Jun 30, 2018 08:07 UTC
  • Aya na Hadithi (24)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambapo kwa leo tutajadili Aya ya Nur ambayo inahesabiwa na wasomi na wajuzi wa Qur'ani kuwa bawa la pili la muumini ambaye anamiliki bawa la kwanza la Aya ya Kursiy.

Kwa mabawa haya mawili muumini hupata uwezo wa kupaa katika mbingu za Tauhidi halisi na mwongozo safi wa Mola Muumba wa mbingu na ardhi. Katika kipindi cha leo tutasoma na kunufaika na nuru ya Aya hii tukufu nayo kimsingi ni Aya ya 35 ya Surat an-Nur. Pamoja na hayo, ni wazi kuwa madhumuni ya Aya hii yanakamilishwa na Aya tatu zinazofuatia kama ambavyo madhumuni ya Aya ya Kursiy yanakamilishwa na Aya mbili zinazofuata Aya hiyo. Hivyo basi hebu na tusikilize kwa makini Aya za 35 hadi 38 za Suratu an-Nur ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota inayomeremeta, inayowashwa kwa mafuta yanayotokana na mti uliobarikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa yenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humuongoza kwenye Nuru Yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu. Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kuisimamisha Swala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka. Ili Mwenyezi Mungu awalipe mazuri ya yale waliyoyatenda, na awazidishie katika fadhila Zake. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.

Ayatul Kursy

 

Wapenzi wasikilizaji, ni wazi kuwa kupitia nuru, mwanadamu huwa na uwezo wa kuona vizuri vitu ambavyo huweza kuvitumia kutambua hakika ya muelekeo anaopasa kuufuata. Yaani jambo hilo humpa uwezo wa kujua njia nyoofu na sifa zake na mambo anayopasa kuyatekeleza katika ibada ili aweze kubakia kwenye njia hiyo nyoofu. Hivyo, nuru ni chanzo cha mwongozo ambao ni Mwenyezi Mungu Mtukufu, na huu ndio mfano bora zaidi wa nuru.

Sheikh Swadouq (MA) ananukuu katika kitabu chake cha Tauhid, Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa al-Abbas bin Hilal ambaye anasema: 'Nilimuuliza (Imam) Ridha (as) kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema, Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi, naye akasema: Ni mwongozaji wa watu wa mbinguni na ardhini. Na katika riwaya iliyopokelewa na al-Barqi katika kitabu cha al-Mahasin alisema: Ni wokovu wa watu walioko mbinguni na ardhini.'

**********

Tunapozingatia kwa makini Aya Tukufu tulizosoma tunaona kwamba zinatupigia mifano ambayo inabainisha wazi wokovu na mwongozo huo wa Mwenyezi Mungu na nyumba zilizo na mwanga wake Mwenyezi Mungu, ambao huwaangazia waumini njia sahihi na halisi ya kumuabudu Mungu Muumba. Sheikh al-Huweizi (MA) anasema katika Tafsiri yake ya Nuru ath-Thiqlain: 'Imepokelewa kutoka kwa as-Swadiq (as) – kama ilivyonukuliwa katika kitabu cha at-Tauhid – kwamba aliulizwa kuhusu kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema, Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka lenye kuwekwa ndani yake taa, akasema: Ni mfano ambao Mwenyezi Mungu ametupigia. Nabii na Maimamu (as) ni miongoni mwa dalili na Aya za Mwenyezi Mungu ambazo waja huongozwa kwazo kuelekea Tauhidi, maslahi ya dini, sheria za Kiislamu, suna na faridha….na nguvu zote zinatokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu.'

 

Na mifano ya mithali hii ya Qur'ani imebainishwa na Hadithi nyingi mojawapo ikiwa ni hii iliyonukuliwa katika kitabu cha Tauhidi na vitabu vingine kupitia al-Fudheil bin Yasar anayesema: 'Nilimwambia Abi Abdallah as-Swadiq (as):  Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi, akasema: Ni Mwenyezi Mungu Mtukufu. Nikasema: Mfano wa Nuru yake, akasema: Ni Muhammad (saw)…. Nikasema: Ni kama shubaka, akasema: Ni kifua cha Muhammad (saw)…Nikasema: Lenye kuwekwa ndani yake taa, akasema: Ndani yake mna nuru ya elimu, yaani Utume….Nikasema: Taa ile imo katika tungi, akasema: Elimu ya Mtume (saw) kwenda kwenye moyo wa Ali (as). Nikasema: Tungi lile ni kama nyota inayomeremeta, inayowashwa kwa mafuta yanayotokana na mti uliobarikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi, akasema: Huyo ni Amir al-Mu'mineen, Ali bin Abi Talib (as), sio Myahudi wala Mnasara. Nikasema: Yanakaribia mafuta yake kung'aa yenyewe ingawa moto haujayagusa, akasema: Elimu inakaribia kutoka kwenye mdomo wa Alim (mjuzi) kutoka katika kizazi cha Muhammad kabla ya alim huyo kuitamka elimu yenyewe….. Nikasema: Nuru juu ya Nuru…, akasema: Imam anayepata msaada wa nuru ya elimu na hekima kutoka kwa Imam aliyemtangulia.'

Ndugu wasikilizaji, tunapoirejea Aya ya an-Nur na Aya nyingine zinazofungamana na Aya hiyo tunaona kwamba zinaashiria mjumuiko wa nuru ya Mwenyezi Mungu ambayo inapatikana katika nyumba zilizotakaswa na Mungu mwenyewe, na pia kuamuru nyumba hizo zitukuzwe na kuinuliwa kwa sababu watu wanaoishi kwenye nyumba hizo wamefikia kilele cha ukamilifu kutokana na nuru ya Mwenyezi Mungu, na hivyo kuwa minara ya wongofu ambayo huwanufaisha wale wanaotafuta na kutekeleza ibada sahihi na ya haki ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

 

Hivyo natija tunayoifikia kutokana na Aya na Hadithi tulizozijadili kwenye kipindi hiki ni kwamba kutafuta mwongozo wa Mwenyezi Mungu kunapasa kutimia kupitia minara maasumu na isiyotenda dhambi ambayo haiwashirikishi watu wengine wasiokuwa Muhammad (saw) na kizazi chake kitukufu (as). Kwa hakika hao ndio mzaituni uliojaa baraka na usiokuwa wa mashariki wala magharibi. Kwa maelezo hayo, wao ndio wanaoangaza kwa mwanga wa hidaya ya Mwenyezi Mungu kwa sababu uwepo wao wote umejaa mwanga.

Na kwa natija hii ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha juma hili cha Aya na Hadithi ambacho mmekisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapopata fursa ya kukutana nanyi tena wapenzi wasikilizaji, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags