Mar 05, 2018 07:15 UTC
  • Aya na Hadithi (11)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tuko pamoja nanyi katika kipindi kingine cha Aya na Hadithi ambapo leo bado tutaendelea kuzungumzia Hadithi ambazo zinatuongoza katika kufahamu maana halisi ya neema ambayo imezungumziwa na Mwenyezi Mungu katika Aya ya mwisho ya Surat At-Takaathur ambapo wanadamu wote wataulizwa Siku ya Kiama kuhusiana na neema hii muhimu.

Uchunguzi wa kina wa Aya za Sura hiyo unabaini wazi kwamba neema hiyo si katika neema hizi za kawaida za kimaada tulizopewa na Mwenyezi Mungu kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mkubwa na mtukufu kiasi kwamba hawezi kamwe kuwapa waja neema za kawaida kama vile vinywaji na chakula na kuwafanyia wema mwingine, kisha awaulize juu ya neema hizo. Bali neema inayokusudiwa hapa ni neema maalumu ambayo Mwenyezi Mungu amewajaaliwa wanadamu kwa madhumuni ya kuwaokoa kutokana na upotovu na ambayo pia inawaepusha na kughafilika na neema za kimaada humu duniani ambazo zinaweza kuwatumbukiza katika moto mkali wa Jahannam. Ni kwa msingi huo ndipo Hadithi hizo tukufu zikasisitiza kwamba neema inayokusudiwa kwenye Sura hii ya at-Takaathur ni Mtume Mtukufu (saw) pamoja na AhluBeit wake watoharifu (as).

**********

Wapenzi wasikilizaji, katika vipindi vilivyopita tuliazungumzia baadhi ya Hadithi Tukufu ambazo zinazungumzia suala hili, na leo tutagusia Hadithi nyingine ambazo zinajadili jambo hili zikiwemo zile ambazo zimepokelewa katika vitabu vya Ta'weel al-Ayaat, Tafsir Nuur at-Thaqalain na Tafsiri Kanz ad-Daqaiq kutoka kwa Sheikh Mufid kupitia kwa Muhammad bin Saib al-Kulbi ambaye amesema: 'Imam Swadiq (as) alipowasili Iraq, alienda al-Hirah ambapo Abu Hanifa alifika kwake na kumuuliza baadhi ya maswali hadi aliposema: Nifahamishe – Nifanywe kuwa fidia yako – kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema. Akasema: Unafahamu nini ewe Abu Hanifa? Akasema: Amani, afya ya kimwili na chakula (riziki).Imam Akasema: Eeh Abu Hanifa! Ikiwa Mwenyezi Mungu atakusimamisha Siku ya Kiama na kukuuliza juu ya kila chakula ulichokula na kinywaji ulichokunywa, bila shaka hilo litachukua muda mrefu sana…. Akasema basi nini maana ya neema hapa, nifanywe kuwa fidia yako? Akasema: Neema ni sisi ambao kupitia kwetu, Mwenyezi Mungu aliwaokoa wanadamu kutokana na upotovu, akawaongoza kutoka kwenye giza la upotovu kupitia kwetu na kuwaelimisha kutoka kwenye ujahili kupitia kwetu.'

 

Ndugu wasikilizaji, maana hii inasisitizwa na Aya kadhaa za Qur'ani Tukufu ambazo zimembainishia mwanadamu maana halisi ya neema kwa kukamilishwa dini ya Mwenyezi Mungu, suala ambalo limeashiriwa kupitia tukio mashuhuri la Ghadir. Suala hilo kwanza limeashiriwa katika kauli ya Mwenyezi Mungu katika Aya ya 67 ya Surat al-Maida inayosema: Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako. Na ikiwa hutafanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri.

Na Mtume Mtukufu (saw) aliwafikishia ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa kutangaza Khalifa na Wasii wake al-Imam Ali (as) na kuwataka Waislamu washikamane na Wilaya na uongozi wa Maimamu Watoharifu (as) ili waepuke upotovu na kufikia neema ya milele. Malaika Jibril (as) aliteremka akiwa amebeba ujumbe ambao umenukuliwa katika Aya ya 3 ya Surat al-Maida inayosema: Leo waliokufuru wamekata tamaa na Dini yenu; basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi. Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini.

Imam Ali (as) alizitolea hoja Aya hizi mara nyingi katika kuwakumbusha Waislamu kwamba yeye na kizazi chake baada ya Mtume Mtukufu (saw) ndio kusudio la neno 'neema' ambayo waja wataulizwa Siku ya Kiama. Hali hiyo inabainika wazi katika hotuba kadhaa za Imam Ali, baadhi zikiwa ni zile zilizonukuliwa katika kitabu cha al-Fadhail cha mwanahadithi mwema Shadhaan bin Jibrail ambapo amemnukuu Imam (as) akisema: 'Mimi ndiye yule ambaye Mwenyezi Mungu amesema kumuhusu, Bali hao ni waja waliotukuzwa. Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya kwa amri yake. Mimi ndiye kishiko madhubuti cha Mwenyezi Mungu kisichovunjika……. Mimi ndiye, Wanaulizana nini, kuhusu wilaya yangu Siku ya Kiama. Mimi ndiye neema ya Mwenyezi Mungu ambayo amewaneemeshea viumbe wake, na katika kauli yake Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema. Mimi ndiye yule ambaye Mwenyezi Mungu amesema kuhusiana nami, Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini……. Mimi ndiye yule ambaye Mtume Mtukufu (saw) amesema kunihusu: Yule ambaye mimi ni mtawala (msimamizi) wa mambo yake basi na huyu Ali ni mtawala (msimamizi) wa mambo yake……Mimi ndiye yule ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema kunihusu na pia adui yangu: Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa, yaani kuhusu wilaya (uongozi) yangu siku ya Kiama.'

**********

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji, ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha leo cha Aya na Hadithi ambacho mmekuwa mkikisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Basi hadi wakati mwingine tutakapojaaliwa kuungana nanyi tena, tunakuageni nyote kwa kusema Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.