Ijumaa 18 Julai, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe 22 Muharram 1447 Hijria sawa na Julai 18 mwaka 2025.
Katika siku kama ya leo miaka 1154 iliyopita, kilianza kipindi cha vita vya miaka 25 kati ya Uingereza na Denmark katika karne ya 9.
Alfred The Great, mfalme kijana wa Uingereza alikuwa kamanda mashuhuri wakati wa kujiri vita hivyo katika kipindi hicho. Wadenmark katika siku hiyo waliivamia Uingereza na kuiteka ardhi kubwa ya nchi hiyo.
Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka 25 hatimaye vilifikia tamati kwa Waingereza kupata ushindi mnamo tarehe 9 Januari mwaka 896.

Siku kama ya leo miaka 987 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi, ambaye ni mashuhuri kwa jina la Sheikhul Twaaifa.
Sheikh Tusi alizaliwa katika mji wa Tus kaskazini mwa Iran na akaelekea Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu ya juu baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa Iraq na miaka kadhaa baadaye akaweka msingi wa chuo kikuu cha kidini cha Najaf. Kituo hicho cha kidini kina historia ya miaka elfu moja na ni moja ya vituo muhimu mno vya elimu ya Kiislamu.
Sheikh Tusi ameandika vitabu vingi sana katika taaluma mbalimbali. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani tukufu ya al Tibyan na vitabu vya Hadithi na fiqhi vya al Istibsar na al Tahdhiib.

Miaka 244 iliyopita katika siku kama ya leo William Herschel, mtaalamu maarufu wa nujumu wa Uingereza alifanikiwa kugundua hakika ya kundi la nyota na sayari ikiwemo hii yetu ya dunia.
Alitumia darubini kubwa aliyokuwa ametengeneza kwa ajili ya kutazama nyota na kuthibitisha kwamba, kundi la nyota na sayari linaundwa na nyota nyingi ikiwemo sayari ya dunia ambayo ni sehemu ndogo sana ya kundi hilo.
Herschel pia ndiye mvumbuzi wa sayari ya Uranus. Alifariki dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 84.

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, Zuheir Muhsein, Katibu Mkuu wa wakati huo wa Harakati ya al Sa'iqa tawi la Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO) aliuawa kigaidi na maajenti wa mashirika ya ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel (Mossad) na lile la Misri huko katika mji wa Cannes nchini Ufaransa. Maajenti wa tawala hizo mbili walikimbia na kutoweka baada ya kufanya mauaji hayo. Zuheir Muhsin alikuwa mpinzani mkubwa wa mapatano ya kisaliti ya Camp David na aliwahi kutishia mara kadhaa kwamba harakati yake ya al Sa'iqa itamuua mtawala wa wakati huo wa Misri, Anwar Sadaat aliyetia saini makubaliano hayo na wazayuni.

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Azimio hilo lilizitaka nchi mbili za Iran na Iraq kusitisha vita na kufanya suluhu. Jamhuri ya Kiislamu ilikubali azimio hilo kutokana na baadhi ya vipengele vyake hususan kile kinachohusiana na kuitambulisha Iraq kuwa ndiye mchokozi katika vita hivyo na kuitaka iilipe Iran fidia ya hasara za vita hivyo.
Hata hivyo utawala wa Saddam Hussein ambao pia ulikubali azimio hilo la Baraza la Usalama, uliendeleza mashambulizi dhidi ya ardhi ya Iran.

Na tarehe 18 Julai, ni "Siku ya Kimataifa ya Mandela".
Mwaka wa 2009, Umoja wa Mataifa ulitangaza siku hii kuwa siku mahsusi kwa Nelson Mandela, mwasisi wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Umoja wa Mataifa uliitangaza siku ya kuzaliwa Mzee Nelson Mandela, yaani tarehe 18 Julai kuwa Siku ya Kimataifa ili kuenzi mchango wake mkubwa katika harakati ya kupigania uhuru nchini Afrika Kusini na juhudi zake kubwa za kutangaza amani, kutilia maanani utatuzi wa migogoro baina ya kaumu na nchi mbalimbali, kutetea haki za binadamu, na kuwepo usawa na maelewano baina ya wanadamu wa mbari na kaumu zote. Mandela alifariki dunia tarehe 5 Disemba mwaka 2013.
