Jul 17, 2025 04:21 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 17 Julai, mwaka 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria, sawa na tarehe 17 Julai mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 721 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Muharram 726 Hijria, alifariki dunia faqihi na msomi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu, Hassan bin Yussuf bin Mutahhari Hilli, maarufu kwa jina la Allamah Hilli.

Allamah Hilli alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa kama Khaja Nasiruddin Tusi na anatajwa kama miongoni mwa wasomi wa kipekee wa zama zake. Aliandika zaidi ya vitabu mia moja katika taaluma mbalimbali za Kiislamu.

Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni Tadhkiratul Fuqahaa' ambacho kinaelezea mitazamo mbalimbali za madhehebu ya Kiislamu, tafsiri ya Qur'ani Tukufu ya 'Nahjul Imaan' na 'Muntaha al Matwalib'.   

Siku kama ya leo miaka 235 iliyopita, alifariki dunia Adam Smith, mwanafalsafa na mtaalamu wa uchumi wa Scotland.

Smith alizaliwa mwaka 1723 Miladia huko Scotland na baada ya kuhitimu masomo ya sekondari akajiunga na Chuo Kikuu cha Glasgow na kisha cha Oxford ambapo baadaye alichaguliwa kuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Glasgow.

Sanjari na kufundisha falsafa chuoni hapo, Adam Smith alijishughulisha na utafiti katika masuala ya uchumi na kufanikiwa kuandika kitabu cha 'Utafiti juu ya Asili na Chanzo cha Utajiri.' Ni kwa ajili hiyo ndio maana akaitwa jina la baba wa elimu ya uchumi wa sasa.

Adam Smith

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita Profesa Roger Garaudy, mwanafalsafa na mwanafikra wa Ufaransa alizaliwa huko katika mji wa Marseille.

Garaudy alipata shahada ya udaktari katika taaluma tatu za masomo ya falsafa, fasihi na utamaduni. Roger Garaudy alifungwa jela katika kambi ya mateka wa kivita wa Ujerumani tangu mwaka 1940 hadi 1943 kutokana na mapambano yake dhidi ya ufashisti wa Adolph Hitler wakati Ufaransa ilipokaliwa kwa mabavu na Ujerumani.

Profesa Garaudy alikuwa mwanachama wa chama cha Kikomonisti cha Ufaransa kwa miaka 36 na pia mwanachama wa kamati kuu ya chama hicho kwa miaka 25. Hata hivyo mitazamo ya kikomunisti na kiliberali haikuweza kukata kiu ya kutafuta ukweli ya msomi huyo wa Ufaransa na hatimaye alikubali dini ya tukufu ya Uislamu baada ya kufanya utafiti mkubwa. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979 ulikuwa na taathira kubwa katika mitazamo ya Profesa Roger Garaudy.   

Profesa Roger Garaudy

Katika siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, chama cha Baath cha Iraq kilichukua hatamu za uongozi kupitia mapinduzi yaliyoongozwa na Ahmad Hassan al-Bakr na kumpindua Rais Abdulrahman Aarif.

Baada ya kuchukua madaraka chama cha Baath, Saddam Hussein ambaye alikuwa kiongozi nambari mbili wa chama hicho alianza kuwauwa wapinzani wake nchini Iraq na vikosi vya usalama na vya jeshi la nchi hiyo pia vikaanzisha hujuma kali dhidi ya wapinzani wa Kikurdi, wazalendo, wanaharakati wa Kiislamu na hata Wakomonisti. 

Ahmad Hassan Bakr