Sep 06, 2018 03:01 UTC
  • Alkhamisi tarehe 6 Septemba 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 25 Dhulhija 1439 Hijria sawa na tarehe 6 Septemba 2018.

Tarehe 25 Dhulhija inasadifiana na siku ya kuteremshwa Suratu Dahr ambayo inawahusu Imam Ali bin Abi Twalib, mkewe Bibi Fatimatu Zahra na watoto wao Hassan na Hussein (as). Baada ya watukufu hao kuweka nadhiri ya kufunga swaumu siku tatu kwa ajili ya kukidhiwa haja zao na kuanza kutekeleza nadhiri hiyo, katika siku zote tatu za swaumu masikini, yatima na fakiri walikwenda nyumbani kwa Imam Ali (as) na kuomba chakula. Watukufu hao walitoa chakula chao kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya futari na kuwapa wahitaji hao kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Hali hiyo iliendelea kwa siku tatu za kutimiza nadhiri ya swaumu na wakati huo ndipo iliporetemshwa Suratu Dahr ikipongeza na kubakisha hai tukio hilo.

Siku kama ya leo miaka 252 iliyopita, alizaliwa John Dalton, msomi na mtaalamu wa fizikia wa Kingereza katika familia ya watu wa kijijini. Kutokana na Dalton kupendelea sana kusoma na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi, hatimaye alifanikiwa kwenda shuleni na kujifunza. Ni wakati huo ndipo alipoanza kufanya uchunguzi na utafiti katika masuala mbalimbali ya kielimu. Dalton alikuwa akiamini kuwa, mada ndogondogo sana zimeundwa na atomu ambayo nayo inatokana na mada hizo. Msomi huyo ambaye macho yake yalikuwa na hali ya upofu, hakuchoka na badala yake aliendeleza utafiti mkubwa katika uga huo. John Dalton alifariki dunia 1944.

John Dalton

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, jeshi la India lilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Pakistan kufuatia machafuko ya zaidi ya mwezi mmoja katika mipaka ya nchi mbili hizo. Hivyo vilikuwa vita vya pili vikubwa kuwahi kutokea kati ya nchi mbili hizo jirani kuhusiana na eneo la Kashmir. Vita hivyo vilidumu kwa takribani wiki tatu. Pakistan na India zilikubaliana kusimamisha mapigano kufuatia upatanishi wa Urusi ya zamani. Viongozi wa nchi mbili hizo hatimaye waliafikiana kuanza mazungumzo tarehe 10 mwezi Juni mwaka 1966 huko Tashkent mji mkuu wa Uzbekistan nchini ya upatanishi wa Waziri Mkuu wa Urusi ya zamani. Japokuwa azimio la Tashkent lilibainisha njia za kumaliza mgogoro wa eneo la Kashmir na namna ya kuboresha uhusiano kati ya New Delhi na Islamabad na pia kukaribishwa na nchi mbalimbali duniani, lakini lilishindwa kumaliza hitilafu kati ya India na Pakistan kuhusu umiliki wa eneo la Kashmir.

Vita vya pili vya Kashmir

Katika siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Swaziland ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na kila inapowadia siku kama ya leo husherekewa nchini humo kwa anwani ya siku ya taifa. Kuimarika ukoloni wa Ulaya huko kusini mwa Afrika kulisababisha pia Swaziland kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Ulaya. Hatimaye katika siku kama ya leo nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika ilipata uhuru. Swaziland ina ukubwa wa kilomita mraba 17364 na kijiografia iko kusini mwa bara la Afrika ikiwa inapakana na nchi za Msumbiji na Afrika Kusini.

Swaziland

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, baada ya kupamba moto harakati za mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah, kulifanyika maandamano makubwa katika maeneo mbalimbali kote nchini. Kwa sababu hiyo utawala wa Shah uliokuwa umepatwa na wasiwasi mkubwa kutokana na harakati hizo za mapinduzi, uliamua kupiga marufuku maandamano ya aina yoyote ile. Wakati huo huo huo Imam Ruhullah Khomeini MA aliyekuwa uhamishoni huko Najaf nchini Iraq alitoa taarifa akiwataka wananchi wa Iran kudumisha harakati za mapambano. Katika sehemu moja ya taarifa yake kwa wananchi, Imam Khomeini aliyataja maandamano yanayofanywa kwa ajili ya kufikia malengo ya Kiislamu kuwa ni ibada.

Maandamano dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah.

 

Tags