Hadithi ya Uongofu (102)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Kipindi chetu cha juma lililopita kilizungumzia suala la kupenda jaha na uongozi. Tulisema kuwa, moja ya sifa mbaya na zinazochukiza ni hatua ya baadhi ya watu kukumbwa na maradhi ya kupenda jaha na uongozi kupita kiasi. Tuliona jinsi dini tukufu ya Kiislamu ilivyokemea mno suala la mtu kupenda jaha na uongozi. Aidha tulitaja baadhi ya madhara ya kupenda cheo na uongozi na tulieleza kwamba, moja ya madhara hayo ni kuondoka dini na imani ya mtu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 102 ya mfululizo hii kitazungumzia moja ya sifa nyingine mbaya ya kimaadili nayo ni kinyongo, chuki na husuda. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.
Katika kitabu Kitukufu cha Qur'ani neno Ghill lenye maana ya chuki na kinyongo limekuja mara kadhaa na hii inatambuliwa kuwa sifa mbaya na isiyofaa kwa mwanadamu. Chuki, kinyongo na ghadhabu za ndani ndio mambo ambayo humfanya mtu asiwe na nia ya kusamehe bali akae na kusubiri ili aje kulipiza kisasi. Hali hii ya chuki na kinyongo katika akthari ya wakati kutokana na kutokuwa na uwezo wa kufanya muqawama au kukabiliana na adui, chimbuko lake huwa ni husuda na hubakia kwa muda mrefu katika roho ya mwanadamu. Kwa msingi huo basi, tunaweza kusema kuwa, chuki ni matunda ya ghadhabu na husuda. Sehemu moja ya aya ya 10 ya Surat al-Hashr inasema:
… wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani (kinyongo) kwa walio amini.
Kimsingi chuki, kinyongo na kuwa na undani na mtu yaani kumuwekea kinyongo ni miongoni mwa sifa mbaya za kimaadili ambayo hupelekea kuibuka katika moyo mtu masuala kama husuda na ghadhabu. Sifa hii mbaya huwa na taathira katika pande zote mbili yaani upande wa mwili na wa kiroho. Hii ni kutokana na kuwa, mtu mwenye chuki na kinyongo hukosa nguvu ya akili na hivyo kushindwa kudhibiti mambo.
Imam Ali bin Abi Twalib as anasema akibainisha chimbuko la chuki kwamba ni husuda kwa kusema: Chuki na kinyongo ni sifa za mahasidi na wanaowataka mabaya.
Aidha ameashiria sifa za uhasidi kwa chuki na kinyongo na kusema kuwa:
Hasidi hukasirika haraka na huchelewa kuondoa chuki na kinyongo katika moyo wake. Kadhalika Imam Ali bin Abi Twalib as anawausia watu na kuwataka wajitenge mbali na watu mahasidi yaani watu wanaoyaonea kijicho mafanikio ya watu wengine; kwani chuki, undani au fundo na kinyongo ni miongoni mwa maradhi hatari ambayo huchukua muda kuyatibu na humsababishia mwanadamu madhara mengi. Kutokana na kuwa chuki na kinyongo huchafua na kuharibu fikra za mtu, hali hiyo hairuhusu na kumpa fursa mhusika ya kufanya mambo mazuri au kuzikubali na kuzipokea kwa mikono miwili kazi nzuri za watu wengine.
Kwa hakika mtu mwenye chuki na kinyongo hushindwa kufanya amali njema na mambo mazuri na huwa hayuko tayari kukubali kwamba, fulani amefanya jambo jema na zuri na akiri na kulikubali hilo. Kwa msingi huo, mtu huyu huishi katika hali ya kinyongo na fundo moyoni akichukia kazi nzuri za mtu ambaye ana kinyongo naye. Kwa msingi huo, maradhi haya humfanya mhusika kuziona kuwa mbaya kazi nzuri ambazo zinafanywa na mtu ambaye ana undani na kinyongo naye.
Wataalamu wa elimu nafsi wanaamini kuwa, chuki na kinyongo ni kama maradhi ya husuda ambapo kabla ya kumdhuru mtu mwingine na kutoa pigo humdhuru mtu mwenye chuki na kinyongo na mtu au watu wengine, kiasi cha kufikia kuharibu hata kazi zake nzuri anazozifanya.
