Hadidhi ya Uongofu (103)
Assalaamu Alaykum Wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Wiki iliyopita tulijadili moja ya tabia mbaya za kimaadili nayo hatua ya mtu kumuwekea kinyongo mwenzake.
Tulisema kuwa, kinyongo na kuwa na undani na mtu yaani kumuwekea kinyongo ni miongoni mwa sifa mbaya za kimaadili ambayo hupelekea kuibuka katika moyo mtu masuala kama husuda na ghadhabu.
Sifa hii mbaya huwa na taathira katika pande zote mbili yaani upande wa kimwili na wa kiroho. Aidha tulisema kwamba, mtu mwenye chuki na kinyongo hushindwa kufanya amali njema na mambo mazuri na huwa hayuko tayari kukubali kwamba, fulani amefanya jambo jema na zuri na akiri na kulikubali hilo. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 103 kitazungumzia suala la kususiana, kutosemeshana au kununiana na kuhasimiana yaani kukosa kuwa na ushirikiano. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio niliyokuandalieni kwa juma hili.
Qur'ani Tukufu inalihesabu suala la watu kukata mawasiliano na maingiliano na ndugu na jamaa zao kuwa ni katika sifa zao watu waovu. Aidha watu wanaokata udugu na kuvunja udugu na ndugu na jamaa zao, wanakabiliwa na maneno mbalimbali ya vitisho. Imam Sajjad AS amesema alipokuwa akimuusia mwanawe Imam Muhammad Baqir AS: … Ewe mwanangu! Jihadhari kufanya urafiki na watu ambao wamekata udugu na wanaamiliana vibaya na jamaa na watu wao wa karibu, kwani mimi nimewapata sehemu tatu katika Qur'ani Tukufu wakiwa ni Maluuni yaani ni wenye kulaaniwa. Kisha baada ya kusema hayo, Imam Sajjad AS akasoma aya za 24 na 25 za Surat Muhammad zinazosema:
Je! Hawaizingatii hii Qur'ani? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli? Kwa hakika wanaorudi nyuma baada ya kwisha wabainikia uwongofu, Shetani huyo amewashawishi na amewaghuri.
Kadhalika Imam Sajjad AS akasoma aya ya 25 katika Surat Ra'ad inayosema:
Na wale wanaovunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuzifunga, na wanakata aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya fisadi katika nchi: hao ndio watakaopata laana, na watapata Nyumba mbaya.
Vile vile akasoma akasoma aya ya 27 iliyoko katika Surat al-Baqara inayosema:
Wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kwisha ifunga, na wakayakata aliyoamrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na wakafanya uharibifu katika nchi; hao ndio wenye khasara.
Kwa hakika mwanadamu ni kiumbe mwanajamii ambaye ana haja ya kuwa na mahusiano, mawasiliano na maingiliano na watu wengine katika jamii anayoishi. Hitajio hili sio la kimwili tu, bali kimsingi ni hitajio muhimu na la ndani la kisaikolojia. Hivyo basi, kubakia na kujiweka mbali na mahusiano kama haya ni jambo gumu mno. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana dini za mbinguni, zinautaja wema na kuwa na muamala mzuri kwa ndugu na watu wa karibu na kuwa na mahusiano nao ya kidugu na kihuba ni jambo lenye umuhimu mkubwa sana.
Kurekebishwa na kuimarishwa mahusiano ya kifamilia, huifanya jamii ifanye harakati kuelekea upande wa uwiano na hivyo kupata saada na mafanikio. Amma kinyume chake, yaani kukata uhusiano, kwanza huifanya familia na kisha jamii kuelekea upande wa kusambaratika na kuangamia. Ni kwa kuzingatia umuhimu huo ndio maana Bwana Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa, Mwislamu kununiana na kutosema na ndugu yake Mwislamu, ni mithili ya kumwaga damu yake. Wakati Imam Ali as alipokuwa katika lahadha zake za mwisho za uhai wake aliuusia yafuatayo: "Wanangu! Shikamaneni pamoja, sameheaneni na fungamaneni na suala la kila mmoja kumtendea wema mwenzake na jiepushe na suala la kutengana.
Katika suala la kufutukiana au kutosemeshana na kununiana na matokeo yake kutengana, mtu huzingatia zaidi katika hali ya kawaida, suala la sifa, maneno na muamala hasi wa upande wa pili. Hii ni katika hali ambayo, katika suala la kupatana na kumaliza hali ya kuhasimiana na kukasirikiana, aina ya fikra hizi hupungua mno. Kwa msingi huo, kutosemeshana na kisha kupatana kunakotokea mara kwa mara na kuwa ni hali ya kudumu, ni jambo linaloudhi na linaloteteresha na kulegeza mazingira tulivu ya maisha. Endapo mizozo na hitilafu au ugomvi mdogo hautapatiwa ufumbuzi na mtu akawa hafikirii kulirekebisha hilo, suala hilo huandaa uwanja na mazingira ya mparaganyiko na kusambaratika jamii ya Kiislamu. Ndio maana tunaona kuwa, dini ya Uislamu inawataka watu wote ambao wamenuniana na kujitokeza hali ya hasama na kukasirikiana, wamalize haraka hitilafu baina yao ambapo kwa kuombana msamaha na kupatana waondoe mbegu mbaya za chuki na uadui katika nyoyo zao ili kwa muktadha huo wapate fursa ya kuwashinda madhalimu.
Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: Endapo watu watakata udugu na kuacha kuwatendea wema watu wao wa karibu, basi utajiri na mali zao zitaangukia mikononi mwa watu waovu na madhalimu. Imam Jaafar Swadiq AS kwa upande wake anasema kuhusiana na jambo hili kwamba, miongoni mwa dhambi zinazopelekea kutoweka na kuangamia haraka ni kukata maingiliano na mawasiliano na ndugu wa karibu. Aidha kuna baadhi ya hadithi zinaonyesha kwamba, watu wawili wanaofutukiana na kununiana wote wawili wanastahiki kulaaniwa. Mmoja wa masahaba akamuuliza Imam Swadiq AS , vipi wote wanastahiki kulaaniwa? Imam akasema kuwa, aliyenuniwa na kufanyiwa uhasama naye pia anastahiki kulaaniwa kwa sababu hajamuita na kumlingania ndugu yake maridhiano na mapatano na hafambii macho maneno yasiyostahiki ya ndugu yake.
Siku moja Bwana Mtume saw aliwaambia masahaba zake, je nikujulisheni jambo ambalo ni bora zaidi ya Swala na kufunga? Masahaba wakajibu kwa kusema, ndio Ewe Mtume wa Allah. Kisha mbora huyo wa viumbe akasema ni kupatana na kumaliza ugomvi baina yenu.
Kupitia maneno haya yya Bwana Mtume saw tunafahamu ni kwa kiasi gani suala la kupatana watu waliohasimiana na kumaliza ugomvi baina yao lilivyo na umuhimu mkubwa kiasi kwamba, Mtume saw analitaja jambo hilo kuwa ni bora kuliko kuswali na kufunga.
Imam Ali bin Abi Twalib AS amenukuliwa akisema katika hotuba moja kwamba, najikinga na madhambi ambayo yanaharakisha kumuangamiza mfanyaji wake. Mmoja wa masahaba zake akamuuliza, Ewe Amirul Muuminina! je kuna dhambi ambazo ni sababu ya kuangamia haraka mwanadamu? Akasema, ndio! Kukata udugu. Kisha akaendelea kusema, familia ambayyo ipo pamoja na wakati huo huo wanafamilia wake wanasaidiana, licha yya kuwa wanatenda dhambi, lakini Mwenyezi Mungu anawapa riziki. Na kuna familia ambayo licha ya kuwa kidhahiri ni wacha Mungu, lakini kutokana na kutengana kwao na kutokuwa pamoja Mwenyezi Mungu anawanyima riziki.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa leo cha Hadithi ya Uongofu.
Msiache kujiunga name wiki ijayo. Kwaherini.