Ijumaa, Machi 9, 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 20 Mfunguo Tisa Jumadi Thani 1439 Hijria sawa na tarehe 9 Machi, 2018 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1447 iliyopita, alizaliwa Bibi Fatima Zahra, binti mtukufu wa Mtume Muhammad (saw). Bibi Fatima Zahra alilelewa katika nyumba ya wahyi na chini ya malezi bora na mwongozo wa baba yake Mtume Muhammad (saw) na hivyo kuweza kufikia daraja za juu za ukamilifu. Bibi Fatima (as) alikuwa na nafasi kubwa katika kukabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikimkabili baba yake kutoka kwa washirikina. Mwaka wa pili Hijiria, Bibi Fatima Zahra alifunga ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) ambaye ni dhihirisho la haki, uadilifu na uchaji-Mungu katika sherehe ndogo iliyosimamiwa na Mtukufu Mtume Muhammad (saw). Vilevile Bibi Fatima akiwa na Imam Ali alifanikiwa kulea shakhsia adhimu kama Hassan, Hussein na Bibi Zainab (as). Mbali na majukumu ya kulea familia, Bibi Fatima Zahra, alijishughulisha pia na malezi ya jamii.

Miaka 564 iliyopita sawa na tarehe 9 mwezi Machi mwaka 1454 Miladia alizaliwa mvumbuzi na baharia wa Kiitalia kwa jina la Americo Vespucci. Vespucci alijishughulisha na kazi za melini kutokana na hamu yake kubwa ya kupenda ubaharia aliyoionyesha tangu akiwa kijana na hivyo kupewa cheo cha unahodha. Baharia Americo Vespucci alisafiri mara nne katika nchi isiyojulikana ambayo hadi wakati huo ilikuwa haina jina na baadaye ikapatiwa jina la mvumbuzi huyo wa Kiitalia yaani Amerika.
Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita, alizaliwa Imam Ruhullah Musawi Khomeini (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko mjini Khomein katikati mwa Iran. Imam Khomeini (MA) alianza kusoma masomo ya kidini akiwa na umri mdogo mjini hapo kabla ya kuelekea Qum kwa ajili ya masomo ya juu. Akiwa mjini Qum, Imam Ruhullah Musawi Khomeini alipata kusoma kwa maulama wakubwa na kutokana na maandalizi makubwa ya kielimu aliyokuwa nayo, haraka akafikia daraja ya ijtihadi. Mbali na fiq'hi, Imam Khomeini (MA) alitabahari pia katika elimu za falsafa, irfan na mashairi. Mwanazuoni huyo alianza harakati zake za kisiasa akiwa kijana na mapambano yake makubwa dhidi ya utawala wa Shah yalishtadi zaidi mwaka 1963. Kutokana na mapambano yake, Imam Khomeini alipelekwa uhamishoni nchini Uturuki na kisha Iraq na Ufaransa. Katika kipindi chote cha kubaidishwa kwake, Imam Khomeini (MA) alijishughulisha na malezi ya wanafunzi na kuongoza harakati za mapambano akifichua njama mbalimbali za utawala wa wakati huo nchini Iran.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita utawala wa chama cha Baath wa Iraq uliwatia nguvuni watu 90 wa familia ya Ayatullah Hakiim na kuwaua 6 miongoni mwao. Miaka miwili baadaye utawala wa Baath uliua watu wengine 9 katika familia ya Ayatullah Hakim. Ayatullahil Udhma Hakim alikuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Kiislamu aliyefariki dunia mwaka 1869. Watoto wa msomi huyo na watu wengi katika familia yake walikuwa mashuhuri kwa elimu na ushawishi mkubwa katika jamii ya Iraq. Kwa sababu hiyo utawala wa Saddam Hussein ambao ulikuwa na woga kuhusu ushawishi wa familia hiyo ulianzisha vita dhidi ya viongozi wa kidini na kuwaua shahidi watu wengi wa familia ya Ayatullah Hakim.
Tarehe 9 Machi mwaka 1992, Menachem Begin mmoja kati ya waasisi wa utawala haramu wa Israel na chama cha mrengo wa kulia cha Likud aliangamia. Begin alizaliwa nchini Russia mwaka 1913 na baba yake ambaye alikuwa Mzayuni mwenye misimamo mikali alikuwa na taathira na nafasi kubwa katika malezi yake. Akiwa na umri wa miaka 12, Begin aliasisi kikosi cha vijana wa Kizayuni na miaka miwili baada ya kuhamia huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, sawa na mwaka 1942 akateuliwa kuwa kamanda wa taasisi ya kigaidi yenye misimamo ya kufurutu ada kwa jina la "Irgun." Taasisi hiyo ilikuwa moja kati ya makundi makuu ya kigaidi na yenye misimamo mikali ya Kizayuni iliyokuwa ikitekeleza mauaji dhidi ya raia wa Palestina na kuwafukuza katika ardhi zao. Alikuwa katili sana dhidi ya raia wa Palestina kiasi kwamba David Ben Gorion ambaye pia ni miongoni mwa waasisi wa utawala haramu wa Israel alisema kuwa Begin ndiye Hitler wa kweli.