Feb 27, 2018 02:14 UTC
  • Jumatatu tarehe 26 Februari 2018.

Leo ni Jumatatu tarehe 9 Jamadithani 1439 Hijria sawa na 26 Februari 2018.

Tarehe 26 Februari miaka 216 iliyopita yaani mwaka 1802 alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri Mfaransa, Victor Hugo. Alikuwa akitetea uhuru na usawa kwa ajili ya matabaka ya watu wote masikini. Hugo alikubaliwa kujiunga na chuo kikuu na wakati huo huo akawa mwanachama wa Baraza la Kutunga Sheria akiwa na umri wa miaka 25. Kutokana na upinzani wake dhidi ya utawala wa ukandamizaji wa Napoeleon wa Tatu alilazimika kuachana na masuala ya siasa na akaishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 20. Katika kipindi hicho Hugo aliandika vitabu muhimu na vya thamani. Miongoni mwa vitabu hivyo ni "Watu Masikini," "The Hunchback of Notre-Dame," " The Man Who Laughs" na "Toilers of the Sea". Victor Hugo alifariki mwaka 1885.

Victor Hugo

Miaka 97 iliyopita siku kama ya leo kulisainiwa mkataba wa urafiki baina ya Iran na Russia ya zamani. Katika mkataba huo ambao ulisainiwa baada ya miaka minne ya mapinduzi ya Muungano wa Sovieti ya zamani, Moscow ilitangaza kwamba, haitaendelea na siasa za kikoloni dhidi ya Iran. Kwa mujibu wa kifungu hicho muungano huo wa Sovieti uliacha kutekeleza mikataba ya huko nyuma iliyokuwa inaidhuru Iran. Katika mkataba huo wa urafiki, Moscow ilitangaza kuwa haiitambui mikataba yote iliyowekwa na utawala wa tatu wa Tzar dhidi ya Iran. Hata hivyo Urusi ya zamani haikuipatia Iran ardhi za Caucasia na Turkmenistan zilizopo Kaskazini Magharibi na Mashariki mwa Iran. Aidha katika mkataba huo Iran iliahidi kutoruhusu nchi nchi nyingine kutumia ardhi yake dhidi ya Urusi.

Iran na Russia ya sasa

Na miaka 62 iliyopita siku kama ya leo mwaka 1334 Hijiria Shamsia, alifariki dunia mtaalamu wa fasihi na malenga mkubwa wa Iran, Allamah Ali-Akbar Dehkhoda. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1258 Hijiria Shamsia na akawa miongoni mwa wanafunzi wa awali wa chuo cha zamani cha siasa mjini Tehran. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali Dehkhoda alikwenda Ulaya na kufanya utafiti kwa miaka 5. Alirudi Iran katika kipindi cha kuchipua fikra za kupigania uhuru, kipindi ambacho alikitumia kufanya kazi za kishairi dhidi ya utawala wa wakati huo. Kazi kubwa zaidi ya msomi huyo ni kamusi maarufu ya Dehkhoda.

Allamah Ali-Akbar Dehkhoda