Nov 05, 2018 06:57 UTC
  • Jumapili, tarehe 4 Novemba, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 25 Mfungo Tano Swafar 1440 Hijiria, sawa na tarehe nne Novemba 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufalme wa Austria-Hungary ulisalimu amri kwa waitifaki ikiwa ni wiki moja tu kabla ya kufikia tamati Vita vya Kwanza vya Dunia. Utawala huo ambao ndio uliokuwa umeanzisha vita, ulikuwa ukihesabiwa kuwa muitifaki muhimu wa Ujerumani. Hata hivyo kutokana na kushindwa mara nyingi katika vita, ulikubaliana na masharti ya kuacha vita. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Austria-Hungary uligawanywa kwa nchi kadhaa na ukoo wa Habsburg uliokuwa ukitawala ukasambaratika. 

Ufalme wa Austria kabla ya kugawanywa

Siku kama ya leo miaka  62 iliyopita na kufuatia kuongezeka upinzani dhidi ya utawala wa kikomonisti huko Hungary, Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti liliikalia kwa mabavu nchi hiyo. Baada ya kifo cha Joseph Stalin, kiongozi dikteta wa Umoja wa Kisovieti 1953 na kupatikana anga ya wazi kwa kiwango fulani kupitia mrithi wake Nikita Khrushchev, baadhi ya nchi za Kikoministi za Ulaya zilitaka kuweko anga ya wazi zaidi. Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Magharibi vilikuwa vikiwashajiisha wananchi na kuwataka waanzishe harakati na mapambano. Hapo ndio wananchi wa Hungary walipoanzisha harakati dhidi ya utawala wa nchi yao na kuwaua Wakoministi kadhaa. 

Nikita Khrushchev

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, askari vibaraka wa utawala wa Shah uliokuwa ukitawala Iran waliivamia nyumba ya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini mjini Qum na kumkamata. Baada ya kumhamishia mjini Tehran, utawala wa Shah ulimbaidishia Imam Khomeini nchini Uturuki. Utawala wa Shah uliamua kufanya hivyo kutokana na uungaji mkono wa Imam Khomeini kwa harakati za mapambano za wananchi Waislamu wa Iran za kutaka kujitawala, uhuru na kutetea thamani za kidini. Lengo la kumpeleka uhamishoni Imam Khomeini lilikuwa ni kusimamisha mapambano yake na wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala huo, kwani utawala wa Shah ulitambua kwamba kuwepo Imam nchini kuliwaamsha wananchi dhidi ya utawala huo wa kidikteta.

Imam Khomeini akibaidishwa

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita yaani tarehe 13 Aban mwaka 1357 Hijria Shamsia, na katika kujiri harakati za mapambano ya wananchi Waislamu nchini Iran, kulifanyika maandamano makubwa ya wanafunzi na wanachuo hapa mjini Tehran. Maandamano hayo yalikandamizwa vibaya na askari wa utawala wa Shah na kusababisha umwagaji damu mkubwa. Katika siku kama hii ambayo ilisadifiana na kumbukumbu ya kubaidishwa Imam Khomeini huko Uturuki, kundi kubwa la wanafunzi na wanachuo, wakiwa na lengo la kulaani kitendo hicho cha mfalme Shah walikusanyika katika Chuo Kikuu cha Tehran. Askari wa utawala wa Shah walishambulia kundi hilo la wanachuo na wanafunzi na kuwaua shahidi wanafunzi na wanachuo wengi. Tarehe 13 Aban ina umuhimu mkubwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu, na ndio maana imepewa jina la "Siku ya Wanafunzi."

Siku ya wanafunzi nchini Iran

Siku kama ya leo 39 iliyopita, wanafunzi na wanachuo wa Tehran walifanya maandamano makubwa katika mji huu kwa mnasaba wa kukumbuka tukio la kubaidishiwa nchini Uturuki Imam Khomeini (MA) na kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tangu kuuawa wanafunzi na wanachuo wa Iran. Mauaji hayo yalifanywa na vikosi vya usalama vya utawala wa Shah. Wanafunzi na wanachuo kadhaa wa Kiislamu walioshiriki kwenye maandamano hayo ambao walikuwa wakijulikana kama Wafuasi wa Sera za Imam, waliuvamia ubalozi wa Marekani mjini Tehran, ambao ulikuwa pango la ujasusi dhidi ya wananchi wa Iran. Kabla ya ubalozi huo kuvamiwa na wanafunzi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na kwa mara kadhaa ilikuwa imeshawasilisha malalamiko yake kwa Marekani kutokana na uingiliaji wa Washington katika masuala ya ndani ya nchi hii. Hata hivyo ikulu ya White House haikuzingatia hata kidogo malalamiko hayo ya Iran. Baada ya kuvamiwa na kufichuliwa nyaraka zilizowekwa wazi, ilibainika kwamba kiuhalisia ubalozi huo ulikuwa kichaka cha ujasusi na kupanga njama dhidi ya Iran, na ni kwa ajili hiyo ndio maana katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, siku ya kudhibitiwa ubalozi huo wa Marekani ikatambuliwa kuwa ni siku ya kupambana na ubeberu wa dunia.

Kudhibitiwa ubalozi wa Marekani na wanafunzi wa Iran

Na siku kama ya leo miaka 23 iliyopita Waziri Mkuu wa wakati huo wa utawala ghasibu wa Israel Yitzhak Rabin aliuawa kwa kupigwa risasi na Mzayuni mwenye misimamo mikali. Rabin alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel kwa tiketi ya chama cha Leba katika mwaka 1974 na kuongoza hadi 1977, ambapo alilazimika kujiuzulu kutokana na ubadhirifu wa mali ya umma. Alichaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Israel mwaka 1992 na kudumisha mazungumzo eti ya amani ya Mashariki ya Kati. Mauaji ya Yitzhak Rabin yaliyofanywa na Myahudi mwenzake Yigal Amir ni mfano wa wazi wa hitilafu kubwa zilizoko kati ya viongozi wa utawala unaoikalia Palestina kwa mabavu wa Israel. Ni muhimu kukumbusha kuwa, Yitzhak Rabin alikuwa miongoni mwa makamanda wa makundi ya kigaidi ya Kizayuni.

Yitzhak Rabin