Ulimwengu wa Spoti, Apr 30
Ufuatao ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita......
Basketboli: Iran yaibuka ya 2 Michezo ya Vyuo Vikuu Ubelgiji
Timu ya mpira wa kikapu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka katika nafasi ya pili kwenye duru ya 19 ya Mashindano ya Kimataifa ya Basketboli ya Vyuo Vikuu PCU huko Ubelgiji. Vijana wa Kiirani walikosa kosa kutwaa ubingwa baada ya kukubali kuchachawizwa vikapu 62-60 kwenye fainali walipovaana na Chuo Kikuu Taifa cha Catalan mjini Antwerp, nchini Ubelgiji siku ya Ijumaa.
Awali vijana hao wa Kiiarani waliwabamiza mahasimu wao wa Chuo Kikuu cha Masuala ya Fedha cha Russia vikapu 10-2. Mashindano hayo ya kimataifa ya vyuo vikuu yalianza Aprili 25 na kumalizika siku mbili baadaye, katika mji wa Antwerp ulioko kaskazini mwa Ubelgiji. Makumi ya wanachuo kutoka nchi za Ubelgiji, Croatia, Uingereza, Ujerumani, Iran, Italia, Lebanon, Russia, Scotland na Uhispania wameshiriki mashindano hayo.
Soka Iran: Persepolis yakabidhiwa rasmi tuzo
Klabu ya Persepolis ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo ilitangazwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka hapa nchini kwa mwaka wa pili mfufulizo, mapema mwezi Aprili baada ya kuichachafya klabu ya Padideh bao 1-0, hatimaye imekabidhiwa rasmi taji hilo. Klabu hiyo ilikabidhiwa kombe hilo siku ya Ijumaa katika Uwanja wa Michezo wa Azdi hapa mjini Tehran, na kutangazwa rasmi kuwa mshindi wa Duruy a 17 ya Ligi Kuu ya Soka hapa nchini inayojulikana pia kama Ligi ya Wataalamu IPL. Mashabiki wa Wekundu wa Tehran walimiminika mabarabarani kusherehekea ushindi huo.
Klabu ya Zob Ahan imetangazwa kuwa mshindi wa pili huku Esteqlal ikifunga orodha ya tatu bora msimu huu. Aidha katika sherehe hizo za Ijumaa, kiungo nyota wa Persepolis, Ali Alipour alikabidhiwa tuzo ya mfungaji bora wa msimu, kwa kufunga jumla magoli 19.
Hii ni mara ya 11 kwa Wekundu wa Tehran kutwaa taji hilo. Mwaka jana, klabu hiyo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka hapa nchini baada ya kuichachafya klabu ya Machine Sazi ya Tabriz mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Yadegare-Imam mkoani Tabriz, kaskazini mashariki mwa nchi, na hiyo kutia kikomo ukame wa miaka tisa wa kutoshinda taji hilo. Persepolis ilishinda taji hili kwa mara ya kwanza katika msimu wa ligi ya mwaka 2001-2002 huku wakitwaa ubingwa huo mara ya pili katika msimu wa mwaka 2007 na 2008. Klabu ya Sepahan ndiyo imetwaa Ligi Kuu ya Soka ya Iran inayofahamika pia kama Persian Gulf Pro League mara nyingi zaidi, ikizingatiwa kuwa imetwaa taji hilo mara tano; katika misimu ya mwaka 2002-03, 2009-10, 2010-11, 2011-12 and 2014-15.
Fainali ya Cecafa U17, Tanzania bingwa baada ya kuicharaza Somalia
Timu ya taifa ya soka ya Tanzania ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 17 imetwaa taji la Soka katika Nchi za Afrika Mashariki na Kati Cecafa, baada ya kuibamiza timu chovu ya Somalia nchini Burundi. Katika mchuano huo wa Jumapili ulioshuhudiwa kwa karibu pia na Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika, CAF Ahmad Ahmad, Timu ya Taifa ya vijana waliochini ya miaka 17, Serengeti Boys imetwaa ubingwa wa CECAFA baada ya kuichapa Somalia kwa mabao 2-0 katika fainali iliyofanyika Jumapili Aprili 29, 2018 mjini Bujumbura nchini Burundi. Magoli ya Serengeti Boys yamefungwa na Edson Jeremiah na Jaffary Mtoo.
