Apr 12, 2018 16:05 UTC
  • Alkhamisi tarehe 12 Aprili. 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 25 Rajab 1439 Hijria sawa na 123 Aprili 2018.

Siku kama ya leo miaka 1281 iliyopita, Zaid bin Ali bin Hussein, mjukuu wa Imam wa Tatu wa Waislamu wa Kishia, alipeperusha bendera ya harakati yake huko mjini Kufa, Iraq wakati wa utawala wa Bani Umayyah. Mapambano ya Zaid ambayo wafuasi wake walitambuliwa kwa jina la Zaidiyyah, yalidumu kwa muda mrefu ambapo mwaka 739 Miladia, aliuawa shahidi na Yusuf Ibn Omar Thaqafi, mmoja wa watawala wa Bani Umayyah. Kufuatia matukio hayo, baadhi ya wafuasi wa kiongozi huyo (Zaid bin Ali) ambao hawakuwa Wairani walihamia nchini Yemen na kuasisi harakati yao ambayo hii leo inafahamika kwa jina la Harakati ya Waislamu wa Shia Zaidiyyah. Ni bora ikafahamika kuwa, hii leo nusu ya jamii ya Wayemen inaundwa na Mashia Zaidiyyah, Shia Ithna Ashariyyah na Shia Ismailia. Maeneo ambayo wanapatikana zaidi jamii ya watu hao ni kaskazini mwa taifa hilo la Kiarabu.

زید ابن علی ابن حسین

Siku kama ya leo miaka 1256 iliyopita, Imam Musa Kadhim (as) mmoja wa wajukuu watoharifu wa Mtume Mtukufu (saw) aliuawa shahidi. Imam Kadhim (as) alizaliwa mwaka 128 Hijiria huko katika eneo la Ab'waa lililoko baina ya miji mitakatifu ya Madina na Makka. Mtukufu huyo kwa miaka 20 alipata malezi na elimu muhimu kutoka kwa baba yake ambaye ni Imam Jaafar as-Swadiq (as). Baada ya kuuawa baba yake huyo, Imam Kadhim (as) alipata fursa ya kuuongoza umma wa Kiislamu kwa muda wa miaka 35, ambapo alipata mateso na mashaka mengi katika njia hiyo. Katika zama zake ambazo zilisadifiana na ustawi mkubwa wa utamaduni na elimu ya Kiislamu pamoja na kuimarishwa uhusiano na mataifa ya kigeni, Imam alifanya juhudi kubwa za kueneza mafunzo ya Kiislamu katika mataifa hayo kupitia wanafunzi wake. Mbali na hayo, Imam pia aliendesha mapambano makali dhidi ya watawala dhalimu wa Bani Abbas. Hatimaye Haroun ar-Rashid kutoka ukoo wa Bani Abbas aliyehofia sana kuporomoka kwa utawala wake, alimfunga jela Imam Kadhim (as). Licha ya kufungwa jela lakini Imam (as) hakusimamisha shughuli zake za kuhubiri dini na kupambana na madhalimu bali alifundisha na kuwaelimisha watu waliokuwa pembeni yake hali halisi ya mambo iliyotawala katika zama hizo. Hatimaye Haroun ar-Rashid alifanya njama ya kumuua Imam kwa kumpa sumu. Huku tukitoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kuuawa shahidi Imam Kadhim (as), tunakunukulieni hapa moja ya semi zake zenye mafunzo na busara kubwa. Imam anasema: 'Njia bora zaidi ya kumkurubia Mwenyezi Mungu baada ya kumjua ni kusimamisha swala, kuwatendea wema wazazi wawili na kuachana na husuda na majivuno.'

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita dawa ya kutibu ugonjwa wa malaria iligundulika kutoka kwenye magamba ya mti wa Cinchona. Asili ya mti huu wenye majani ya kijani kibichi ni maeneo ya Amerika ya Kusini lakini hii leo unapandwa katika ameneo mengine ya dunia. Utomvu wa mti huu hutumika kutengeneza dawa chungu sana ya Quinine. Tarehe 12 Aprili mwaka 1820 kwa mara ya kwanza kabisa madaktari Pierre Joseph Pelletier na Joseph Bienaimé Caventou wa Ufaransa walifanyika majaribio dawa hiyo ya malaria katika Maabara ya Paris na kukaanza jitihada za kuzalisha dawa ya Quinine. 

Miaka 86 iliyopita sawa na tarehe 12 Aprili 1932 mfumo wa jamhuri uliasisiwa kwa muda huko Uhispania na utawala wa kisultani ukafikia ukomo. Wananchi wa Uhispania waliokuwa wakipigania mfumo wa jamhuri waliendesha mapambano dhidi ya utawala wa kimabavu na kidikteta wa Alphonce wa 13 Mfalme wa wakati huo wa Uhispania na kumlazimisha kujiuzulu.

Uhispania

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika katika anga za mbali na kuizunguka dunia. Siku hiyo Yuri Gagarin mwanaanga wa Urusi ya zamani aliyekuwa na umri wa miaka 27 aliizunguka dunia kwa dakika 89 kwa kutumia chombo cha anga za mbali kwa jina la Vastok 1 na kwa msingi huo kukapatikana mafanikio makubwa katika sekta ya masuala ya anga. Gagarin alifariki dunia akiwa pamoja na mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa sekta ya masuala ya anga wa Urusi ya zamani katika ajali ya ndege hapo mwaka 1968.

Yuri Gagarin