Nov 02, 2018 23:24 UTC
  • Jumamosi, 3 Novemba, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 24 Mfunguo Tano Safar 1440 Hijria sawa na tarehe 3 Novemba 2018.

Siku kama ya leo miaka 1055 iliyopita, Sahib bin Ubbad, mwanafasihi maarufu na msomi wa Kiislamu wa kizazi cha Dailami alifariki dunia. Sahib alikuwa mwandishi hodari na mtu mwenye hadhi na mtajika sana katika zama zake. Licha ya kwamba alikuwa waziri katika serikali ya kizazi cha Dailami, lakini alikuwa mtu mnyenyekevu na mwema kwa watu wa chini yake. Sahib bin Ubbad ameandika vitabu vingi, na maarufu zaidi ni kile cha "al-Muhiit" chenye juzuu saba. ***

Kaburi la Sahib bin Ubbad mjini Isfahn Iran

 

Miaka 115 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Panama ilifanikiwa kujipatia uhuru wake kutoka Colombia na siku hii huadhimishwa nchini humo kama siku ya taifa. Ardhi ya Panama iligunduliwa na kukaliwa kwa mabavu na Wahispania mnamo mwaka 1501 Miladia. Panama ilikaliwa kwa mabavu na Colombia mwaka 1821 Miladia na tangu wakati huo wananchi wa nchi hiyo walianzisha mapambano dhidi ya wavamizi wa Colombia. Mapambano hayo ya wananchi yalishadidi zaidi baada ya kuwasilishwa mpango wa mfereji wa Panama. Mwaka 1903,Panama ikafanikiwa kujitenga na Colombiana kujitawala. ***

Bendera ya Panama

 

Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, wakati wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Misri, askari wa utawala huo waliwaua kwa umati Wapalestina katika mji wa Khan Yunus uliopo katika Ukanda wa Gaza. Baada ya kuingia katika mji huo askari hao wa Kizayuni waliwaua askari 25 wa Misri na baadaye wakavamia hospitali na kuwaua wagonjwa na wauguzi waliokuwa humo. Baadaye askari hao katili wa utawala wa Kizayuni walishambulia kwa mabomu na kuteketeza kambi ya wakimbizi ya mji wa Khan Yunus ambako makumi ya wanawake na watoto wadogo walikuwa wakiishi. ***

Mahala ulipo mji wa Khan Yunus katika Ukanda wa Gaza

 

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 12 Aban 1352 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'arani arifu, faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 71. Msomi huyo alibobea katika elimu mbalimbali za kidini na alikuwa mahiri katika lugha kadhaa za kigeni. Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'arani ameandika vitabu vingi na alikuwa mahiri katika elimu za mujumu na nyota. ***

Marhum Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'arani

 

Na miaka 22 iliyopita katikak siku kama ya leo ya tarehe 3 Novemba, alifariki dunia Jenerali Jean-Bedel Bokassa dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Jean-Bedel Bokassa anayejulikana pia kama Bokassa I (wa kwanza) alichukua madaraka mwaka 1921 kupitia mapinduzi ya kijeshi, baada ya kuiondoa madarakani serikali ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Afrika ya Kati David Dacko. Bokassa alifanya mapinduzi hayo kwa uungaji mkono wa Ufaransa. Katika miaka 14 ya utawala wake, kiongozi huyo alitenda jinai na mauaji mbalimbali na kujilimbikizia mali nyingi. ***

Jean-Bedel Bokassa