Hadithi ya Uongofu (93)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita klilijadili maudhui ya msamaha na kusamehe katika Uislamu.
Tulisema kwamba, moja ya sifa njema za kimaadili na zinazopendwa katika Uislamu ni kusamehe makosa ya wengine na kwamba, kusamehe sifa ambayo muumini anapaswa kujipamba nayo ni moja ya ukamilifu wa kibinadamu. Aidha tuliashiria kisa cha Nabii Yusuf (as) na nduguze na jinsi alivyowaseheme licha ya wao kumtendehea ubaya kiasi cha kufikia kumuuza kwa thamani duni, kwa akali ya pesa. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 93 ya mfululizo huu kitazungumzia suala la "kulipiza kisasi" na kubainisha miongozo ya Uislamu kuhusiana na jambo hili. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo.
*****
Kulipiza kisasi ni hisia ambayo Mwenyezi Mungu ameiweka katika ujudi na uwepo wa wanadamu wote. Hisia hii aliyopatiwa mwanadamu na Mwenyezi Mungu ni kwa mujibu wa kigezo cha akili na kwa ajili ya kulinda mfumo wa jamii na kuhakikisha kwamba, haki inapatikana. Kwa hakika Uislamu unapinga aina yoyote ile ya dhulma na ukandamizaji dhidi ya mtu au jamii. Kwa muktadha huo, kukabiliana na madhalimu na kulipiza kisasi ni jambo lenye kufaa na wakati mwingine linahesabiwa kuwa ni la lazima.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya za 14 na 15 za Surat Tawba:
Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awafedheheshe na akunusuruni muwashinde, na avipoze vifua vya kaumu ya Waumini. Na aondoe hasira ya nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu humkubalia toba ya amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
Hivyo basi wapenzi wasikilizaji, kila mahala katika Qur'ani au hadithi ambapo ulipizaji kisasi umenasibishwa na Mwenyezi Mungu, makusudio ni kulipiza kisasi kwa mtu ambaye amekanyaga haki miongoni mwa haki za Mwenyezi Mungu na sharia za mbinguni.
Katika dua ya Makarim al-Akhlaq Imam Zeinul Abidin (as) anamuomba Mwenyezi Mungu ampe nguvu ya kukabiliana na madhalimu. Anasema: Ewe Mola! Nipe nguvu mbele ya mtu ambaye ananidhulumu, nipe ulimi (uwezo wa kuzungumza) mbele ya mtu ambaye anajadiliana na mimi, na unipe ushindi mkabala na mtu anayenifanyia uadui.
Tab'an kuna aina nyingine ya ulipizaji kisasi ambayo ni ulipizaji kisasi hasi na usio sahihi yaani mkabala kabisa na moja ya sifa kubwa za kimaadili yaani kusamehe. Aina hii ya ulipizaji kisasi huacha chuki na vinyongo katika moyo wa mtu na daima husubiri siku ambayo atamshinda adui yake na hivyo kumlipizia kisasi. Wakati mwingine ulipizaji kisasi wa aina hii sio tu kwamba, mtu hulipiza ubaya kwa ubaya bali kuna wakati hufikia kutenda mambo mabaya mara kadhaa ya ubaya aliofanyiwa, yaani kuchupa mipaka na kulipiza kisasi kwa kiwango ambacho ni zaidi ya ule ubaya aliotendewa. Baya zaidi ni kwamba, mtu anayefanya hivi hufikia hatua ya kujifakharisha, na kuona kwamba, ametenda jambo la sawa kwa kukomoa aliyemfanyia ubaya.
Kwa hakika ulipizaji kisasi ambao chimbuko lake ni taasubi na chuki za kijahilia, uadui usiofaa unaombatana na ukiukaji wa haki za wengine ni jambo ambalo limekatazwa na kuzuiwa katika Uislamu. Kwani katika ulipizaji kisasi wa namna hii si tu kwamba, haki haipatikani na dhulma kutoondolewa, bali huwa sababu ya kukanyagwa haki za wengine jambo ambalo huwa chimbuko la dhulma na ufisadi Zaidi katika jamii.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana viongozi wa Mwenyezi Mungu hakuna wakati ambao waliamiliana mithili ya walivyofanyiwa mkabala na dhulma na ukosefu wa adabu wa watu wengine, bali walikuwa wakisamehe katika mambo yaliyokuwa yakihusiana na masuala yao binafsi, isipokuwa pale wanapoona kwamba, sharia na hukumu za Mwenyezi Mungu zinadharauliwa na kupuuzwa. Mmoja wa wake za Bwana Mtume saw anasema kuwa: Katu sikuwahi kumuona Mtume wa Mwenyezi Mungu akilipiza kisasi kwa dhulma aliyotendewa, isipokuwa pale inapotokea kwamba, Mwenyezi Mungu anavunjiwa heshima. Inapotokea Mwenyezi Mungu kuvunjiwa heshima, basi Mtume alikuwa mkali katika hilo kuliko watu wote.
Katika hadithi nyingine Bwana Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa, wanadamu wanatofautiana.
Baadhi yao wanachelewa kukasirika na wanapokasirika hasira zao hazikawii kuondoka. Wengine hukasirika haraka yaani wana hasira za haraka na hasira zao pia kuondoka haraka. Kuna kundi jingine la watu ambao hasira zao ziko karibu yaani wanakasirika haraka na hasira zao huchelewa kuondoka, huku wengine huchelewa kukasirika na huchelewa kuondokewa na hasira.
Kundi bora kabisa miongoni mwa makundi haya ni wale ambao wanachelewa kukasirika na haraka huondokwa na hasira na kurejea katika hali ya kawaida. Aidha kundi baya kabisa miongoni mwa makundi haya ni lile la watu ambao wanakasirika haraka na hasira zao kukawia kuondoka yaani wanaochelewa kutulia hasira zao."
p
Wapenzi wasikilizaji, kila mahala ambapo kuna dhulma na haki za watu zinakanyagwa na kukiukwa, dini tukufu ya Uislamu inalitambua suala la kulipiza kisasi na kusimama kwa ajili ya kuzuia dhulma na ukandamizaji huo kuwa ni jambo la lazima na mafundisho ya Uislamu yanasisitiza juu ya jambo hili. Lakini pale inapotea kwamba, kuna haki ya mtu binafsi yaani jambo la binafsi na endapo mtu ataacha kulipiza kisasi na jambo hilo likawa halina dhulma na uenezaji ufisadi, basi njia bora hapa ni kusamehe.
Katika hali hii, si tu kwamba, Uislamu hauoni kwamba, kulipiza kisasi hapo inajuzu, bali unamshajiisha mtu asamehe na unaahidi kuwapatia ujira wanaosamehe.
Mtume Muhammad saw amenukuliwa akisema kuwa: Kila ambaye atadhulumiwa na akasamehe basi Mwenyezi Mungu atampatia badala ya hilo izza na heshima hapa duniani na kesho akhera.
Kwa hakika endapo mtu atasamehe katika mazingira ambayo ana nguvu na anaweza kulipiza kisasi, hali hii haiwezi kuhesabiwa kuwa ni udhaifu. Msamaha kama huu ni mzuri, wenye faida na wenye kujenga. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema: Samehe wakati ambao una nguvu ili ufikie ukamilifu.
Katika mafundisho ya Uislamu si tu kwamba, Uislamu unawataka waumini wasemehe na kujipamba na sifa hii nzuri ya kimaadili ya kufumbia macho ubaya waliofanyiwa, bali umekwenda mbali zaidi na na kuwataka waumini wajibu wema kwa ubaya na sio ubaya kwa ubaya.
Hii ni kutokana na kuwa, kusamehe na kujibu wema kwa ubaya hupelekea kuondoa chuki na vinyongo na baadhi ya wakati huwabadilisha maadui wenye roho mbaya na kuwa marafiki wenye huruma. Aya ya 34 ya Surat Fussilat inaashiria hilo kwa kusema: Mema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu.
Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.