Denmark: Tutasimama kidete dhidi ya mpango wa Trump kwa Greenland
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135028-denmark_tutasimama_kidete_dhidi_ya_mpango_wa_trump_kwa_greenland
Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen amepinga vikali juhudi mpya za Marekani za kuinunua Greenland, akitoa hotuba kali dhidi ya mpango huo, huku mvutano wa kidiplomasia baina ya pande mbili hizo ukipamba moto.
(last modified 2026-01-02T10:13:06+00:00 )
Jan 02, 2026 10:13 UTC
  • Denmark: Tutasimama kidete dhidi ya mpango wa Trump kwa Greenland

Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen amepinga vikali juhudi mpya za Marekani za kuinunua Greenland, akitoa hotuba kali dhidi ya mpango huo, huku mvutano wa kidiplomasia baina ya pande mbili hizo ukipamba moto.

Frederiksen amelaani kile alichokiita "vitisho, mashinikizo, na mazungumzo ya dharau" kutoka kwa "muitifaki wa karibu zaidi," akimaanisha Marekani bila kuitaja jina moja kwa moja, tovuti ya Al-Mayadeen ya Kiingereza imeripoti.

Frederiksen amekosoa wazo la kutwaa nchi nyingine, akiuita "mtazamo wa ulimwengu uliopitwa na wakati na usiokubalika."

Amesisitiza kuwa, "Haikubaliki kutaka kutwaa nchi nyingine, na taifa jingine, kana kwamba ni kitu ambacho mtu anaweza kununua na kumiliki. Sisi sio tunaotafuta migogoro. Lakini mtu yeyote asiwe na shaka, haijalishi kitakachotokea, tutasimama kidete kupambanua kilicho sahihi na kibaya."

Taarifa hiyo inakuja wiki kadhaa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kumteua Gavana wa Louisiana Jeff Landry kama mjumbe maalum wa Greenland. Trump ameonyesha nia ya kununua kisiwa hicho cha Aktiki kwa muda mrefu, akitoa vizingizio vya usalama wa taifa na uwezo wa kiuchumi.

Mwishoni mwa mwaka uliomalizika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark ilimwita balozi wa Marekani kufuatia ripoti za intelijensia zinazosema kwamba raia wa Marekani wamehusika kwa siri katika kuchochea upinzani dhidi ya mamlaka ya Copenhagen huko Greenland.

Aidha Umoja wa Ulaya umeonyesha mshikamano na Denmark na eneo la Greenland kufuatia tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuteua mjumbe wake maalumu katika eneo hilo.

Trump alijitokeza kwa mara ya kwanza kwa kutoa pendekezo la kununua Greenland wakati wa muhula wake wa kwanza, lakini amekuwa na hamu  ya "kumiliki" kisiwa hiki chenye madini adimu kwa kasi mpya tangu aliporejea kwenye Ikulu ya White House kwa muhula wake wa pili mnamo  mwezi Januari mwaka jana 2025.