Sep 23, 2018 13:24 UTC
  • Jumapili, Septemba 23, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 13 Muharram 1440 Hijria, sawa na 23 Septemba 2018, Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita, yaani sawa na tarehe 13 Muharram mwaka wa 61 Hijria Abdullah bin Afif aliuawa shahidi na gavana wa Yazid bin Muawiya, Ubaidullah bin Ziad. Afif alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha malalamiko na upinzani wa wazi wazi dhidi ya jinai za Ubaidullah bin Ziad za kumuua shahidi mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as). Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kuwashambulia kwa maneno makali na kuwavunjia heshima mateka wa Karbala waliokuwa wamepelekwa katika majlisi yake, Abdullah bin Afif ambaye alikuwa miongoni mwa wacha-Mungu wakubwa wa mji wa Kufa huko Iraq na wafuasi wa kweli wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as), alikerwa mno na mwenendo huo wa gavana wa Yazidi wa kuwavunjia heshima Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na kumjibu mtawala huyo kwa hasira. Ubaidullah ambaye hakutarajia kuona majibu kama hayo baada ya kuua watu wa Nyumba ya Mtume (saw) alitoa amri ya kukamatwa Afif na kupelekwa kwake. Hata hivyo watu wa kabila lake walizuia kitendo hicho. Askari wa utawala wa Bani Umayyah walivamia nyumba ya Abdullah bin Afif usiku na kumtoa nje kisha wakamuua shahidi kwa kumkatakata kwa mapanga.

Abdullah bin Afif

Siku kama ya leo miaka 343 iliyopita, Valentin Conrart mwandishi na mwanafasihi wa Kifaransa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 72. Alizaliwa mwaka 1603 katika familia iliyokuwa na mapenzi makubwa na fasihi ya lugha na ni kwa msingi huo ndio maana alipokuwa katika rika la ujana, Conrart akawa amevutiwa sana na taaluma ya fasihi ya lugha na taratibu akaanza kujihusisha na fani ya uandishi.

Valentin Conrart

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, alifariki dunia Urbain Le Verrier mnajimu na mtaalamu wa nyota akiwa na miaka 66. Le Verrier alipenda sana masuala ya unajimu na elimu nyota ambapo hadi mwishoni mwa maisha yake, msomi huyo wa Kifaransa alifanya utafiti mkubwa na kutwalii kwa wingi katika uwanja huo. Mnajimu wa Kifaransa Urbain Le Verrier alifanikiwa kuvumbua sayari mpya kwa jina la Neptune kupitia moja ya tafiti zake. 

Urbain Le Verrier

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita sawa na tarehe Mosi Mehr 1281 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil-Udhmaa Sayyid Ruhullah al Musawi Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baba yake Imam Khomeini ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa Kiislamu aliuawa shahidi Imam akiwa bado mtoto na hivyo akalelewa na mama na shangazi yake. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi Ruhullah Khomeini alijiunga na masomo ya juu kwa walimu mashuhuri hususan Ayatullah Abdul Karim Hairi na Muhammad Ali Shahabadi. Imam Khomeini alianzisha harakati kubwa zaidi za kupambana na utawala wa kidhalimu wa Shah baada ya kufariki dunia Ayatullah Borujerdi. Upinzani na mapambano yake yalimfanya mtawala kibaraka, Shah ampeleke uhamishoni katika nchi za Uturuki, Iraq na Ufaransa. Imam aliendeleza mapambano yake dhidi ya Shah akiwa uhamishoni alikobakia kwa kipindi cha miaka 15 na baadaye alirejea nchini na kuuondoa madarakani utawala wa kifalme wa Shah na kuasisi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hapo mwaka 1979.

Imam Khomeini (MA)

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, nchi ya Saudi Arabia iliasisiwa, na Abdulaziz bin Saud akawa mfalme wa nchi hiyo. Nchi hiyo ina miji mitakatifu ya Makka na Madina na Mtume wa Uislamu Muhammad SAW alizaliwa katika mji wa Makka. Tangu mwanzoni mwa karne ya tatu Hijria, Saudi Arabia iliondoka chini ya himaya ya utawala wa Bani Abbas na hali ya mambo ya nchi hiyo haikuwa shwari kwa karne kadhaa. Serikali ya Othmania iliivamia Saudia katika karne ya 16 Miladia na kuanzia katikati mwa karne ya 17 ukoo wa Aal Saud ulianza kufanya juhudi za kuiongoza nchi hiyo na jitihada hizo ziliendelea hadi mwanzoni mwa karne ya 20.

Bendera ya Saudi Arabia

Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sigmund Freud daktari wa magonjwa ya akili raia wa Austria. Sigmund alizaliwa mwaka 1856. Daktari huyo alifanya utafiti na kuchunguza matatizo mbalimbali ya kiakili yanayomkumba mwanadamu na kutoa maoni na nadharia mpya kuhusu chanzo cha magonjwa ya akili. Kutokana na hilo, anahesabiwa kuwa mwasisi wa elimu ya uchunguzi wa kisaikolojia au Psychoanalysis.

Sigmund Freud