Oct 29, 2018 04:07 UTC
  • Jumatatu tarehe 29 Oktoba, 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 19 Safar 1440 Hijria sawa na 29 Oktoba 2018.

Siku kama ya leo miaka 1269 iliyopita yaani tarehe 19 Safar mwaka 171 Hijria  alizaliwa Abu Ma'ashar Balkhi mmoja kati ya wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya nujumu wa Kiirani. Alielekea Baghdad na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Abu Ma'ashar Balkhi alitumia vyanzo vya lugha za Kiarabu, Kihindi, Kigiriki na Kisiriani kwa ajili ya kupata elimu ya nujumu na kuwa miongoni mwa wanajimu wakubwa katika zama zake. Kazi zake katika taaluma hiyo zilitumiwa kwa karne kadhaa katika ulimwengu wa Kiislamu na Kimagharibi hata baada ya kufariki kwake dunia. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawalidul al Saghirah.

Katika siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, mfumo wa utawala wa serikali ya jamhuri uliasisiwa nchini Uturuki kwa uongozi wa Rais Mustafa Kemal mashuhuri kwa jina la Ataturk. Kemal Ataturk aliiongoza kidikteta nchi hiyo kwa muda wa miaka 15 na kufanya hujuma za kufuta sheria, nembo pamoja na matukufu ya Kiislamu na wakati huo huo, kueneza utamaduni na nembo za Kimagharibi nchini humo. Hata baada ya kufariki dunia kiongozi huyo aliyekuwa na uadui na Uislamu mnamo mwaka 1938, njama hizo dhidi ya Uislamu nchini Uturuki ziliendelezwa na wafuasi wake.

Kemal Ataturk

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita yaani tarehe 7 Aban mwaka 1305 Hijria Shamsia Ayatullah Sayyid Hassan Modarres aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na wanamapambano maarufu nchini Iran alinusurika jaribio la kuuawa. Jaribio hilo lilifanywa na vibaraka wa Shah Reza Pahlavi aliyekuwa maarufu kwa udikteta, ukatili na upinzani mkubwa dhidi ya maulama wa Kiislamu. Uhasama wa utawala wa kifalme wa Pahlavi dhidi ya Ayatullah Modarres ulitokana na mchango mkubwa wa mwanazuoni huyo wa Kiislamu katika kuwaamsha wananchi na kufichua njama za utawala wa Kipahlavi na muungaji mkono wake yaani serikali ya Uingereza. Kwa kipindi fulani Ayatullah Modarres alikuwa mwakilishi wa wananchi wa Tehran katika Bunge. Baada ya kunusurika kifo katika jaribio hilo Ayatullah Modarres alipelekwa uhamishoni kwa amri ya mfalme dikteta Reza Khan na muda mfupi baadaye aliuawa shahidi na vibaraka wa Shah.

Ayatullah Sayyid Hassan Modarres

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, askari jeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia Peninsula ya Sinai iliyoko Misri. Mashambulio hayo yalianza baada ya Rais wa wakati huo wa Misri, Gamal Abdul Nassir kutaifisha mfereji wa Suez. Siku mbili baada ya mashambulio hayo, Uingereza na Ufaransa zilipeleka majeshi yao pembezoni mwa mfereji huo kwa lengo la kuusaidia utawala ghasibu wa Israel. Mnamo mwaka 1957 majeshi vamizi ya Ufaransa, Uingereza na utawala haramu wa Israel yaliondoka katika ardhi ya Misri kufuatia mashinikizo ya fikra za waliowengi, madola mengi ya Magharibi na upatanishi wa Umoja wa Mataifa.

Zana za kivita za Misri zilizoharibiwa katika vita vya mfereji wa Suez.

Na siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, katika jinai yao nyingine, Wazayuni waliwauwa kwa umati wakazi wa kijiji cha Kafr Qasim huko Palestina. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni walitangaza utawala wa kijeshi katika kijiji hicho. Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni waliwauwa kwa umati wanawaume, wanawake na watoto madhlumu wa Palestina wasiopungua 49 na kujeruhi makumi ya wengine huko Kafr Qasim.

Msikiti wa Mashahidi, kumbukumbu ya mashahidi wa Kafr Qasim.