Ijumaa 23 Februari, 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 6 Jamadithani 1439 Hijria sawa na Februari 23, 2018.
Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita Abdulmalik Rigi kiongozi wa kundi la kigaidi la Jundullah lenye makao yake huko Pakistan, alitiwa mbaroni katika oparesheni tata ya kiintelijinsia iliyofanywa na maajenti wa Wizara ya Usalama wa Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya kufanya mashambulizi mengi ya kigaidi, gaidi huyo katili alikuwa safarini kuelekea nchini Kyrgyzstan akitokea Dubai, Imarati, kwenda kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani. Hata hivyo maafisa usalama wa Iran waliokuwa wakifuatilia kwa karibu nyendo zake waliweza kuitambua ndege iliyokuwa imembeba gaidi huyo na kuisubiri iingie katika anga ya Iran na hivyo kuilazimisha kutua katika uwanja wa ndege wa Bandar Abbas wa kusini mwa Iran na baadae wakamtia mbaroni kiongozi huyo wa kundi la kigaidi la Jundullah. Rubani wa ndege hiyo alifanya jitihada kubwa za kutoroka na kutoka nje ya anga ya Iran, lakini alizidiwa nguvu na maafisa usalama wa Iran, na kulazimishwa kuishusha chini ndege hiyo kabla haijaingia kwenye anga ya Imarati. Abdulmalik Rigi alifanya jinai nyingi ikiwa ni pamoja na kutega na kuripua mabomu katika maeneo ya umma nchini Iran, kuwauwa kwa umati raia pamoja na kuwateka nyara. Rigi hakuwa na huruma hata kwa watu wake wa karibu. Abdulmalik Rigi alikiri kwamba alikuwa anapata misaada ya kila namna ikiwemo ya kifedha na kisilaha kutoka kwa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kama njia ya kuliwezesha kundi lake lifanye mauaji ya watu ndani ya Iran hususan katika maeneo ya kusini mashariki mwa Iran na kusababisha mizozo ya kimadhehebu katika maeneo hayo. Gaidi huyo alinyongwa tarehe 30 Khordad mwaka 1389 Hijria Shamsia sawa na tarehe 20 Juni, 2010 Milaadia yaani miezi minne baada ya kutiwa mbaroni. Kukiri huko kwa Rigi kunaonyesha wazi madai ya uwongo ya serikali ya Marekani ya eti inapambana na ugaidi.
Tarehe Nne mwezi Esfand miaka 38 iliyopita, Ayatullah Dakta Muhammad Husseini Beheshti aliteuliwa kuwa mkuu wa kwanza wa Mahakama Kuu ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Hatua hiyo ilichukuliwa na Imam Ruhullah Khomeini baada ya kupasishwa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu na kuundwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge. Dakta Beheshti alikuwa miongoni mwa wanafikra wakubwa na shakhsia mashuhuri wa Mapinduzi ya Kiislamu. Msomi huyo aliuawa kigaidi katika shambulizi la bomu lililotekelezwa na kundi la kigaidi la MKO mwaka 1360 Hijria Shamsia.
Siku kama ya leo miaka 219 iliyopita, Napoleon Bonaparte mfalme wa Ufaransa, alianza kuishambulia Sham, ambayo wakati huo ilikuwa ikiundwa na nchi za Syria, Jordan, Lebanon na Palestina. Mashambulio ya Bonaparte dhidi ya Misri yalifanyika kwa lengo la kutoa pigo kwa Uingereza iliyokuwa mkoloni wa Misri. Sababu ya mashambulio ya Napoleon Bonaparte dhidi ya Sham iliyokuwa sehemu ya ardhi ya utawala wa Othmania, ilikuwa ni hatua ya mfalme wa utawala wa Othmania ya kutangaza vita dhidi ya Ufaransa. Katika mashambulio hayo, na licha ya kwamba awali Bonaparte alipata ushindi, lakini baadaye alilazimika kuacha vita na kurejea kwao kutokana na uungaji mkono wa Uingereza na Urusi kwa utawala wa Othmania bila kusahau kuharibika hali ya mambo ndani ya Ufaransa.