Nabii huyu alivyowasamehe ndugu zake, licha ya ubaya mkubwa waliomfanyai hata wa kufikia kumuuza ili tu aende mbali na asiwe karibu nao kutokana na roho mbaya walizokuwa nazo za kuona kwamba, baba yao anamuonyesha Yusuf mapenzi zaidi kuliko wao.

Kwa hakika viongozi wa dini wameonyesha katika sira ta matendo yao jinsi walivyokuwa na cifua vipana vya kusamehe, jambo ambalo bila shaka liliwaongozea hadhi, daraja na heshima pia. Jinsi Mtume saw alivyoamiliana na Mushrikina wa Makka baada ya Fat'h na ukombozi wa Makka ni mfano bora kabisa wa kusamehe kwa Waislamu. Baada ya kuukomboa mji wa Makka na mji huo kuangukia mikononi mwa Waislamu aliwahutubu makafiri kwa kuwaambia:

"Tambueni kwamba, mlikuwa majirani wabaya kwa Mtume wa Allah na mlimkadhibisha, hamkumuona yeye kuwa ni katika nyinyi, mkamfukuza, mlimuudhi na kumtendea ubaya na hamkuridhika bali mkaanzisha vita dhidi yake. Lakini kwa sasa, nyinyi nendeni na mko huru nyote."

 

Hapa tunaona ni jinsi gani Mtume alivyowasamehe makafiri licha ya maudhui na ubaya wa kila aina waliomfanyia. Katika tukio hili, Bwana Mtume saw sio tu kwamba, aliwasamehe bali aliitangaza nyumba ya mkubwa wao yaani Abu Sufyan na mke Hindu aliyekuwa mashuhuri kwa jina la "Mla Maini" mahala salama na kimbilio.

Aidha Imam Ali bin Abi Talib as wakati alipokuwa katika lahadha za mwisho za uhai wake baada ya kupigwa upangwa na Abd al-Rahman ibn Muljam al-Murādī aliyekuwa Khawarij alimwambia mwanawe Hassan kuhusiana na mtu aliyempiga upanga kwamba: Kama nitabakia haki, mwenyewe nitajua la kumfanya ima kumsamehe au kumlipizia kisasi. Na kama mauti yatanichukua ambayo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu, endapo nitamsaheme nitakuwa karibu Zaidi na Mwenyezi Mungu, hivyo nyinyi pia ninakutakeni mfanye wema na hisani, hivyo ni bora na nyinyi mkamsamehe.

Kwa hakika kusamehe humpa mtu hisia ya shakhsia na ukubwa na humuongezea mhusika nguvu za kiroho.

Hata hivyo, kuweko msamaha isiwe sababu ya mtu kukariri na kukariri makossa na ubaya wake kwa watu wengine kwa kutegemea msamaha.

Msamaha pia una masharti. Endapo mtu atakuwa na uhakika na yakini kwamba, mtenda kosa amejutia na kujilaumu kutokana na ubaya aliyomfanyia mwenzake, basi hapa ni mahala pake kwa aliyefanyiwa ubaya kusamehe. Lakini kama mhusika yaani aliyefanyiwa ubaya atafikia natija hii kwamba, kumsamehe mkosa kutazidi kumfanya awe na kiburi Zaidi na hata msamaha wake huenda ukatafsiriwa na mhusika kwamba, ni uoga na udhaifu, basi katika hali kama hii mtu hapaswi kusamehe.

Imam Zeinul Abidin as anasema katika kitabu mashuhuri cha Risat al-Huquuq Risala ya Haki kwamba: Haki ya mtu aliyekufanyia ubaya ni kumsamehe, lakini kama utaona msamaha wako una madhara kwake, basi muadhibu.

Imam Ali bin Abi Twalib as anaamini kwamba, mtu ambaye amefanya kosa kwa kufahamu yaani akiwa na ufahamu kamili, hastahiki msamaha.

Anasema kuwa: Mtu ambaye anafanya ubaya na dhambi akiwa na ufahamu kamili, hastahiki msamaha.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo.