Apr 03, 2018 14:07 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 34 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa, serikali ya Austria kwa sasa imejikita katika kuwawekea mashinikizo na kuwafuatilia Waislamu, huku ikiwataja kuwa watu hatari kwa usalama, katika hali ambayo nchi hiyo haijashuhudia matukio yoyote ya kigaidi katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Aidha wakati serikali ya nchi hiyo ikiwasakama Waislamu, mwaka 2015 pekee maafisa usalama wa Austria waliorodhesha karibu matukio 1700 ya hujuma na maudhi kuwalenga Waislamu na wahajiri, vitendo vilivyofanywa na wafuasi wa chama cha mrengo wa kulia na kufurutu ada ndani ya taifa hilo. Hata hivyo jambo la kusikitisha ni kwamba, vitendo hivyo huwa havitangazwi na vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Sebastian Kurz, Kansela wa Austria alipowahi kukutana na Waislamu wakati akihudumu katika Wizara ya Mambo ya Ndani Austria

Pamoja na uwepo wa ongezeko la vitendo hivyo kuwalenga Waislamu, ndio kwanza viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Vienna hususan Sebastian Kurz, wanapanga mipango mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi hewa eti ya Waislamu. Suala la kufaa kuashiria ni hili kwamba wakati chuki na mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Austria vinaongezeka, Waislamu wa nchi hiyo wanaishi kwa mujibu wa sheria na kuheshimu misingi ya uraia sawa raia wengine wa taifa hilo. Aidha hatua ya serikali ya Vienna ya kujikita tu katika kuwafuatilia na kuwachunguza wafuasi wa dini ya Uislamu, ni jambo ambalo lilikuwa halijawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo ya Ulaya. Ni kwa ajili hiyo ndio maana taasisi mbalimbali za kutetea haki za binaadamu nchini humo kwa mara kadhaa zikaonyesha wasi wasi wao kutokana na miamala hiyo hasi. Hii ni kwa kuwa Waislamu wana historia ya muda mrefu ndani ya taifa hilo. Ili kuthibitisha ukweli huo, hatuhitajii kupekuwa sana kuhusiana na suala hilo, kwani hata mfalme wa wakati huo wa Austria na Hungary, aliitambua dini ya Uislamu kuwa moja ya dini rasmi za nchini humo.

Waislamu barani Ulaya

Aidha tangu mwaka 1912 Mfalme Franz Joseph wa Kwanza na baada ya kuiunganisha Bosnia na Herzegovina pamoja na Austria, Uislamu ulikuwa kati ya dini rasmi zilizotambuliwa na serikali. Inafaa kuuashiria kwamba, jamii ya Waislamu wa Austria inakadiriwa kuwa ya watu laki tisa. Ni muongo wa 1960 ndipo kulishtadi wimbi la uhajiri la Waislamu kuelekea nchi hiyo. Katika uwanja huo, Waislamu walikuwa na nafasi athirifu na ya kimaendeleo kwa ajili ya Austria hususan katika kipindi cha baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Aidha katika kulinda utambulisho wao, Waislamu wa Austria walifungamana na sheria zote za serikali ambapo hawakushuhudiwa kuwa na tatizo lolote. Waislamu wa nchi hiyo walikuwa wakijifundisha lugha, wakilipa kodi kama ambavyo pia walitaka daima waonekane kuwa raia wema wa Austria. Hata hivyo pamoja na juhudi zao hizo na kwa mujibu wa İbrahim Olgun, kiongozi wa Jumuiya ya Kiislamu nchini humo, katika kipindi cha miaka 10 ya hivi karibuni, Waislamu hao wameshuhudia wimbi kubwa la chuki na ubaguzi dhidi yao jambo ambalo linahatarisha maisha yao.


