Jumanne 6 Novemba, 2018
Leo ni Jumanne tarehe 27 Safar 1440 Hijria sawa na Novemba 6 mwaka 2018.
Miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Ayatullah Sayyid Abdul Ali Musawi Sabzavari mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Iran. Ayatullah Sabzavari alizaliwa mwaka 1290 Hijria shamsia katika mji wa Sabzavar huko kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanazuoni huyo alianza masomo ya Kiislamu akiwa na umri wa miaka 14 na baadaye akaendelea na masomo hayo katika mji mtakatifu wa Mash'had Iran. Baadaye alielekea katika mji wa Najaf nchini Iraq na kunufaika na elimu ya mafunzo ya Kiislamu na katika kipindi kifupi akafikia daraja ya Ijtihad. Mwanazuoni huyo mkuwba ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha Lubbul Maarif.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita Meir David Kahane, kuhani aliyekuwa na chuki na misimo mikali ya kidini wa Kizayuni aliuawa mjini New York huko Marekani. David Kahane alizaliwa mwaka 1932 katika mji huo huo na alifungwa jela miaka kadhaa katika kipindi cha ujanani kutokana na uhalifu wa wizi, ubakaji na kadhalika. Baadaye Meir David Kahane alijiunga na Uzayuni hadi kufikia daraja ya kutambuliwa kuwa kuhani mwenye misimamo mikali. Mwaka 1968 aliasisi kile kilichojulikana kama Jumuiya ya Kulinda Wayahudi (JDL) ambayo wanachama wake walikuwa Wazayuni wenye misimamo mikali na waliopewa mafunzo ya jeshi. Polisi ya Marekani ililazimika kuwatia nguvuni baadhi ya wanchama wa kundi hilo akiwemo Kahane mwenyewe kutokana na shughuli na harakati zao za kigaidi. Miaka mitatu baadaye alihamia Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kujiunga na Bunge la Israel (Knesset). Meir David Kahane alikuwa akihimiza kufukuzwa Wapalestina wote katika ardhi yao na alikuwa akisema kuwa, Msikiti wa al Aqsa unapaswa kupingwa mabomu na kubomolewa.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita wafanyakazi wa redio na televisheni ya Iran walianza mgomo wakipinga utawala wa Shah. Mgomo huo ulifanyika kwa shabaha ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya utawala wa Shah na kuharakisha mwenendo wa kuipindua serikali yake. Siku hiyo hiyo maafisa wa jeshi la Shah walishambulia taasisi za magazeti na vyombo vya habari na kuwatia nguvuni waandishi kadhaa. Hatua hiyo ilipelekea kusitishwa uchapishaji wa magazeti yaliyokuwa yakichapishwa kwa wingi nchini.
Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Novemba 1860 Abraham Lincoln aliyekuwa mpinzani wa utumwa nchini Marekani, alichukua madaraka na kuwa rais wa nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wake vita kadhaa vilitokea nchini humo na kupelekea waliokuwa wakiunga mkono utumwa kushindwa. Abraham Lincoln aliuawa mwaka 1865 na mmoja wa wapinzani wa harakati za kupinga utumwa nchini Marekani.
Siku kama ya leo miaka 205 vita vya kwanza vya Simon Bolivar, shujaa wa uhuru wa mataifa ya Amerika ya Latini vya kukomboa nchi ya Venezuela kutoka kwa wakoloni wa Kihispania vilimalizika kwa ushindi. Katika vita hivyo askari 6500 wa Simon Bolivar waliwashinda askari elfu 13 wa Uhispania. Hatimaye shujaa huyo wa Amerika ya Latini aliikomboa Venezuela kutoka utawala wa kikoloni wa Uhispania na kisha akashiriki katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi nyingine kadhaa za kusini mwa Amerika.
Miaka 386 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Gustav wa Pili, mfalme wa Sweden. Alizaliwa mwaka 1594 na alikalia kiti cha ufalme alipokuwa na umri wa miaka 17. Umaarufu wake ulitokana na kushinda kwake katika vita vya kidini vya miaka 30 kati ya Waprotestant na Wakatoliki vya mwaka 1618 hadi 1648.