Apr 17, 2018 09:55 UTC
  • Aya na Hadithi (20)

Assalaam Aleikum wasikilizaji wapenzi wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikiliza sehemu nyingine mpya ya kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambapo kwa juma hili tutazungumzia maandiko matakatifu ambayo yanatuongoza katika kuelewa misdaki na mifano halisi ya watu wanaomnusuru Mwenyezi Mungu kikweli kweli na kwa ikhalsi ambapo kutokana na hilo, Mwenyezi Mungu naye huwanuru kiuhalisi na kwa mifano iliyo wazi.

Hao ndio wema ambao wametajwa na Mwenyezi Mungu katika Aya za 38 hadi 41 za Surat al-Haj ambazo tunazitegea sikio kwa pamoja. Aya hizo Tukufu zinasema: Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila khaini, mwenye kukufuru sana. Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu! Na lau Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu kwa watu, basi hapana shaka yangelivunjwa mahekalu na makanisa na masinagogi na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humnusuru yule anayemnusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye enzi. Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Swala na wakatoa Zaka, na wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote.

 

Wapenzi wasikilizaji, tunapozingatia kwa kina Aya hizi Tukufu tunaona kwamba zinatubainishia wazi suna na taratibu zisizobadilika za Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kusaidia na kuwanusuru waumini katika makabiliano yao na mahaini sugu wenye kukufuru. Bila shaka nusura hii ya Mwenyezi Mungu ni ya kudumu katika mapambano marefu dhidi ya maadui wa dini, mapambano ambayo kwa yakini mwisho wake ni kufikiwa matakwa na mapenzi ya Mwenyezi Mungu kama inavyoashiria Aya ya mwisho kati ya Aya hizo tulizosoma. Nusura hii ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake waumini huanzia pale anapowaruhusu kupigana Jihadi ambayo kwa hakika ni ya kujieteta na kujilinda kutokana na hujuma ya maadui. Hii ni kwa sababu ruhusa ya kupigana Jihadi na kujitetea, ilitolewa kwa wale waliodhulumiwa na kufukuzwa kidhulma kutoka kwenye nyumba zao. Walikabiliwa na dhula mara tu walipoamua kumuabudu Mungu Mmoja na kukiri kwamba Mola wao ni Mwenyezi Mungu. Hivyo walishambuliwa na kudhulumiwa kutokana na imani yao hiyo kwa Muumba wao na katika hali hiyo, Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kuwatetea na kuwalinda kutokana na shari ya wahaini wanaofanya juhudi za kuwazuia watu kumuabudu Yeye. Wale wanaoruhusiwa kupigana Jihadi na kisha kupata msaada na nusura ya Mwenyezi Mungu katika vita hivyo vitakatifu ni kundi maalumu la waumini ambao sifa yao kuu na ya kipekee ni kuwa wanaamini na kumtakasia ibada Mweyezi Mungu tu. Huwa hawatafuti radhi za mtu mwingine katika Jihadi hiyo ila za Mwenyezi Mungu na hii ndio maana ya kumnusuru Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu anapowanusuru waumini hao na kuwamakinisha kwenye ardhi, yaani kuwapa madaraka na uongozi, huwa hawasiti katika kusimamisha Swala, kutoa Zaka na kuamrisha mema na kukataza mabaya.

***********

Wapendwa wasikilizaji, jambo linalombainikia wazi mtu anayezingatia Aya Tukufu tulizotangulia kusoma linafafanuliwa zaidi na Hadithi kadhaa ambazo zimenukuliwa katika vitabu vyetu vya kuaminika ambapo tuzitapitia kadhaa hivi punde ili tupate kunufaika zaidi na jambo hili. Moja ya Hadithi hizo ni maneno ya Amir al-Mu'minun, al Imam Ali (as) ambapo anasema kuwa Jihadi iliyoruhusiwa na Mwenyezi Mungu ni ile inayohusiana na kundi maalumu la mawalii Wake, yaani waumini walio na imani madhubuti na yenye ikhlasi. Wao ndio wanaonufaika na nusura ya Mwenyezi Mungu kwa sababu huwa ni wakweli katika kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Imam Ali (as) anasema mwanzoni mwa hotuba yake ambayo imenukuliwa na Thiqatul Islam al-Kuleini katika kitabu chake cha al-Kafi: 'Kwa kweli Jihadi ni mlango miongoni mwa milango ya Peponi, Mwenyezi Mungu ameufungua kwa ajili ya wapenzi Wake maalumu. Nayo (Jihadi) ni vazi la ucha-Mungu, na ni ngao ya Mwenyezi Mungu yenye kuhifadhi, na sitara yake ni thabiti.'

 

Wapenzi wasikilizaji, hivi ndivyo inavyotubainikia wazi kwamba wale wanaojipamba kwa sifa nzuri ya ucha-Mungu ndio waliofunguliwa mlango wa kupigana Jihadi kwa njia ya Mwenyezi Mungu na kuruhusiwa kutekeleza ibada hiyo muhimu. Wao ndio wanaonusuriwa na Mwenyezi Mungu na irada yake kusimamisha kupitia kwao, dola lake lililosimama juu ya msingi wa mafudisho ya dini. Hii ni kwa sababu wao huwa hawafuatilii jambo lolote lile isipokuwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kutekeleza uadilifu Wake duniani na wala sio kama wanavyofanya baadhi ya watawala katika kutekeleza irada na matakwa ya mataghuti kama walivyofanya watawala wa Bani Ummayia na Bani Abbas na wale wote wanaowafuata hadi leo kwa kisingizio cha dini. Hebu tuzingatie kwa pamoja sehemu hii ya barua iliyonukuliwa katika kitabu cha al-Kafi na ambayo iliandikwa na Maulana Abu Ja'ffar al-Imam Baqir (as) kwa baadhi ya watawala wa Bani Ummayyia ambapo alisema (as): 'Na katika hayo na yale yaliyopotosha Jihadi ambayo imefadhilishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya amali na kumfadhilisha anayeitekeleza juu ya watekelezaji wa mambo mengine, fadhila katika daraja, maghfira na rehema. Hii ni kwa sababu alidhihirisha dini kupitia Jihadi, kuilinda kwayo na Mwenyezi Mungu kununua nafsi na mali za waumini kwayo, ambapo Naye aliwauzia Pepo kupitia mauzo yenye mafanikio na yanayookoa. Aliwashurutisha wachunge mipaka kwenye Jihadi hiyo, la kwanza likiwa ni kuita watu kwenye utiifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na sio utiifu kwa wanadamu, kumwabudu Mwenyezi Mungu badala ya kuwaabudu wanadamu na kufuata wilaya ya Mwenyezi Mungu badala ya wilaya ya wanadamu…..na sio kuwaita watu wawatii wanadamu kama wao (wenzao).'

**************

Wapenzi wasikilizaji, katika kipindi chetu cha juma lijalo Inshallah, tutaendelea kujadili Aya hizi zinazozungumzia sifa za wale walioruhusiwa na Mwenyezi Mungu kupigana Jihadi, Aya ambazo kama tulivyoona zinafafanuliwa zaidi na Hadithi zilizopokelewa kutoka kwa Nyumba ya Watu wa Mtume (saw). Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Aya na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags