Jan 16, 2018 13:34 UTC
  • Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.
    Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.

Ni wasaa na wakati mwingine wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia suala la kususiana, kutosemeshana au kununiana na kuhasimiana yaani kukosa kuwa na ushirikiano.

Tulisema kuwa, Qur'ani Tukufu inalihesabu suala la watu kukata mawasiliano na maingiliano na ndugu na jamaa zao kuwa ni katika sifa za watu waovu. Tulieleza kwamba, katika suala la kufutukiana au kutosemeshana na kununiana na matokeo yake kutengana, mtu huzingatia zaidi katika hali ya kawaida, suala la sifa, maneno na muamala hasi wa upande wa pili. Aidha tulibainisha kwamba, kutosemeshana na kisha kupatana kunakotokea mara kwa mara na kuwa ni hali ya kudumu, ni jambo linaloudhi na linaloteteresha na kulegeza mazingira tulivu ya maisha. Endapo mizozo na hitilafu au ugomvi mdogo hautapatiwa ufumbuzi na mtu akawa hafikirii kulirekebisha hilo, suala hilo huandaa uwanja na mazingira ya mparaganyiko na kusambaratika jamii ya Kiislamu. Ndio maana tunaona kuwa, dini ya Uislamu inawataka watu wote ambao wamenuniana na kujitokeza hali ya hasama na kukasirikiana, wamalize haraka hitilafu baina yao ambapo kwa kuombana msamaha na kupatana waondoe mbegu mbaya za chuki na uadui katika nyoyo zao ili kwa muktadha huo wapate fursa ya kuwashinda madhalimu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 104 ya mfululizo huu kitazungumzia maudhui ya kupatana na kumaliza ugomvi na uhasama. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo.

 

Kupatana maana yake ni kuweka kando hasama na ugomvi wa hapo kabla na kuanzisha tena urafiki baada ya kuwa kumejitokeza hali ya kuhasimiana na ugomvi baina ya mtu na mtu au kundi fulani na kundi jingine. Katika Qur'ani Tukufu, Mwenyezi Mungu amebainisha kwa sura tofauti thamani ya kumaliza ugomvi na uhasama na kuanzisha tena urafiki na ushirikiano. Hii kwamba, ajitokeze mtu na kuwa mpatanishi na kuondoa hitilafu na hali ya kutoelewana iliyojitokeza baina ya watu wawili ni jambo zuri na lililokokotezwa mno katika dini Tukufu ya Kiislamu. Hata hivyo, jambo linalopendwa zaidi ni mtu mwenyewe aliyefutuka na kununa achukue hatua ya kupatana na mgomvi wake au mtu aliyehasimiana naye na kuondoka hali ya ushirikiano na maelewano baina yao bila kumsubiri mtu mwingine aje kuwapatanisha.

Imam Hussein bin Ali AS anaashiria na kuzungumzia thamani kubwa ya mtu kuchukua hatua kabla ya mgomvi wake kwa ajili ya kuleta suluhu na mapatano baina yao kwa kusema: Endapo watu wawili watakosana na kujitokeza hali ya kutoelewana na kutoshirikiana baina yao, kisha mmoja wao akajitokeza na kuwa mstari wa mbele katika suluhu na mapatano, basi mtu huyo atakuwa wa kwanza kuingia peponi kabla ya mwenzake huyo.

Hata hivyo kuna haja ya kuzingatia nukta hii kwamba, mtu ambaye amemuudhi mwenzake asiwe na matarajio kwamba, mhusika huyo atarejea haraka katika hali ya kawaida na kuonyesha huba na mapenzi kama ilivyokuwa awali kabla ya ugomvi au uhasama kujitokeza baina ya pande mbili.

Endapo watu waliogombana na kuhasimiana hawataweza wao wenyewe kuchukua hatua ya kuhitimisha uhasama baina yao na hivyo kufanya hali ya suluhu na mapatano kupatikana, basi watu wengine wanapaswa kuingilia kati na kumaliza mzozo na ugomvi baina ya wahusika hao. Kwa hakika hatua ya wahusika hawa ya kuingilia kati katu haihesabiki kuwa ni udadisi na kufuatilia mambo ya watu au kujihusisha na mambo ambayo hayawahusu, bali uingiliaji huu ni jambo lenye fadhila.

 

Kwa hakika Aya za Qur'ani Tukufu  zinatilia mkazo umuhimu wa miamala kama hii ya kijamii ya upatanishi ikiwa kama ni amali njema na kumebainishwa athari na baraka tele zinazopatikana kwa mpatanishi. Katika aya ya kwanza ya Surat al-Anfal Mwenyezi Mungu anasema:

Wanakuuliza juu ya Ngawira. Sema: Ngawira ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na suluhisheni mambo baina yenu, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni Waumini.

