Hadithi ya Uongofu (101)
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha juma lililopita kilizungumzia suala la kiburi na namna ya kujiepusha na tabia hii mbaya ya kimaadili. Tulisema kuwa, kiburi ni hisia ya mtu kujiona kuwa yeye ni mbora kuliko watu wengine. Kiburi kinajulikana pia kuwa ni hali ya kutakabari, kuwa na majivuno na kuwaona watu wengine si lolote si chochote.
Tulibainisha kwamba, katika aya na hadithi mbalimbali, kiburi kimekewa mno na moto wa Jahanamu kutajwa kuwa ndio makazi na mafikio ya wenye kiburi. Aidha tulinukuu hadithi ya Mtume Muhammad saw alipokuwa akiwausia watu wajiweke mbali na kiburi na kujiona wabora kuuliko watu wengine kwa kusema: Jiepusheni na kiburi, kwani yumkini mja akajipamba na kiburi kiasi cha Mwenyezi Mungu kufikia kusema kuwa: Andikeni jina la mwenye kiburi na mwenye kujiona katika kundi la madhalimu.
Sehemu ya 101 ya kipindi chetu cha juma hili ambayo ni muendelezo wa maudhui wa maudhui ya kiburi na jinsi ya kujiepusha na tabia hii mbaya ya kimaadili itazungumzia suala la kupenda jaha na uongozi. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio kile nilichokuandalieni kwa leo. Karibuni.
Moja ya sifa mbaya na zinazochukiza ni hatua ya baadhi ya watu kukumbwa na maradhi ya kupenda jaha na uongozi kupita kiasi. Kutokana na watu hao kuwa na hamu na shauku hiyo ya kupenda uongozi na jaha hujiona wao ni wabora kuliko watu wengine na hufanya kila hima na idili kwa ajili ya kupata uongozi na madaraka. Wataalamu wanasema kuwa, kupenda jaha maana yake ni kuwa na mapenzi ya kupindukia ya uongozi na cheo kiasi kwamba, katika mazingira kama haya, mtu wa aina hii awe yuko tayari kufikia lengo hilo kwa thamani na gharama yoyote ile. Kwa hakika kupenda jaha na uongozi ni miongoni mwa mambo hatari mno ambayo sio tu hutoa pigo kwa mtu katika upande wa kimaanawi, bali kwa mtazamo wa kijamii humfanya mtu huyo achukiwe na kutengwa na wanajamii wenzake. Hii hali ya kupenda jaha, uongozi na umashuhuri na cheo katika jamii, humpelekea mtu huyo kuikanyaga haki na kuipuuza moja kwa moja, ili tu aweze kufikia katika malengo yake aliyokusudia yaani ya cheo au kulinda nafasi na uongozi wake alionao.
Dini tukufu ya Kiislamu imekemea mno suala la mtu kupenda jaha na uongozi. Moyo ambao unapiga na kudunda kutokana na kupenda kukuza jina hauwezi kuwazingatia watu, bali huwa mtumwa wa hilo unalolihangaikia. Tabia ya kupenda jaha na uongozi ni sifa mbaya na hatari ya kimaadili. Hii ni kutokana na kuwa, mtu anayetaka uongozi na cheo na moyo wake daima unadunda kwa ajili ya kufikia lengo hilo, huwa yuko tayari kufanya jambo lolote lile, ili tu atimize mradi wake. Akiwa na lengo la kumbwaga mshindani wake katika kufikia cheo au uongozi wanaoshindania, hutumia kila hila, hadaa na njama za kishetani kama urongo, tuhuma, kusengenya au hata kueneza uvumi na propaganda dhidi ya mshindani wake. Ni kwa kuzingatia uhakika huo, ndio maana Imam Jaafar Swadiq as amenukuliwa akisema kuwa: Ameangamia kila anayetafuta cheo na uongozi.
Kupitia hadhithi hii ya Imam Swadiq as tunajifunza nukta moja muhimu nayo ni kwamba, moja ya athari haribifu za kupenda na kutafuta cheo na uongozi kwa thamani yoyote ile ni kuangamia kutokana na athari ya madhambi.
Moja ya nadhara ya kupenda cheo na uongozi ni kuondoka dini na imani ya mtu. Muumini daima hufanya hima na idili kwa ajili ya kulinda imani yake. Lakini kuna mambo ya pembeni ambayo huwa chanzo na chimbuko la kuondoka na kusambaratika imani na itikadi yake. Moja ya sababu hizo ni kupenda jaha na uongozi. Jambo hilo ni hatari kiasi kwamba, kuna hadithi kadhaa zinazoeleza kwamba, hatari na uharibifu wa mbwa mwitu wanaoshambulia kundi la kondoo sio mkubwa ikilinganishwa na hatari na ufisadi, uharibifu wa hamu na kupenda uongozi, mali, na umashuhuri katika dini ya Mwislamu. Hivyo basi mtu anayetaka jaha na uongozi kwa thamani yoyote ile ni sawa na kuwa amekabidhi imani yake kwa mbwa mwitu na bila shaka mnyama huyo hatari atairarua imani hiyo na kuiangamiza.
Kwa hakika watu wanaopenda jaha na uongozi, daima hufanya hima ya kuhifadhi na kulinda uongozi wao usiwatoke na daima hufanya juhudi kadiri wawezavyo ili kuhakikisha kwamba, vyeo walivyonavyo wanaendelea kuwa navyo kwa thamani yoyote ile. Mtu wa namna hii huugua na kupata maradhi mara anapopoteza cheo au uongozi alionao. Watu wa aina hii husononeka na kupata maradhi ya nafsi mara wanapopokonywa vyeo na madaraka walionayo.
Watu wa aina hii hushughulishwa na pirika za kuhifadhi vyeo walivyo navyo kiasi cha kughafilika na Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama.
Akthari ya watu ambao wanahangaika kutafuta cheo na madaraka wanapenda watu wengine wawaonyeshe heshima. Wanapenda watu wote wawaheshimu na kuwanyenyekea na kila wanapotokea basi watu wasimame na kuonyesha heshima kwao. Hii ni katika hali ambayo, mapenzi na kiburi hiki kina adhabu mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kuhusiana na jambo hilo, siku moja Bwana Mtume saw alimwambia sahaba wake Abu Dharr al-Ghifari kwamba: Mtu ambaye anapenda watu wasimame kwa ajili yake basi na achague moto wa Jahanamu kuwa ndio makazi yake. Kwa hakika mtu mwenye kufikiri kwa makini na akatilia maanani faida na madhara ya cheo na uongozi, bila shaka atafikia natija hii kwamba, endapo jaha na uongozi utaambatana na hila na ujanja ujanja, hautakuwa na natija ghairi ya kupoteza heshima na hadhi duniani na akhera. Hata hivyo kama uongozi huo utaambatana na ukweli na kufanya mambo kwa njia sahihi basi utafuatiwa na mambo mengi magumu, kwani uongozi si lele mama. Kwa msingi huo basi, endapo mtu atafikiri kwa makini atadiriki na kufahamu kwamba, uongozi hauna kingine ghairi ya mashaka na taabu.
Mtume saw anataja sifa tatu ambazo humkumba mtu aliyeko uongozi, tabaani endapo hataongoza kama inavyotakiwa. Mosi, ni lawama, pili ni majuto na tatu ni adhabu Siku ya Kiyama.
Aidha katika Kitabu Kitukufu cha Qur’ani na hadithi suala la kupenda jaha na uongozi limekemewa sana. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 83 ya Surat al-Qasas:
Hayo ndiyo makaazi ya Akhera, tumewafanyia wale wasio taka kujitukuza duniani wala ufisadi. Na mwisho mwema ni wa wachamngu.
Katika aya hii haijaelezwa kwamba, saada ya akhera si ya watu wanaojitukuza na kutaka ukubwa na cheo bali aya imekwenda mbali zaidi na kueleza kwamba, saada na akhera ni ya watu ambao hata hawafikirii kuwa na cheo na ukubwa na kuwaongoza wengine.
Endapo cheo na uongozi litakuwa ndilo lengo la mwisho la mwanadamu, litakuwa jambo baya mno na linalochukiza. Hata hivyo kama suala hilo litakuwa ni kwa ajili ya kutekeleza uadilifu na kuhakikisha haki za watu zinapatikana, sio tu kwamba, jambo hilo halipendezi, bali hapo itakuwa ni dharura kutekeleza hilo.
Ibn Abbas mfasiri mkubwa wa Qur’ani Tukufu mwanzoni mwa Uislamu anasimulia kwamba: Siku moja nilikwenda kwa Imam Ali bin Abi Twalib (as) na nilipoingia nilimkuta akishona kiatu. Aliponiona akaniuliza, thamani ya kiatu hiki ni kiasi gani? Nikamwambai, hakina thamani. Akasema, ninaapa kwa Mwenyezi Mungu kiatu hiki kisicho na thamani, ninakipenda zaidi kuliko kukutawaleni nyinyi, isipokuwa kama nitasimamisha haki au kuiondoa batili.
Tunamalizia kipindi chetu cha leo kwa kusema kuwa, mtu muumini si mwenye kutaka kuwatawala watu wengine, lakini kama atakubali kubeba na kuchukua jukumu la kuwaongoza watu, basi anapaswa kukitumia cheo hicho kwa ajili ya kusimamisha haki na uadilifu.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa juma hili. Tukutane wiki ijayo ijayo, siku na wakati kama wa leo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh.