Nov 21, 2017 06:54 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (94)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya mfululizo wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia suala la kulipiza kisasi na kuashiria miongozo ya Uislamu kuhusiana na jambo hilo.

Tulisema kuwa, kulipiza kisasi ni hisia ambayo Mwenyezi Mungu ameiweka katika ujudi na uwepo wa mwanadamu. Tuliona pia jinsi Uislamu ulivyotilia mkazo suala zima la kujiepusha na ujahili na taasubi katika suala la kulipiza kisasi.
Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 94 ya mfululizo huu kitazungumzia suala la hasira na ghadhabu na kubainisha miongozo Uislamu katika uwanja huu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki ili mtegee sikio kile nilichokuandalieni kwa leo. Karibuni.

*******

Moja ya ghariza na hisia zenye nguvu kwa mwanadamu ni hasira au ghadhabu. Nguvu hii imeweka katika ujudi wa mwanadamu ili aitumie kujihami na kulinda haki. Hata hivyo nukta muhimu na ambayo inapaswa kuzingatiwa ni hii kwamba, nguvu hii ya hasira inapaswa kuwa na hali ya uwiano; kwani kama itatoka katika hali ya kati na kati na uwiano, hugeuka na kuwa moja ya tabia na mienendo mibaya kabisa ya kimaadili. Hivyo basi, hasira na ghadhabu kama itakuwa katika hali ya uwiano katika njia ya haki sio tu kwamba, si yenye kuchukiwa bali ni yenye kupendwa na itakuwa iko katika ridhaa ya Mwenyezi Mungu. Imam Ali bin Abi Twalib as, Imam wa kwanza katika mlolongo wa Maimamu 12 wa Shia Ithaashara wa kizazi cha Bwana Mtume saw anazungumzia hasira za Bwana Mtume saw kwa kusema:

Mtukufu huyo katu hakuwa akikasirika kwa mambo ya dunia; lakini kila mara alipokuwa akikasirika kwa ajili ya haki, hakuwa akimtambua mtu na hasira za Mtume hazikuwa zikishuka mpaka anapoitetea na kuinusuru haki.

Kwa hakika mwanadamu katika mahusiano ya kijamii na wengine anaoishi nao kuna wakati hushuhudia makosa na utendaji usio sahihi na usiotarajiwa kutoka kwa wanajamii wenzake, na hivyo kumfanya akasirike na kughadhibika. Katika hali kama hii, jukumu la kiakhlaqi, kimaadili na kidini ni mtu kutodhihirisha hasira zake na kudhibiti ghadhabu zake.

Hii ni kutokana na kuwa, kama hasira hazitadhibitiwa na moto wa hasira za mtu ukawaka utamfanya adhalalike na kupata madhara yasiyofidika. Imam Ali as anaiona ghadhabu kuwa ni mithili ya moto na kwamba, kama hasira zitaondoka katika fremu ya dini, basi huunguza mizizi ya saada na ufanisi wa mtu na jamii kwa ujumla. Ndio maana amenukuliwa akisema kuwa: “Jiepusheni na hasira kwani ni moto uunguzao.”

 

Kikawaida pindi hasira zinapompanda mtu na kumshinda, mja huyo huondoka kabisa katika mamlaka ya sheria na utumiaji akili na ndio maana mtu aliyeshindwa kudhibiti hasira hufanya mambo ambayo si tu huwashangaza watu walionaye, bali hata yeye mwenyewe huingiwa na mshangao wa kile alichokifanya baada ya hasira na ghadhabu kumtoka.

Ndio maana tunashuhudia katika jamii tunayoishi wakati mwingine mtu hushikwa na hasira na kufanya mambo ambayo pindi anapotulia na hasira kumuondoka hujuta na kusikitika. Hata hivyo wakati huo majuto huwa ni mjukuu. Hii leo kuna watu wanaosota jela kutokana na kuua mtu katika ugomvi mdogo na usio na maana, ambapo kama mtu angelizuia hasira zake, basi asingekumbwa na majuto aliyonayo hivi sasa.

