Dec 03, 2017 04:45 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (98)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji mnapokutana nami Salum Bendera katika mfululizo wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu, kipindi ambacho hujadili masuala mbalimbali ya kijamii, kimaadili, kidini na kadhalika na kukunukulieni baadhi ya hadithi na miongozo kutoka kwa Bwana Mtume saw na Maimamu watoharifu as kuhusiana na maudhui hizo.

Kipindi chetu kilichopita kilijadili moja ya sifa mbaya ya kimaadili ambayo ni kinyume cha ushujaa yaani woga au kitete na hawafu. Tulisema kuwa, woga ni miongoni mwa hali ya kisaikolojia anayokuwa nayo mwanadamu, ambayo humfanya mtu mwenye hali hii ashindwe kukabiliana na matatizo na kuondoa vizingiti vinavyomkabili maishani. Hali hii humpokonya mtu uwezo wa kufanya hima kwa ajili ya kukabiliana na kile kilichoko mbele yake. Tulibainisha kwamba, hofu imegawanyika katika makundi mawili yaani hofu mbaya na nzuri, ambapo hofu nzuri na inayopendwa ni ya kumuoga Mwenyezi Mungu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 98 ya mfululizo huu kitazungumzia moja ya tabia njema nayo ni ya huruma, upole na ulaini. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo.

*********

Upole na ulaini na kuamiliana na watu kwa huruma ni miongoni mwa njia bora kabisa za kuleta marekebisho katika jamii. Upole na ulaini wa Mtume ulimsaidia mbora huyo wa viumbe katika kufikia malengo yake ya muda mrefu na akafanikiwa kuibadilisha jamii ya wakati huo iliyokuwa imetawaliwa na chuki, adawa na utumiaji mabavu na matunda yake yakawa ni kuenea Uislamu katika kila kona ya ulimwengu. Kimsingi ni kuwa, kuwaongoza na kuwapatia wanadamu hidaya na uongofu hakupatikani isipokuwa kwa huruma, upole na ulaini. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana katika Qur'ani Tukufu Mwenyezi Mungu anautaja upole na ulaini kwamba, ni moja ya neema kubwa kwa Mtume saw. Aya ya 159 ya Surat al-Imran inaashiria suala hilo kwa kusema:

"Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. "

Wapenzi wasikilizaji tabia njema, upole na ulaini wa Mtume uliwavutia wengi na kuwa sababu muhimu ya kuzima hitilafu na mifarakano. Tabia yake njema wakati mwingine iliwafanya hata maadui wake wakubwa kuungana na wafuasi wake.

Kwa hakika ulaini ni ile hali ya huruma na upole na kuacha utumiaji mabavu katika kauli na matendo. Mtu ambaye ni mlaini na mpole katika hali zote, sawa afanyiwe upole au mtu aamiliwe kwa mabavu, siku zote hufanya mambo kwa bashasha na huruma. Huu muamala yaani hali ya kuwa na ulaini na upole, ni jambo ambalo lina nafasi kubwa katika kujenga na kutengeneza maisha ya kifamilia na ya kijamii ya mtu. Aidha kupatikana kheri na baraka katika maisha, kudumu huba na urafiki, kusitiriwa aibu na kuondoka chuki, vinyongo na uadui, yote hayo chimbuko lake ni athari za baraka za ulaini, upole na huruma. Kadhalika upole na ulaini ni katika sifa za Mwenyezi Mungu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana wakati mtu anapolingania neno la haki anapaswa kutumia mbinu na misingi sahihi na hapaswi kutumia mabavu au kulazimisha hata kidogo katika ulinganiaji wake.

 

Tukirejea kisa cha Manabii Mussa na Harun as tunaona jinsi Mwenyezi Mungu alivyowataka watumie maneno mazuri na malaini walipotakiwa kwenda kumlingania Firauni mfalme aliyekuwa amechupa mipaka katika zama hizo. Aya za 43 na 44 za Surat Taha zinaashiria hilo pale Mwenyezi Mungu anaposema:

Nendeni kwa Firauni. Hakika yeye amepindukia mipaka. Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa.

Waswahili pia wana msemo mashuhuri usemao maneno mazuri humtoa nyoka pangoni; wakimaanisha kwamba, kauli njema huweza kumlainisha hata adui yako na kumfanya abadilishe msimamo au kusikiliza unayomueleza.

Katika mantiki ya Uislamu, tabia njema au upole na ulaini unatajwa kuwa moja ya sifa za watu wema na wakarimu. Imam Jaafar Swadiq as anavitaja vitu vitatu kwamba, ni katika ishara za ukarimu wa mtu ambavyo ni tabia njema, kudhibiti hasira na kufumbia macho makossa ya wengine.

Kwa hakika sifa zote hizo tatu hupelekea kutokea marekebisho na utulivu katika jamii na familia.  Imam Ali bin Abi Twalib as licha ya haiba, adhama na ushujaa mkubwa aliokuwa nao vitani wakati wa kupambana na maadui wa Uislamu, lakini alisifika pia kwa sifa ya upole na ulaini, unyenyekevu na kuyachukulia mambo kwa wepesi yaani kutokuwa mgumu katika mambo ya kawaida.

Katika wasia wake wa kudumu aliwausia watoto na wafuasi wake wajipambe kwa sifa ya upole na ulaini. Anasema katika sehemu moja ya wasia wake huo katika barua ya 31 inayopatikana katika kitabu cha Nahaj al-Balagha kwamba: Kila anayeamiliana nawe kwa ukali, wewe amialiana naye kwa ulaini. Kwani ulaini wako unaweza kubadilisha kwa haraka mtazamo wake na hivyo akaamiliana nawe kwa ulaini na upole.

Aidha katika nasaha yake nyingine Imam Ali as anaashiria jambo hili kwa kusema: Uzoeshe ulimi wako kusema maneno laini, mazuri na kusalimia, ili marafiki zako waongezeke na maadui zako wapungue. Kadhalika amenukuliwa katika hadithi nyingine akisema kuhusiana na maudhui hii kwamba:  Kila mwenye hali ya ulaini, atanufaika kwa mahaba ya daima ya familia.

Muhammad Mtume wa Allah

 

Kwa hakika baina ya matendo na maadili ya mwanadamu kuna uhusiano wa moja kwa moja. Kama ambavyo tabia na mwenendo mwema una taathira chanya ya moja kwa moja katika muamala mzuri wa mtu na ukarimu wa nafsi, vivyo hivyo, tabia mbaya na mwenendo usiofaa hupelekea ugumu wa moyo na mhusika kuwa na hali ya ukali ambayo ni kinyume cha ulaini na upole. Ni jambo lisilo na shaka kwamba, mtu mkarimu hulainika mbele ya utafadhalishaji wa watu wengine. Hii ni katika hali ambayo, mtu mbaya huonyesha ugumu wa moyo mbele ya utadhalishaji wa watu wengine.

Tunasoma katika sehemu moja ya Dua ya Makarim al-Akhlaq ya Imam Ali bin Hussein Sajjad as kwamba'; Ewe Mola! Nipe tawfiki ya kuamiliana na watu kwa upole, ulaini na unyenyekevu.

Kwa hakika upole na kuwa na hali ya ulaini ni jambo lenye taathira kubwa katika maisha ya kijamii ya mtu. Katika maisha ya haya mwanadamu hukumbana na matatizo na matukio machungu na endapo mwanadamu huyu hatakuwa na hali ya upole na ulaini kwa watu, atakabiliwa na matatizi zaidi. Kwani kuamiliana na watu kwa ukali na utumiaji mabavu ni jambo ambalo huwa na madhara kwa itibari ya kijamii na usalama wa kidini na kimaadili wa mtu.

Kuchunga hali ya upole na ulaini wakati wa kuamiliana na watu hupelekea kuchanua vipaji vya mtu. Aidha katika jamii tunayoishi, watu huwapenda na kuwapa heshima maalumu watu wapole na wanaoamiliana na watu kwa ulaini, huku wakiwachukia na kuwa na uhasama na watu wagumu na wanaoamiliana na watu wengine kwa ukali na utumiaji mabavu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha Hadithi ya Uongofu kwa wiki hii umefikia tamati. Msikose kujiunga nami juma lijalo, siku na wakati kama wa leo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.