****************

Katika uchaguzi wa bunge wa hivi karibuni nchini Austria vyama viwili pekee vya kufurutu ada na vyenye kueneza chuki dhidi ya Uislamu yaani chama cha Uhuru na chama cha kihafidhina cha Wananchi, viliibuka na ushindi sambamba na kuendesha kampeni mbaya ya kimashambulizi kuwalenga Waislamu.

Wimbi la chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi

Kabla ya uchaguzi huo vyama hivyo vilikuwa vimesisitizia udharura wa kupigwa marufuku vazi la burqa na mavazi mengine ya staha kwa ajili ya wanawake wa Kiislamu nchini humo. Katika uwanja huo Sebastian Kurz, kiongozi wa chama cha Wananchi na ambaye pia ni Kansela kijana zaidi katika historia ya Austria, anaifahamu vyema historia ya kuvutia ya jamii ya Waislamu wa nchi yake hasa kwa kuzingatia kuwa, utendajikazi wake katika siasa aliuanzia ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo, Carla Amina Baghajati, Msemaji wa Taasisi ya Waislamu nchini Austria ambaye kwa muda fulani aliwahi kufanya kazi na Kurz siku za nyuma anasema: "Ninakumbuka safari moja katika kikao, kundi moja la wanawake wa Kiislamu lilikutana naye kwa muda mrefu ambapo lilimtaka kuwaondolea matatizo yaliyowakabili. Katika hali ya kushangaza ni kwamba jioni ya siku hiyo ofisi ya Sebastian Kurz, iliwapigia simu wanawake hao na kuwambia kuwa, matatizo yao yametatuliwa." Mwisho wa kunukuu.

Waislamu nchini Austria

Hata hivyo na baada ya kupita muda mwingi na kufuatia kupanda cheo katika ulingo wa kisiasa, ghafla kiongozi huyo aligeuka na kuwa mmoja wa waendesha propaganda chafu na za chuki dhidi ya Uislamu. Katika uwanja huo, Joseph Hotchal mmoja wa wanachama wakongwe wa chama cha Wananchi nchini Austria anasema: "Kuna udharura wa kubadili mfumo wa siasa zetu hasa kwa kuzingatia hali ya mambo tunayoishi ndani yake na inaonekana pia hata Sebastian Kurz  naye anaendesha siasa zake kwa mujibu wa mwenendo huo." Mwisho wa kunukuu.

 

**********

Ndugu wasikilizaji mwaka 2015 nchi nyingi za Ulaya zilikumbwa na wimbi la wahajiri ambao kimsingi walitoka mataifa yaliyokumbwa na migogoro ya vita ikiwemo pia Syria. Mwaka 2016 na 2017 hatua kali ambazo zilichukuliwa na mataifa hayo ya Ulaya kwa ajili ya kufunga njia ambayo awali ilikuwa ikitumiwa na wahajiri na wakimbizi, zilipelekea kupungua wimbi hilo la wahajiri. Hii ni katika hali ambayo kituo cha kwanza cha Waislamu waliokuwa wanaelekea Ulaya, kilikuwa ni Austria. Mwaka 2015 karibu wahajiri elfu 90 waliingia Austria, idadi ambayo ni sawa na karibu asilimia moja ya jamii yote ya nchi hiyo. Mwaka mmoja baadaye Sebastian Kurz na akiwa na cheo cha Waziri wa Mambo ya Nje alitoa amri ya kufungwa njia ya Rasi ya Balkan kwa ajili ya kuwazuia wahajiri hao.