Kufuatia ubingwa huo, Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Milambo amesema ishara nzuri kwa timu ya taifa ya baadaye kwani itakuwa na vijana wazuri zaidi.
Serengeti Boys imetinga fainali baada ya kuifunga Kenya mabao 2-1 kwenye hatua ya nusu fainali huku Somalia wakiitwanga Uganda bao 1-0. Uganda imechukua nafasi ya mshindi wa tatu baada ya kuifunga Kenya magoli 4-1 mchezo uliochezwa mapema kabla ya fainali. Katika hatua nyingine katibu Mkuu wa Cecafa Nicholaus Musonye amesema baada ya kukamilika kwa michuano hiyo, Cecafa itahamishia nguvu kuandaa michuano ya Cecafa kwa wanawake itakayofanyika mwezi ujao nchini Rwanda. Hata hivyo michuano ya Cecafa kwa vijana chini ya miaka 17 ilikumbwa na changamoto ambapo timu ya Taifa ya Vijana ya Zanzibar iliondolewa kwenye mashindano baada ya kubainika wachezaji wake kuzidi umri unaotakiwa.
Soka Tz Bara: Simba na Yanga zaumana tena
Mchuano wa watani wa jadi wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara uliokua ukisubiriwa kwa hamu na shauku kuu ulipigwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam, ambapo Simba alifanikiwa kumtafuna na kummeza mzima mzima hasimu wake Yanga. Simba wamefanikiwa kuondoka na point zote tatu baada ya kufanikiwa kupata ushindi wa goli 1-0, goli la Simba lilipatikana dakika ya 37 kupitia kwa Erasto Nyoni aliyetumia vyema pasi ya iliyochongwa kiustadi na Shiza Kichuya.
Yanga walicheza karibia kipindi chote cha pili wakiwa pungufu uwanjani baada ya beki wao wa kulia, Hassan Kessy kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 48 ya mchezo kwa kumchezea rafu beki wa simba, Asante Kwasi. Ushindi huo sasa unawafanya vijana wa Simba au ukipenda waite Wekundu wa Msimbazi ambao wamecheza michezo 26 ya Ligi na kusaliwa na michezo minne, ili iwe Bingwa bila ya kujali matokeo ya timu nyingine inahitaji point tano yaani ishinde mchezo mmoja na itoke sare mchezo mmoja, wakati Yanga wao kutetea Ubingwa wao kunategemeana na Simba apoteze mechi tatu huku yeye akipata matokeo chanya. Mpaka sasa, Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 62 baada ya mechi 26 wakati Yanga ikiwa nafasi ya pili ikimiliki pointi 48 kutokana na mechi zake 24. Simba wanahitaji pointi 5 tu katika mechi zake 4 zijazo ili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitano ya kusubili ubingwa huo tokea walipoutwaa mwaka 2012.
Takwimu za WADA kuhusu pufya
Katika eneo la Afrika Mashariki, Kenya iliongoza ikifuatwa na Tanzania (2), Ethiopia (2) na Rwanda (1), visa vyote katika riadha, na Uganda, ambayo ilikuwa na kisa kimoja cha mtunishaji misuli kutumia dawa hizo haramu. Mataifa ya Somalia, Burundi, Eritrea, Djibouti, Sudan Kusini na Sudan hayako kwenye orodha hii. Licha ya kuwa katika orodha ya mataifa yanayochunguzwa sana kwa wanaspoti wake kutumia dawa za kusisimua misuli, Kenya ilishuhudia visa vichache vya uovu huu mwaka 2016, huku Italia, Ufaransa, Marekani, Australia, Ubelgiji na Urusi zikishikilia nafasi sita za kwanza, mtawalia. Katika ripoti ya Shirika la Kukabiliana na Matumizi ya Pufya duniani (WADA) ya mwaka 2016 iliyotolewa Aprili 26, 2018, Kenya ni ya 35 duniani kwa visa tisa. Kenya, ambayo ilishuhudia karibu visa 50 kati ya mwaka 2012 na 2016, iliingia kwenye orodha ya mataifa yanayotenda uovu huu sana Mei 12 mwaka 2016 na bado haijatolewa katika orodha hiyo ya WADA. Wanariadha wake saba walivunja sheria hizi mwaka 2016. Kenya ilikuwa na kisa kimoja katika utunishaji misuli na kingine katika riadha za walemavu. Wanaspoti kutoka Italia waliongoza kutumia njia hii ya mkato michezoni.
Waitaliano 147 walivunja sheria hizi katika kipindi hicho. Ufaransa inashikilia nafasi ya pili kwa visa 86. Inafuatwa na Marekani (visa 76), Australia (75), Ubelgiji (73), Urusi na India (69 kila mmoja), Iran na Brazil (55 kila mmoja) nayo Afrika Kusini inafunga 10-bora kwa visa 50. Uingereza, Misri na Ujerumani zilishuhudia visa 27, 26 na 21, mtawalia. Katika eneo la Afrika Mashariki, Kenya iliongoza ikifuatwa na Tanzania (2), Ethiopia (2) na Rwanda (1), visa vyote katika riadha, na Uganda, ambayo ilikuwa na kisa kimoja cha mtunishaji misuli kutumia dawa hizo haramu. Mataifa ya Somalia, Burundi, Eritrea, Djibouti, Sudan Kusini na Sudan hayako kwenye orodha hii. Kenya ni mojawapo wa mataifa yanayofanya vibaya katika riadha. Katika fani hii, Urusi ililishuhudia visa vingi (30) ikifuatwa na India (21), Morocco (14), Marekani (11), Saudi Arabia, Romania na Ufaransa (tisa), Italia (nane), Kenya (saba) na Uhispania na Brazil (sita). Orodha ya visa vya kututumua misuli michezoni inaonyesha kwamba riadha ilishuhudia visa vingi kuliko fani zingine. Ilikuwa na visa 205 ikifuatiwa kwa karibu na utunishaji misuli (183), uendeshaji baiskeli (165) na unyanyuaji uzani (116). Soka imeruka juu hadi nafasi ya tano kwa visa 79, ingawa idadi ya visa ilipungua kutoka 108 vilivyoshuhudiwa mwaka 2015. Kwa jumla, WADA ilipata visa 1,595 vya matumizi ya pufya katika michezo 112 mwaka 2016, kutoka visa 1,929 mwaka 2015.
Kombe la Dunia 2022; Uhasama wa Saudia dhidi ya Qatar
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Qatar amefichua kwamba, nchi nne zinazoizingira nchi hiyo zikiongozwa na Saudi Arabia, zimetoa sharti zito kwa Doha kwamba, inatakiwa kuchagua moja ya mambo mawili, ima kuachana na maandalizi ya michuano ya kombe la dunia 2022, au kuendelea kuzingirwa na nchi hizo. Ali Ibn Fatiz al-Marri ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la Uhispania la ABC na kuongeza kuwa, polisi ya Imarati, imetangaza kwamba ikiwa serikali ya Qatar inataka kumalizika mzingiro wa nchi nne za Kiarabu dhidi yake, basi inatakiwa kuachana na maandalizi ya kombe hilo la dunia. Hii si mara ya kwanza kwa Umoja wa Falme za Kiarabu kuitaka Qatar iache kuandaa mashindano ya fainali za kombe la dunia za mpira wa miguu mwaka 2022 kama sharti la kuondolewa mzingiro wa nchi nne za Kiarabu dhidi yake.
Mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana pia, Dhahi Khalfan afisa wa ngazi za juu wa usalama katika Umoja wa Falme za Kiarabu Imarati alinukuliwa kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter akisema kuwa, mgogoro uliopo kati ya Doha na nchi kadhaa za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia utapatiwa ufumbuzi iwapo tu Qatar itaachana na azma yake ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 2022. Nchi hizo nne za Kiarabu zinazoizingira Qatar huko nyuma pia zilikuwa zimetoa masharti 13 ya kuitaka Doha iyatekeleze bila kuhoji vinginevyo itaendelea kuzingirwa. Kwa mujibu wa Khalfan, iwapo Kombe la Dunia 2022 halitaandaliwa na Qatar, basi mgogoro wa Qatar utaisha. Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri tarehe Tano Juni mwaka jana 2017, zilitangaza kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar zikiituhumu Doha kuwa inaunga mkono ugaidi na kwamba haiendi sambamba na malengo ya nchi hizo. Baada ya kukata uhusiano huo wa kidiplomasia, nchi nne hizo za Kiarabu baadaye ziliiwekea Qatar mzingiro wa kiuchumi na kuipa masharti chungu nzima.
…………………………TAMATI……………….