Apr 03, 2018 12:57 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 30 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tulikunukulieni kauli za Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu nchini Uingereza, Haroon Khan ambapo alibainisha ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu nchini humo na mataifa mengine ya Ulaya. Ndugu wasikilizaji, watoto katika kila nchi, ni wahanga wa vitendo vya ubaguzi katika jamii, lakini watoto wa Kiislamu barani Ulaya mbali na kukabiliwa na tatizo hilo, wanakabiliwa pia na chuki inayolenga dini ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla. Matokeo ya uchunguzi uliofanywa na mtaalamu mmoja wa masuala ya kifamilia na watoto nchini Uingereza yanaonyesha kwamba, watoto wa Kiislamu nchini humo wamekuwa wakikumbwa na vitendo vya ukatili, ubaguzi na chuki na suala hilo limekuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku. Ongezeko hilo la chuki na ubaguzi limekuwa kubwa kiasi kwamba, baadhi ya watoto wa Waislamu, wanaogopa hata kwenda misikitini.

Waislamu nchini Uingereza

Siham al-Qasim, mtaalamu wa masuala ya kifamilia na watoto wa kituo kimoja cha watoto mjini London anazungumzia uchunguzi alioufanya kuhusiana na chuki dhidi ya Uislamu na hasa inayowalenga watoto wa Kiislamu nchini humo na kusema: "Akthari ya watoto wanaeleza ukweli huu kwamba, kuwa kwao Waislamu kunayaweka maisha yao hatarini. Uchunguzi huo ambao ulifanyika kwa kushirikiana na Chuo cha King's College na pia kituo cha Kiislamu kwa ajili ya jamii mjini London, unaonyesha kwamba, watoto wa Waislamu wanahisi kutokuwa na usalama kutokana tu na dini yao." Mwisho wa kunukuu. Uchunguzi wa al-Qasim unasisitiza kwamba, kuwa na woga wa kulengwa na hujuma, ni moja ya maudhui muhimu za maisha ya kila siku ya watoto hao wa Kiislamu nchini humo. Katika uchunguzi huo, wanafunzi wa Kiislamu walisema kwamba, wakati wowote wanapofungamana na itikadi ya dini yao ya Uislamu, basi huwa wanafanyiwa maskhara na kuchekwa na daima huwa wanapewa vitisho kwamba, lazima waondoke nchini Uingereza. Akthari ya wanafunzi wa Kiislamu baada ya kufahamu kwamba mtazamo wa wanafunzi na majirani zao kuwahusu unatofautiana sana na mtazamo walionao Waislamu wenyewe, huwa wanakumbwa na matatizo mengi ya kisaikolojia.

Chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi

Kuhusiana na suala hilo Siham al-Qasim anatoa indhari kwamba, taasubi na ubaguzi huo una taathira hasi angamizi kwa watoto hao wa Kiislamu. Al-Qasim ameutambua uungaji mkono na ushirikiano wa matabaka ya kijamii kwa wahanga wa taasubi na ubaguzi, kuwa ni njia athirifu kwa ajili ya kuondoa matatizo hayo. Naye kwa upande wake Mihad Fahmi, kutoka tume ya haki za binaadamu katika Baraza la Kitaifa la Waislamu nchini Canada pia anazungumzia suala hilo kwa kusema: "Waislamu daima wamekuwa wahanga wa mitazamo ghalati na hasi inayoukabili Uislamu, hususan kutoka kwa watu ambao hawana uelewa sahihi wa Uislamu. Wao hudhani kwamba watoto wa Kiislamu wanatoka katika familia zilizosambaratika. Kwa hakika mtazamo huo sio sahihi na uko mbali na uhalisia wa mambo." Mwisho wa kunukuu.

*******************

Ongezeko la wimbi la chuki dhidi ya dini ya Uislamu barani Ulaya kuwalenga watoto wa Waislamu, linaonyesha kiini cha hatari ya wimbi hilo katika barani humo. Kama ambavyo pia linaonyesha malezi ya kizazi yaliyosimama juu ya msingi wa vinyongo na chuki kali dhidi ya wafuasi wa dini hii ya mbinguni huko barani Ulaya.

Licha ya nchi za Magharibi kujinadi kuwa watetezi wa haki za binaadamu, lakini zinafumbia macho haki hizo kwa ajili ya Waislamu

Kwa upande mwingine ni kwamba, mwenendo huo huathiri roho ya kujiamini ya watoto wa Kiislamu tangu kipindi cha utotoni. Ndugu wasikilizaji ni vyema kuashiria kwamba, moja ya mambo ambayo jamii za Magharibi zinajifakharisha nayo, ni kuheshimu suala la uhuru wa kujieleza. Katika sheria za nchi za Magharibi na hata katika tamaduni zao, Wamagharibi hujaribu kuonyesha kwamba wanaheshimu sana shakhsia ya wanadamu na matukufu yao. Hii ni katika hali ambayo, ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi huko Ulaya na katika jamii zingine za Magharibi linabainisha wazi uongo wa madai yao hayo. Hii ikiwa na maana kwamba,  vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na kwa mujibu wa uchunguzi wa Siham al-Qasim, mtaalamu wa masuala ya kifamilia na watoto wa kituo kimoja cha watoto mjini London Uingereza, vimeongezeka zaidi dhidi ya watoto wa Kiislamu. Kwa hakika hiyo ni kengele ya hatari kwa jamii ya Ulaya. Kwani kuendelea hali hiyo, kunaimarisha harakati za mrengo wa kulia zenye kufurutu mpaka na chuki dhidi ya Uislamu barani humo. Hii ni kwa kuwa harakati hiyo hadi sasa ni tishio kubwa dhidi ya mshikamano na ushirikiano wa kiutamaduni na uthabiti ndani ya nchi hizo. Aidha moja ya vyanzo ambavyo vinatajwa kuwa chanzo cha baadhi ya vijana Waislamu barani Ulaya kujiunga na harakati za makundi yenye misimamo mikali ya kuchupa mipaka na ugaidi, ni kuchanganyikiwa, kubaguliwa na kudharauliwa katika jamii za Magharibi.

Dini Tukufu ya Kiislamu inayovutia mafundisho yake

Serikali na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kwa pamoja vimekuwa vikichochea chuki dhidi ya Uislamu na wafuasi wa dini hii. Zimeweza kushirikiana na harakati zinazoeneza chuki dhidi ya Uislamu ndani ya nchi hizo na kueneza ubaguzi pamoja na kuweka mipaka na mashinikizo zaidi kwa Waislamu kama vile kuwazuia wanawake wa Kiislamu kuvaa hijabu au kuwawekea sheria kali Waislamu katika vituo vyao vya kidini pamoja na misikiti. Baada ya muda, siasa hizo huwa na taathira hasi juu ya jamii yenyewe ya Magharibi. Kwa hakika harakati za chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu, zitaiondoa jamii ya Magharibi katika wigo wa fikra sahihi na uvumilivu sambamba na kuhatarisha uthabiti na usalama wao wa kisiasa na kijamii.

*************

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako kipindi kilicho hewani ni makala ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika nchi za Magharibi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ndugu wasikilizaji Waislamu katika jamii za Magharibi na katika kukabiliana na wimbi hilo la chuki dhidi ya Uislamu hawajasalimu amri na badala yake wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali katika kuuarifisha Uislamu halisi unaolingania amani, uadilifu na uhuru katika jamii.

Mtume Muhammad (saw), ambaye alilingania ubinaadamu, upendo, uadilifu na tabia njema

Miongoni mwa hatua hizo ni kuonyesha akhlaqi nzuri ya Mtume Muhammad (saw) ambaye ni Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, akhlaqi ambayo inajumuisha tabia yake nzuri na upole. Katika Qur'ani pia tabia njema imetajwa kama moja ya ukamilifu wa akhlaqi ya mwanadamu. Ndugu wasikilizaji mtafahamu kwamba, moja ya sababu za kuenea kwa kasi Uislamu kuanzia mashariki hadi magharibi mwa dunia ikiwa ni baada tu ya kupita miaka 25 ya Utume wa Mtume Muhammad (saw), ilikuwa ni shakhsia yake ya upole na huruma. Mtume Muhammad (saw) mwenyewe alijiarifisha kuwa baba wa Umma huu, si katika zama zake tu, bali kwa ajili ya kila mwanadamu hadi siku ya Kiama. Katika miaka ya hivi karibuuni, Waislamu wa nchi za Magharibi wameongeza harakati na shughuli zao za kijami kwa ajili ya kukabiliana na harakati za chuki dhidi ya Uislamu sambamba na kuuarifisha Uislamu halisi kupitia tabia njema za Nabii huyo wa Allah. Kwa hakika moja ya tablighi muhimu inayofanywa na Waislamu ni kuiarifisha shakhsia ya Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu.

Dini ya Uislamu

Katika uwanja huo Waislamu barani Ulaya na Marekani na katika siku za kusherehekea kuzaliwa Nabii Isa (as) walibuni njia nzuri ya tablighi kukiwemo kutumia barua za pongezi katika nyumba mbalimbali, barua zenye jumbe tofauti za mafundisho ya dini ya Uislamu na zenye kubainisha nafasi ya Nabii Isa katika Qur'an Tukufu. Kwa njia hiyo Waislamu waliweza kueneza moyo wa upendo ndani ya jamii za Magharibi ambazo zina  fikra ghalati kuhusu dini ya Uislamu.

****************

Katika uwanja huo, jumuiya ya wanafunzi Waislamu mjini London sambamba na kuwadia mwaka mpya wa Miladia (2018) waligawa kadi za pongezi kwa mnasaba wa uzawa wa Nabii Isa (as) ambapo waliambatanisha na jumbe za aya za Qur'ani kumuhusu Nabii huyo wa Allah kwa ajili ya wafuasi wa dini ya Ukristo mjini humo. Aidha katika kadi hizo mbali na kuambatanisha Aya za Qur'ani Tukufu zinazomzungumzia Nabii Isa (as) na picha ya msikiti wa al-Aqsa (Kibla cha kwanza cha Waislamu duniani), pia walitoa mkono wa heri na fanaka kwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis, Malikia Elizabeth wa Uingereza, wanasiasa, viongozi wa makanisa na majirani wao Wakristo.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis, ambaye naye huwa anatumiwa barua hizo na kuzijibu

Dakta Mohammed Fahim anasema: Ni miaka kadhaa sasa ambapo katika siku za kuadhimisha mwaka mpya wa Miladia huwa kunagawiwa kadi elfu nne za mkono wa kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuzaliwa Nabii Isa (as) na ambazo huwa zimeambatanishwa na Aya za Qur'ani Tukufu na picha ya msikiti wa al-Aqsa, kwa viongozi wa serikali na makanisa nchini Uingereza lengo kuu likiwa ni kuuarifisha Uislamu sahihi kwa jamii ya nchi hiyo.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 30 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

Tags