Wimbi chafu la chuki dhidi ya Uislamu nchini Austria

Kuhusiana na suala hiyo Joseph Hotchal, mjumbe mwandamizi wa chama tawala cha Wananchi anasema: "Ikiwa tutaendelea kuwapokea wahajiri, si tu kwamba jambo hilo litasababisha kuharibiwa mfumo wetu wa kiutamaduni, bali pia litasababisha kusambaratisha mfumo wa kijamii wa nchi. Ni kweli kwamba ni lazima kutofautisha kati ya Uislamu wa kawaida na Uislamu wa asili, kwa kuutimua Uislamu wa pili." Mwisho wa kunukuu. Kwa hakika kitendo cha kuugawa Uislamu katika makundi mawili, ya Uislamu wa kawaida (Uislamu usiozingatia sana mafundisho ya dini) na ule wa kihafidhina (Unaoenda sawa na mafundisho asili) kimsingi kina lengo la kuhalalisha siasa za chuki na ubaguzi dhidi ya dini hiyo. Watu wa Ulaya wanawafahamu Waislamu wenye kushikamana na misingi ya dini yao, kuwa ndio wale wanaotenda jinai na ugaidi, suala ambalo kwa hakika halina mahusiano yoyote na Uislamu wa Bwana Mtume Muhammad (saw). Hii ni kwa kuwa dini hii ya mbinguni haina mahusiano hata kidogo na uchupaji mipaka, wala ugaidi. Bali ni dini ya amani, uadilifu, upendo na kulingania kuishi pamoja watu wa dini nyingine tofauti kwa namna ya uhuru na amani.

Waislamu wakiswali

Waislamu wameweza kuwathibitishia watu wa Ulaya kuhusiana na suala hilo. Kuwepo jamii ya wachache wanaoishi ndani ya nchi za Kiislamu kwa uhuru na amani, licha ya wao kuwa na dini nyingine isiyo ya Uislamu, kunabainisha ukweli huu kwamba Waislamu, ni watu wa amani na upendo kinyume na propaganda chafu zinazoenezwa na maadui wa dini hii. Madola ya Magharibi yanataka Uislamu ule ambao umesimama juu ya misingi ya mafundisho ya Usekulari. Ni kwa ajili hiyo ndio maana kila mara kunazidishwa mashinikizo na vikwazo dhidi ya Uislamu asili. Kwa hakika siasa hizo zinakinzana pia na misingi ya uliberali ambao unadaiwa kuheshimu  uhuru wa itikadi au uhuru wa kujieleza.

 

**************

Siasa za chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu zinazotekelezwa na madola ya Magharibi, zimefikia kiwango hata cha kuhatarisha maisha ya mamilioni ya Waislamu wanaoishi nchi hizo mkabala wa wafuasi wa dini nyingine.

Vazi la hijabu likitetewa na wanawake wa Kiislamu baada ya kupigwa na marufuku Ulaya

Matokeo ya siasa hizo hasi za madola ya Magharibi, yanaendelea kudhihiri kila uchao na kumfanya kila mtu aweze kufahamu ukweli wa mambo. Ndugu wasikilizaji nchini Austria kama zilivyo nchi nyingine, watoto wote wanaozaliwa ndani ya dakika au saa za mwanzo wa mwaka mpya wa Miladia, huwa wanatangazwa na familia zao kupongezwa. Katika uwanja huo, mwaka huu 2018, familia moja ya Kiislamu nchini Austria ilipata mtoto ambaye alizaliwa mwanzoni mwa mwaka huo. Baada ya picha za baba na mama wa mtoto huyo kuenea katika mitandao ya kijamii, watu wa nchi hiyo na katika kuonyesha chuki yao dhidi ya Uislamu, waliandika kando ya picha hizo maneno yaliyosema, 'gaidi mwingine amezaliwa.'

Mtoto wa kwanza kusaliwa nchini Austria mwaka 2018, ni huyo mtoto wa Kiislamu

Aidha mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Herbert Kickle alimtaka waziri mpya wa mambo ya ndani wa nchi hiyo na anayetoka chama cha mrengo wa kulia na chenye misimamo mikali, kuifukuza familia ya mtoto huyo Austria. Matukio hayo pamoja na mengine, yanaonyesha ni kwa kiasi gani chuki dhidi ya Uislamu nchini humo ilivyoshika kasi na kuwa hatari kwa maisha ya Waislamu.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 34 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

Tags