Imam Ali as amenukuliwa akisema kuwa: Kukasirika haraka ni aina ya umajununi na upunguani, kwani mwenye kufanya mambo wakati wa hasira baadaye hujuta, na kama hakujuta, upunguani wake huota mizizi na kuimarika. Kwa upande wake Imam Jaafar Swadiq as anasema kuwa: Kila anayeshindwa kumiliki na kudhibiti hasira zake, si mwenye kumiliki akili yake.

Kwa hakika hasira hutia dosari imani ya mtu. Akthari ya wakati mtu mwenye hasira hufanya dhambi ambazo zinakinzana kabisa na moyo wa imani. Ndio maana tunaona kuna hadithi nyingi zinazobainisha kwamba, hasira huharibu imani ya mtu.

Bwana wetu Mtume Muhammad saw amesema: Hasira inaharibu imani, kama siki inavyoharibu asali.

Kwa hakika hali hii kushabihisha aliyoibainisha Mtume saw katika hadithi hiyo inabainisha nukta hii kama, hasira na ghadhabu isiyo ya mahala pake hutoa pigo kubwa kwa imani na mahusiano na mawasiliano ya kiroho ya mwanadamu na Mwenyezi Mungu na hilo huondoa athari na baraka za imani na mawasiliano ya mja na Muumba kama vile hakukuwa na mawasiliano ya kiimani.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana mtu anapokuwa na hasira, shetani humuingia na kumshawishi kiurahisi na kwa wepesi kabisa.

 

Imekuja katika kitabu cha Akhlaq cha Muhajjatul Baidha kwamba: Dhulqarnein alikutana na mmoja wa Malaika na kumwambia:

 “Nifundishe elimu ambayo itaongeza imani na yakini yangu. Malaika akamwambia Dhulqarnen: Acha hasira na ghadhabu, kwani wakati mtu anapokasirika shetani humtawala mtu huyo kuliko wakati mwingine wowote, hivyo kabiliana na hasira kwa subira na unyeyekevu na zima moto wa hasira kwa utulivu, jiepushe na pupa na haraka, kwani unapofanya mambo kwa pupa na haraka unajinyima haki yako; na kuwa mwenye huruma na upole kwa watu wako wa karibu na wa mbali na usiwe mgumu, mkali na mwenye chuki.”

Wapenzi wasikilizaji, hasira hubomoa na kuharibu mantiki ya mtu na kumfanya azungumze mambo ya hovyo hovyo na ya batili. Imenukuliwa kutoka kwa Mtume saw ya kwamba, amesema: Mtu ambaye ana jukumu la kutoa hukumu, asitoe hukumu wakati akiwa na hasira.

Hadithi hii inaonyesha kwamba, endapo kadhi au hakimu atatoa hukumu hali ya kuwa ni mwenye hasira na ghadhabu atapelekea haki ya mtu kupotea. Miongoni mwa matokeo mengine mabaya ya hasira na ghadhabu ni kudhihirika aibu na mapungufu ya mtu yaliyojificha.

Kwani katika hali ya kawaida kila mtu anaweza kujidhibiti na kujizuia na hivyo kuficha mapungufu aliyonayo ambayo yamejificha na hivyo kulinda heshima na hadhi yake. Lakini pindi mtu anapopandwa na hasira na moto wa hasira kuwaka, pazia na kizuizi huondoka, hushindwa kuidhibiti akili yake na kwa msingi huo mapungufu aliyonayo hudhihirika na kujitokeza na mwishowe heshima yake kuondoka.

Tunahitimisha kipindi chetu cha leo kwa kusema kuwa, ghadhabu na hasira ni kikwazo kinachomzuia mwanadamu kufikiri kwa njia sahihi na inayofaa.

Kwa maana kwamba, mtu akiwa na hasira hawezi kufikiri kwa njia sahihi na mara nyingi mtu anayechukua uamuzi akiwa na hasira matokeo yake huwa ni majuto. Imam Ali AS anasema: "Watu ambao hawanufaiki na hekima na elimu ya kweli ni wale ambao akili zao zina maradhi ya ghadhabu na matamanio ya nafsi.

Kwa leo tunakomea hapa kutokana na kumalizika muda wa kipindi chetu. Jiungeni nami wiki ijayo, katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.