Feb 20, 2018 23:40 UTC
  • Jumatano, Februari 21, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 4 Mfunguo Tisa Jamadithani 1439 Hijria sawa na Februari 21, 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, alizaliwa Reinhart Dozy, mtaalamu wa masuala ya mashariki mwa dunia mwenye uraia wa Uholanzi. Dozy alizamili katika fani za historia na lugha huku akifikia daraja ya PHD katika fani ya fasihi akiwa na umri wa miaka 24. Reinhart Dozy alipendelea sana kusomea tamaduni za Kiislamu ambapo mbali na kuwa mahiri katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani, alikuwa pia mtaalamu katika lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Uholanzi alifanya utafiti mwingi wa tamaduni za Kiarabu na historia ya Kiislamu, hususan Waislamu wa Andalusia, kusini mwa Uhispania. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Historia ya kisiasa na tamaduni za Kiarabu katika Andalusia' 'Historia ya Uislamu kuanzia mwanzo wake hadi katikati ya karne ya 19' na 'Tamaduni za mavazi ya Kiislamu.' Reinhart Dozy alifariki dunia mwaka 1883.

Reinhart Dozy

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, inayosadifiana na 21 Februari 1916 vilianza vita vikubwa vya umwagikaji damu vilivyojulikana kwa jina la 'Verdun' kati ya Ujerumani na Ufaransa.

Vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa miezi kumi vilimalizika kwa kushindwa vikosi vya Ujerumani na wanajeshi karibu milioni moja wa nchi hizo mbili kuuawa. Kushindwa huko ni miongoni mwa sababu za kushindwa Ujerumani kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.

Tarehe 4 Jumadi Thani miaka 64 iliyopita Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi akiwa pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.

Navvab Safavi

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, wananchi wa Misri na Syria walishiriki kwenye kura ya maoni ya kuunganisha nchi mbili hizo chini ya Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Wananchi wa nchi hizo mbili walimchagua Jamal Abdul-Nasser kiongozi wa wakati huo wa Misri, kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Baada ya kupita miezi kadhaa, Yemen nayo ilijiunga kwenye muungano huo. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa zaidi ya miaka mitatu, kwani Syria ilitangaza kujitoa kwenye muungano huo kutokana na kutoridhishwa na uongozi wa Jamal Abdul-Nasser.

Na siku kama ya leo 53 iliyopita, Malcolm X, Mmarekani mweusi aliuawa baada ya kushambuliwa na magaidi nchini humo. Malcolm X alizaliwa mwaka 1925, na wakati alipokuwa kwenye rika la ujana alifahamiana na makundi ya vijana wa Kiislamu na hatimaye akasilimu. Itikadi ya mwanaharakati huyo wa Kiislamu iliwachukiza watawala wa Marekani na makundi ya ubaguzi wa rangi nchini humo. Malcolm X aliuawa akihutubia mkutano. Alikuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, Wamarekani weusi ambao wanakandamizwa na kubaguliwa na serikali ya Marekani wanaweza kujipatia uhuru na uadilifu chini ya mwavuli wa utawala wa Kiislamu.

Malcolm X