Ni kutokana na sababu hiyi ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib AS anaihesabu chuki na kinyongo kwamba, ni muangamizaji wa mambo na kazi nzuri za mtu na anawatahadharisha watu na jambo hili na anasema: Chuki na kinyongo, inaangamiza na kutokomeza mambo mazuri.
Moja ya sababu za mtu kuwa na chuki na kinyongo au undani na mtu ni dhana mbaya kwa watu wengine. Baadhi ya watu wana maradhi haya mabaya ya kuwadhania vibaya watu wengine na daima si wenye kudhania watu wengine dhana nzuri. Tukirejea Qur'ani na hadithi tunaona ni kwa kiwango gani, suala la watu kudhaniana dhana nzuri lilivyotiliwa mkazo. Hii ni kutokana na kuwa, chimbuko la chuki na vinyongo vingi katika jamii ni kuwa na dhana mbaya. Mtu ambaye ataweza kubadilisha dhana mbaya aliyonayo kwa mtu fulani na kuifanya kuwa dhana nzuri basi bila shaka chuki na kinyongo chake kitaondoka na moyo kuwa msafi kabisa. Katika hali hiyo, mtu huyo hapati isipokuwa kheri na mambo mazuri.
Sababu nyingine inayopelekea kujitokeza chuki na uadui au kinyongo ni utani na mzaha usio na maana na usio na heshima ndani yake.
Mtume saw anawasia waumini wasifanyiane mzaha na chuki kwa kusema: Usifanye uadui na mzaha na ndugu yako, kwani yote mawili haya ni sababu ya uadui na kinyongo.
Dhihaka na utani mbaya na usio na mipaka hupelekea anayefanyiwa hilo kukasirika na matokeo yake ni mhusika kuwa na kinyongo na aliyemfanyia utani huo mbaya.
Imam Ali bin Abi Twalib AS anawaasa watu akiwataka wajihadhari na mzaha. Anasema: Jiepusheni na mzaha, kwani huleta jambo mbaya na kuacha chuki.
Kwa hakika mtu anapaswa kutambua kwamba, madhali katika moyo wake kuna chuki na kinyongo, daima atakuwa ni mtu wa huzuni na ghamu. Imam Hassan al-Askary AS anasema kuwa: Mtu mwenye utulivu mdogo kabisa miongoni mwa watu ni yule mwenye chuki na kinyongo moyoni mwake.
Kwa muktadha huo ili kuondoa tatizo na maradhi haya kuna haja kwa mtu kujiepusha na kinyongo na kuondoa chuki na fundo katika moyo wake. Ukweli wa mambo ni kuwa, kama mtu atawapendelea wengine kile anachokipenda yeye na kutowafanyia watu wengine kile ambacho yeye mwenyewe anakichukia, katika hali kama hiyo atasalimika na chuki na kinyongo. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib anasema kuuwa: Ili kuondoa chuki na kinyongo katika vifua vya wengine, ondoa kinyongo na chuki katika kifua chako. Katika Qur'ani Tukufu, Mitume, waumini na watu wa peponi wamewekwa mbali na sifa mbaya ya kinyongo na chuki. Hii ni kutokana na kuwa, kimsingi ni kuwa, chuki au kinyongo na imani ni vitu viwili ambavyo haviendani yaani havikai pamoja. Kwa mujibu wa Mtume saw ni kuwa, Muumini si mtyu mwenye chuki na kinyongo. Imam Swadiq as katika kubainisha kwamba, muumini hamuwekei mwenzake kinyongo na kama atakasirika basi ni kwa muda mfupi sana, anasema kuwa: Kinyongo cha muumini hubakia kifuani kwake madhali amekaa, lakini mara anaposimama tu, kinyongo nacho huondoka katika moyo wake.
Hadithi hii inaonyesha kwamba, katika hali ya kawaida Muumini si mtu wa vinyongo na undani na kama ikitokea hivyo, basi jambo hilo hudumu kwa muda mfupi sana katika moyo wa muumini.
Wapenzi Wasikilizajio kutokana na kumalizika kwa muda wa kipindi hiki kwa leo, sina budi kukomea hapa, tukutane tena wiki ijayo, siku na wakati kama wa leo. M
Wassalaamu Alaykum Warhamtulla hi Wabakaatuh.