Ijumaa, Juni 8, 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 18 Khordad mwaka 1397 Hijria Shamsia sawa na 23 Ramadhani mwaka 1439 Hijria, zinazosadifiana na 8 Juni mwaka 2018 Miladia.
Miaka 501 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, Vasco Núñez de Balboa mwanabaharia Mhispania aliyevumbua Bahari ya Pasifiki alinyongwa. Alizaliwa tarehe 4 Novemba mwaka 1475 Miladia katika kijiji kimoja kilichoko kusini mwa Uhispania. Wazazi wake hawakuwa na uwezo mkubwa na hivyo akiwa na umri wa miaka 16, Vasco Núñez alilazimika kufanya kazi kama muhudumu katika kasri ya mmoja wa watawala kwa muda wa miaka minane hadi alipofika katika cheo cha kanali. Baada ya hapo alianza kufunga safari kuenda maeneo mbali mbali kutafuta dhahabu. Mnamo 29 Septemba mwaka 1513 alifika Panama ya leo na kujitangaza mtawala wa eneo hilo. Baada ya kupata ngawira na mafanikio makubwa, alirejea Uhispania ambapo uhusiano wake na mfalme haukuwa mzuri. Hatimaye kwa tuhuma kuwa alikuwa amemsaliti na kumfanyia mfalme hiana, alihukumiwa kunyongwa mnamo Juni 8 mwaka 1517 akiwa na umri wa miaka 42.
@@@@
Siku kama ya leo miaka 185 iliyopita sawa na tarehe 23 Mwezi wa Ramadahni mwaka 1254 Hijria Qamaria, ilikamilika kazi ya uandishi wa kitabu cha ‘Jawaahirul-Kalaam’ ambacho kimejumuisha masuala muhimu ya sheria za Mwenyezi Mungu juu ya halali na haramu na kadhalika sheria mbalimbali za dini ya Kiislamu. Ni vyema kuashiria kuwa, kitabu cha Jawaahirul-Kalaam kimebainisha kwa undani masuala mengi ya sheria kiasi kwamba hadi sasa hakuna msomi aliyeweza kuandika kitabu kama hicho. Kunukuu kauli za wasomi wakubwa wa sheria za Kiislamu na kuzitolea ushahidi kwa umakini wa hali ya juu, ni kati ya nukta zinazopatikana katika kitabu hicho. Ayatullah Muhammad Hassan Najafi, mtunzi wa kitabu hicho, alianza kazi ya uandishi wa kitabu cha Jawaahirul-Kalaam akiwa na umri wa miaka 25 huku akitumia karibu muda wa miaka 30 katika uandishi wake na kutokea kuitwa kwa lakabu ya ‘Sheikhul-Fuqahaa.’ Katika kipindi cha maisha yake kulitawala hujuma za fikra potofu za genge la Uwahabi na watu wa kundi la Ikhbariyyun suala ambalo lilimfanya Ayatullah Muhammad Hassan Najafi kuelezea umuhimu wa kuwa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu. Ni baada ya hapo ndipo kukazaliwa fikra ya kuwepo waliyyu Faqihi ‘walii kiongozi' anayesimamia masuala ya sheria za Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel, Mossad, lilifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya kiongozi mwingine wa Kipalestina katika moja ya nchi za kigeni. Siku hiyo maajenti wa Mossad walimuuwa Atef Bseiso mmoja wa viongozi wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Paris, Ufaransa. Licha ya kwamba hakukuwepo shaka juu ya kuhusika utawala wa Kizayuni katika mauaji hayo, lakini utawala huo ghasibu ulikana kufanya jinai hiyo ya kinyama kwa kuhofia hasira za walimwengu. Hata hivyo miaka saba baadaye, polisi ya Ufaransa ilitangaza kwamba shirika hilo la ujasusi la Israel Mossad ndilo lililopanga na kutekeleza mauaji hayo.
@@@@
Tarehe 8 Juni miaka 123 iliyopita, alizaliwa Said Nafisi, mwandishi na mtarjumi wa kisasa wa nchini Iran hapa mjini Tehran. Nafisi alikuwa mtoto wa Ali Akbar Nafisi, maarufu kwa jina la Nadhim al-Atwibba, msomi na mwandishi wa kitabu cha ‘Tamaduni ya Thamani’. Baada ya kumaliza masomo yake ya awali, Ustadh Said Nafisi alikamilisha masomo yake katika taaluma za sheria na elimu ya siasa. Nafisi alijishughulisha na ukufunzi katika taaluma za historia na fasihi huku akiwa mmoja wa wanaharakati wa utamaduni nchini Iran. Mbali na Iran, Ustadh Said Nafisi alikuwa na uanachama katika taasisi mbalimbali za kiutamaduni na katika vyuo vikuu vya nchi kadhaa za Ulaya na Asia.
@@@
Na Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita yaani tarehe 23 Ramadhani mwaka 1392 Hijria Qamaria, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai mwanafalsafa, arifu na faqihi mkubwa wa Kiirani alikamilisha kazi ya uandishi wa tafsiri kubwa na ya aina yake ya Qur’ani ya al Mizan. Tafsiri hiyo ya Qur’ani ni moja kati ya tafsiri kubwa na makini zaidi za Qur’ani Tukufu na iliandikwa katika kipindi cha karibu miaka 20. Sifa kubwa zaidi ya tafsiri hiyo ni kwamba imefasiri aya za Qur’ani kwa msaada wa aya nyingine za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Tafsiri hiyo kubwa na adhimu iliandikwa na Allamah Tabatabai kwa lugha ya Kiarabu na hadi sasa imetarjumiwa kwa lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiingereza na Kihispania.