Nov 21, 2017 07:01 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (97)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu, kipindi ambacho hukujieni siku na wakati kama huu kutoka hapa Tehran, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia sifa nzuri ya ushujaa na tulisema kwamba, miongoni mwa sifa nzuri ambazo huwa sababu na chimbuko la izza na heshima ya shakhsia ya mtu ni ushujaa. Aidha tulisema kuwa, ushujaa maana yake ni kuwa na hali ya moyo thabiti na kutoogopa kile ambacho hakipaswi kuogopwa. Kadhalika tulibainisha kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu endapo mtu ataweza kujitenga mbali na dhambi na hali ya kuteleza katika sheria za Mwenyezi Mungu na akadumu katika hilo, basi huyo anahesabiwa kuwa ni shujaa. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 97 ya mfululizo huu kitazungumzia moja ya sifa mbaya ya kimaadili ambayo ni kinyume cha ushujaa yaani woga au kitete na hawafu. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa juma hili. Karibuni.

*******

Woga ni miongoni mwa hali ya kisaikolojia anayokuwa nayo mwanadamu, ambayo humfanya mtu mwenye hali hii ashindwe kukabiliana na matatizo na kuondoa vizingiti vinavyomkabili maishani. Hali hii humpokonya mtu uwezo wa kufanya hima kwa ajili ya kukabiliana na kile kilichoko mbele yake. Pamoja na hayo, woga kwa kiwango fulani ni wa lazima katika mwenendo wa ukamilifu wa shakhsia ya mtu. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana hofu na woga hugawanywa katika makundi mawili yaani hofu mbaya na nzuri. Hofu nzuri na inayopendwa ni ya kumuoga Mwenyezi Mungu. Hofu hii sio tu si mbaya, bali imehimizwa katika mafundisho na maamrisho ya dini. Hofu hii hutokana na kuzembea na kutotekeleza majukumu ambayo mtu alipaswa kuyatekeleza na hivyo kumfanya aogope mahakama ya uadilifu wa Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo, hofu na woga wa namna hii kiuhakika ni woga wa mtu kufanya madhambi. Mtu ambaye ameshikamana na imani juu ya Mwenyezi Mungu na akatawakali na kumtegemea Muumba na nguvu zisizo na mpaka za Allah, ni shujaa na katu hamuogopi asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Imam Jaafar Swadiq as anasema: Mtu ambaye anamuogopa Mwenyezi Mungu, Allah humfanya aogopwe na kila kitu na kila mtu; na mtu ambaye hamuogopi Mwenyezi Mungu, Allah humuogopesha na kumtisha na kila mtu na kila kitu.

Kwa hakika hofu na woga ni miongoni mwa sababu muhimu za kumfanya mtu ashindwe na kuwa dhalili, si katika medani ya vita tu bali hata katika masuala ya kisiasa na kijamii na vile vile katika mambo ya kielimu. Imam Ali as anawataka watu wasiogope chochote isipokuwa kutenda dhambi. Hii ni kutokana na kuwa, kumuogopa Mwenyezi Mungu maanake ni kuogopa uadilifu wake.  Katika dua maarufu ya Jawshan Kabir tunasoma:

یا مَن لا یُخافُ إلاّ عدلُه‌

"Ewe ambaye hauogopwi isipokuwa uadilifu wake".

Imam Jafar Sadiq AS

 

Wakati mwingine woga na hofu hutokana na kudiriki adhama na daraja ya Mwenyezi Mungu na kuzingatia uwepo usio na kikomo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hofu na woga huu haupatikani isipokuwa kwa watu ambao wanatambua vyema adhama ya Mwenyezi Mungu.  Qur'ani Tukufu inaitaja hali hii kwamba, ni maalumu na makhsusi kwa waja wake wasomi na wenye welewa na ujuzi. Aya ya 28 ya Surat Faatir inasema:

إِنَّمَا یَخْشَی اللَّهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَآؤُاْ 

Kwa hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni.

Aya hii inaonyesha kuwa, wanamuogopa zaidi na kumcha zaidi Mwenyezi Mungu ni wajuzi na wanazuoni. Mtume saw anaitaja hofu juu ya Mwenyezi Mungu na hali ya kumuogopa Muumba kwamba, ni kiini cha hekima zote.  Hii ni kutokana na kuwa, aina hii ya woga na hofu humfanya na kumuweka mtu katika njia ya ukamilifu na ya kupigania haki. Imam Ja'afar Swadiq as amenukuliwa akisema kuwa: Kila mwenye kumtambua Mwenyezi Mungu humuogopa, na kila mwenye kumuogoa, hali hii humfanya awe ni mwenye kutii haki na hujipamba adabu na mwenendo mzuri.

Amma woga na hofu isiyofaa ni mtu kuogopa kila asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Aina hii ya hawafu na woga humzuia mtu kufanya mambo makubwa. Hii ni kutokana na kuwa, kazi na mambo makubwa, siku zote hukabiliwa na matatizo makubwa na watu wanapaswa kufanya hima kwa ajili ya kuhakikisha wanavuka vizingiti hivyo vya matatizo.

Kwa hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni

 

Kwa hakika ni jambo lisilo na shaka kwamba, mtu ambaye ni mwoga hawezi kuyafanya hayo. Hivyo basi watu wa aina hii siku zote hutosheka na kazi na mambo madogo tu, kwani ni waoga na hawana ujasiri wa kufanya mambo makubwa ambayo yana vizingiti na matatizo mengi na makubwa ambayo yanahitajia ujasiri na kutokuwa na woga na hofu.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana katika mafundisho ya Uislamu, watu wamekatazwa kushauriana na watu waoga. Hiyo ni kutokana na kuwa, watu waoga huwazuia watu wengine kufanya mambo makubwa kutokana na woga wa ndani ya nafsi walionao. Imam Ali bin Abi Twalib as anamtaka Malik al-Ashtar Gavana wake wa Misri kutoshauriana na watu waoga, kwani watu wa aina hiyo watapelekea kudhoofika rai na uamuzi wake. Sehemu ya barua ya 53 ya Imam Ali kwa Malik al-Ashtar inasema:….Watu waoga huyakuza mambo ambayo kwa mtazamo wako ni madogo.

Kwa hakika woga na kitete kisichofaa huwa na matokeo mabaya. Kadiri mtu anavyozidi kuogopa, ndivyo anavyozidi kujidhoofisha zaidi na hivyo kutoa pigo kubwa zaidi kwa shakhsia yake. Lakini kama mtu mwoga atachukua hatua za maana na thabiti kwa ajili ya kutibu maradhi yake ya woga, anaweza kusaidia mno kuboresha usalama wake wa kinafsi na kisaikolojia na hivyo kufikia saada na ukamilifu.

Imam Ali bin Abi Twalib as anasema: Haifai na si laiki  kwa mtu mwenye akili awe katika katika hali ya hofu na woga, endapo atakuwa na njia ya utulivu na usalama.

Kwa bahati nzuri woga usiofaa una tiba. Kutafakari juu ya athari mbaya na zenye madhara za woga, ni moja ya mbinu na mkakati mzuri na unaofaa sana wa kutibu sifa hii mbaya ya kimaadili. Aidha kutafakari juu ya madhila na uduni unaotokana na woga usio wa mahala pake na vitu anavyokosa mtu katika maisha yake kutokana na woga nayo ni njia bora ya kuepukana na woga. Imam Ali as anasema: Kutafakari na kufikiria kuhusiana na matokeo ya kazi za mwanadamu, humuokoa na hilaki na maangamizi.

Njia nyingine ya kutibu woga na hofu ni kuingia katika medani ya kutisha na kuogopesha na kukariri hilo mara kadhaa.

Muda wa kipindi chetu kwa leo unakomea hapa, tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.