Jun 01, 2018 00:58 UTC
  • Ijumaa, Juni Mosi, 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 16 Ramadhani mwaka 1439 Hijria, inayosadifiana na Juni Mosi mwaka 2018 Miladia.

Miaka 712 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 16 Ramadhani mwaka 727 Hijria Qamaria, aliaga dunia Ibn Zamlakani, faqihi na msomi wa Hadithi na Fasihi wa Kiislamu, aliyefahamika kama Dimishqi. Msomi huyo alipata kustafidi na hazina ya elimu ya dini na hadithi kutoka kwa maulamaa wa zama hizo. Kutokana na kipaji chake cha elimu, msomi huyo aliruhusiwa kutoa fatua kwa kipindi cha miaka 20, mbali na kufunza masomo mbalimbali ya kidini katika vyuo tofauti, na kuwa kadhi mjini Damascus nchini Syria. Miongoni mwa kazi za msomi huyo ambazo tunaweza kuashiria hapa ni kitabu alichokipa jina "Al Buranul Kaashif An I'ijazil Qurani".

Ibn Zamlakani,

##############

Miaka 32 iliyopita, yaani tarehe Mosi Juni mwaka 1986 Miladia, wanafunzi kadhaa wa shule za msingi waliwaandikia barua wenzao duniani kote na kuwataka kupitisha muda wao wa siku nzima kwa ajili ya amani. Sehemu moja ya barua ya wanafunzi hao inasomeka kama ifuatavyo: "Wazazi wetu wana imani thabiti na kutupenda, kwa kuwa sisi ni watoto wao. Hata hivyo je, mnafahamu ni dunia ya aina gani waliyotuandalia? Sisi kamwe tusingekuwa na fursa ya kukua, iwapo wazazi wetu wangefanya kosa japo dogo tu. Tunahitaji suhula kwa ajili ya kukua na malezi." Kwa mnasaba huo, siku ya kwanza ya mwezi Juni kila mwaka, imepewa jina la "Siku ya Watoto Duniani". Kwa ajili hiyo marasimu maalumu hufanyika katika pembe mbalimbali za dunia katika kuadhimisha siku hiyo.

Siku ya Mtoto Duniani

 

##############

Miaka 95 iliyopita muwafaka na siku kama ya leo, moja kati ya zilzala kubwa zilizouwa watu wengi duniani, iliikumba Tokyo mji mkuu wa Japan. Zilzala hiyo ilitokea nyakati mbili tofauti kwa kupishana muda mfupi. Mtetemeko huo wa ardhi uliharibu nusu ya mji wa Tokyo na kuuwa watu zaidi ya laki moja na elfu hamsini mjini humo.

Zilzala

 

#############

Na siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, aliaga dunia John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alizaliwa 20 Oktoba mwaka 1859 na alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na aliweza kujifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri alivyoviandika katika kipindi cha uhai wake ni pamoja na "How we think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture." John Dewey alifariki dunia mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 93.

John Dewey

 

Tags