Aidha Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 10 ya Surat al-Hujuraat kwamba:

Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.

Aya hizo na nyinginezo zinaonyesha ni kwa namna gani kazi ya upatanishi na kuleta suluhu baina ya watu wawili waliogombana na kuhasimiana ilivyokuwa ni amali njema ya kijamii na inayopendwa na Uislamu. Si hayo tu, bali Mwenyezi Mungu ameliamrisha hilo na kuwataka waumini walete suluhu na upatanishi baina ya ndugu zao waumini. Kwa maana kwamba, ni jukumu la Mwislamu kuingilia kati na kuleta suluhu na upatanishi baina ya ndugu wawili waumini waliogombana na kuhasimiana. Katika kubainisha nafasi, daraja pamoja na umuhimu wa kuwapatanisha watu, Imam Jafar Swadiq AS anasema: Wallahi! Luqman al-Hakim hakupewa hekima kwa sababu ya mali, ukoo na uwezo wa kimwili, bali yeye alikuwa mtu imara na madhubuti katika jambo la Mwenyezi Mungu na alikuwa Mcha Mungu katika njia ya Mwenyezi Mungu… Kisha Imam Swadiq AS anaendelea kusema: Luqman alipokuwa akiwaona watu wawili wanagombana au wanapigana vita, hakuwa akiwaacha ila baada ya kuwakalisha pamoja na kuleta suluhu na mapatano baina yao, na hakuwa akiondoka na kuwaacha isipokuwa baada ya kuwafanya waaache ugomvi wao na kupeana mikono yaani kupatana.

Kwa hakika kupatanisha na kuleta suluhu baina ya watu ni jambo ambalo linahitajia ujuzi na ustadi maalumu. Kwa maana kwamba, si kila mtu anaweza kuifanya kazi hiyo na hivyo kufanikiwa kuwapatanisha watu ambao wamegombana na hawana ushirikiano na mahusiano tena. Hii ni kutokana na kuwa, kama yalivyo mambo mengine, upatanishi pia unahitajia tajiriba na umahiri.

Waislamu wote ni ndugu

 

Wapenzi wasikilizaji, kuna baadhi ya wakati ili kuleta upatanishi baina ya watu waliohasimiana na kugombana mpatanishi analazimika kulipa gharama. Jambo hili ni muhimu na lenye taathira hasa katika hitilafu na mizozo ya fedha na mali. Jambo hilo ni muhimu kiasi kwamba, Imam Jafar Swadiq AS amenukuliwa akimwambia mmoja wa wanafunzi wake aliyejulikana kwa jina la Mufadhal bin Kufi kwamba: Wakati unapowaona watu wawili miongoni mwa wafuasi wetu wana ugomvi na hasama baina yao, tumia mali yangu iliyoko kwako kama amana ili wawili hao wapatane..

Jambo jingine ambalo linahitajika wakati wa kupatanisha watu na kuleta suluhu baina yao ni kutumia hata maneno yasiyo sahihi ili kuhakikisha kwamba, wahusika wanapatana.

Imam Jafar Swadiq AS amenukuliwa akisema kuwa: Maneno ni ya aina tatu. Ukweli, uongo na kuleta suluhu baina ya watu. Kisha akaulizwa. Nini maana ya kuleta suluhu na upatanishi baina ya watu? Akasema: Wakati unaposikia neno kumhusu mtu fulani na kama mhusika aliyesemwa atasikia atakasirika, basi wewe unapokutana na yule aliyesemwa, mueleze kinyume cha ulivyosikia. Mwambie, nimemsikia fulani akikitaja kwa wema kwamba, wewe uko hivi na hivi.

Kwa hakika hadithi hii inatuonyesha kwamba, ni kwa kiasi gani suala la kuhifadhi usalama, maelewano na mahusiano ya jamii lilivyo na umuhimu kwani wakati mwingine kusema ukweli kunaweza kuzusha fitina hivyo kuna haja ya kusema uongo wenye maslahi.

Kuhusiana na jambo hilo Bwana Mtume SAW amenukuliwa akisema kuwa: Kwa hakika Mwenyezi Mungu anapenda uongo ambao ni sababu ya urekebishaji na anautambua kuwa ni adui ukweli ambao ni sababu ya uharibifu.

Hata hivyo ni jambo la dharura kuchunga kiwango cha maneno yasiyo sahihi kwa ajili ya kuleta urekebishaji na haipaswi kuvuka kiwango cha lazima kwani kufanya hivyo humfanya mtu atumbukie na kunasa katika tabia mbaya ya kusema uongo.

Kwa leo wapenzi wasikilizaji tunakomea hapa. Bila shaka mmenufaika na yale niliyokuandalieni kwa leo. Tukutane tena juma lijalo saa na wakati kama wa leo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh