Hadithi ya Uongofu (116)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongo. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia makundi ya watu ambao inaruhusiwa kuwasengenya.
Tulinukuu hadithi kutoka kwa Bwana Mtume SAW ambaye amenukuliwa akisema: Hakuna tatizo kusengenya watu wa aina tatu; Mosi, mtawala dhalimu, pili, fasiki (mtu mwenye mwenendo mbaya wa kimaadili) ambaye anafanya dhambi shahir shahir na tatu mtu mwenye kuanzisha bidaa na uzushi (katika dini). Tulieleza kwamba, madhulumu au mtu aliyedhulumiwa ana haki ya kueleza kuhusiana na kile alichodhulumiwa tu. Na endapo atamsengenya dhalimu na kutaja aibu na mapungufu mengine ambayo hayana uhusiano wowote na dhulma aliyotendewa, basi atakuwa amesengenya na kutenda dhambi jambo ambalo ni haramu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 116 ya mfululizo huu kitazungumzia maudhui ya tuhuma au kuwatuhumu watu ambayo nayo ni katika tabia mbaya za kimaadili. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Wapenzi wasikilizaji kwanza kabisa kuna haja ya kuelezea maana ya maneno mawili. Neno la kwanza ni kusengenya na maana yake ni mtu kusema mambo na sifa au tabia ya mtu au aibu ya mtu fulani kwa watu wengine. Kufanya hivi huhesabiwa kuwa ni kusengenya. Neno la pili ni tuhuma na hili lina maana ya mtu kutaja sifa na mambo fulani ya mtu ambayo hanayo. Kwa mfano kusema kwamba, fulani ni muongo, mwizi na mzushi, huku katika uhalisia wa mambo mtu mtajwa hana sifa hizo. Kufanya hivi kunahesabiwa kuwa ni kutuhumu.
Imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume SAW kwamba, siku moja aliwaambia masahaba zake: “Je nikupeni habari ni watu gani wabaya kabisa miongoni mwa watu? Masahaba zake wakasema, ndio ewe Mtume wa Allah. Mbora huyo wa viumbe akasema: Watu wabaya kabisa ni wale ambao wanazuia kheri yao kwa watu wengine na kila walichonacho wanakitaka kwa ajili yao tu.” Masahaba waliokuweko wakadhani kwamba, kwa maneno haya ya Mtume SAW hakuna tena kundi la watu wabaya kama hilo alilolitaja. Hata hivyo, Mtume SAW akaendelea kusema, je nikujulisheni kundi gani la watu ambalo ni baya zaidi ya hili? Kisha akataja kundi jingine. Masahaba wakasema, tulidhani kwamba, hakuna kundi jingine baya kuliko ulilolitaja mwanzo. Hata hivyo Mtume SAW akaongeza kwa kusema, je mnataka nikutajieni kundi ambalo ni baya zaidi? Masahaba wakauliza kwa mshangao mkubwa, kwani kuna kundi jingine baya zaidi ya hili? Hapo Bwana Mtume SAW akalitaja kundi la tatu kwa kusema: Kundi baya zaidi miongo mwa watu ni wale wenye ndimi chafu, wenye kutoa matusi, kuwatuhumu wengine na kuharibu heshima za watu.
Wapenzi wasikilizaji kwa mujibu wa hadithi hiyo ya Bwana Mtume saw ni kuwa, kutuhumu ni katika tabia mbaya za kimaadili na ambazo zimekemewa mno katika mafundisho ya Uislamu.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 112 ya Surat Nisaa kwamba:
Na atendaye kosa au dhambi kisha akamsingizia asiye na kosa, basi amejitwika dhulma na dhambi iliyo wazi.
Kuna wakati kukwea kijamii, kiuchumi au kisiasa na kupata maendeleo kwa mtu huwa ni jambo ambalo haliwapendezi baadhi ya watu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana watu hao kutokana na kushindwa kustahamili maendeleo ya mtu huyo huona kwamba, mwenzao amefikia hapo kwa kutumia njia za ujanja ujanja na wizi na hivyo kumsukumia kila aina ya tuhuma, ilihali mhusika hana ushahidi wowote wa kuthibitisha maneno yake. Bali ni uongo anaoutunga lengo likiwa ni kutilia shaka maendeleo ya mwenzake. Kitendo hiki katika Uislamu kinajulikana kwa jina la "tuhuma". Kwa mtazamo wa Uislamu kumtuhumu mtu ni katika madhambi makubwa.
Imam Ja'afar bin Muhammad al-Swadiq AS anasema: Wakati muumini anapomtuhumu nduguye muumini, imani yake hufutika moyoni mwake kama chumvi inavyoyeyuka katika maji; na wakati imani ya muumini inapofutika na kutobakia athari yoyote ya imani katika moyo wake, mafikio yake huwa motoni.
Wapenzi wasikilizaji, sababu ya kwamba, tuhuma huifanya imani ya mwenye kutuhumu kuondoka ni kwamba, imani inaambatana na ukweli na uaminifu ilihali tuhuma ni kuwavurumishia uongo watu wengine. Hivyo basi mtu anapokuwa na ada na mazoea ya kuwasingizia na kuwabambikizia uongo watu wengine, hawezi tena kuwa ni mtu wa kutafuta ukweli na uhakika na kwa utaratibu huo imani ya mwenye kutuhumu huondoka hatua kwa hatua na kwa muktadha huo kutobakia athari yoyote ile ya imani katika moyo wake, hatua ambayo huifanya hatima yake isiwe ghairi ya kuingizwa katika moto wa jahanamu.
Kwa hakika tuhuma au kutuhumu ni aina mbaya kabisa ya uongo. Hii ni kutokana na kuwa, kitendo hiki kina mabaya ya uongo, kina madhara ya kusengenya na wakati huo huo ni aina mbaya kabisa ya dhulma kwa wengine. Kwa maana kwamba, mtu anapomtuhumu mtu kwa mfano ameiba au ametenda kitu fulani hali ya kuwa hajafanya hivyo, anakuwa amemtendea dhulma yule aliyemtuhumu kwa jambo hilo.
Kwa upande mmoja dini tukufu ya Kiislamu imeharamisha kutoa tuhuma na kuwatuhumu watu na kuwataka waumini wajiweke na kujitenga mbali na tabia hiyo mbaya ya kimaadili na wasimnasibishe mtu na aibu fulani bila ya hoja na ushahidi; na katika upande wa pili Uislamu umewataka waumini wasijiweke katika mazingira ya kutuhumiwa na hivyo kutoandaa mazingira ya watu wengine kutenda dhambi.
Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa: Mtu ambaye amejiweka katika mazingira ya kutuhumiwa hapaswi kumlaumu mtu ambaye atamdhania vibaya."
Hivyo basi, moja ya njia bora kabisa za kuepukana na tuhuma ni mtu kuwa makini katika matendo na nyendo zake na hivyo kutowapatia kisingizio wale wenye nyoyo chafu na maradhi ya kutuhumu watu wengine. Kufanya hivyo kutamnyima fursa hata yule ambaye amekusudia kumtuhumu kwa kukusudia kwani atakosa jambo lolote au mwendo wowote kutoka kwako wenye kutia shaka kwa ajili ya yeye kuthibitisha kwamba, tuhuma zake kwako zina ishara na dalili kadha wa kadha.
Kuhusiana na hilo Imam Ali AS anawausia waumini wasiende katika maeneo au kukaa katika vikao ambavyo vina kila dalili ya kutuhumiwa au ambavyo vinadhaniwa kufanyika mambo mabaya.
Wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, tukutane tena wiki ijayo siku na wakati kama wa leo.
Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.