Nov 07, 2018 23:06 UTC
  • Alkhamisi tarehe 08 Novemba, 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 29 Safar 1440 Hijria sawa na Novemba 8, mwaka 2018.

Siku kama ya leo miaka 1236 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Ali bin Mussa al Ridha AS, mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW. Mtukufu huyo alizaliwa mwaka 148 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Mussa al Kadhim AS. Mnamo mwaka 200 Hijria, Maamun, Khalifa wa Bani Abbasi, alimtaka Imam Ridha AS aelekee kwenye makao ya Khalifa huyo yaliyokuwa katika mji wa Marwi, kusini mashariki mwa Turkemenistan ambayo ilikuwa sehemu ya Khorasan Kuu. Ijapokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam Ridha kuwa mrithi wake, lakini kwa njia hiyo alikusudia kuimarisha zaidi nguvu za utawala wake. Utukufu na daraja ya juu ya kielimu na kiroho ya Imam Ridha na ushawishi wake uliokuwa ukiongezeka siku baada ya siku ndani ya fikra na nyoyo za watu vilimtia woga na hofu Maamun na hivyo akaamua kufanya njama za kumpa sumu na kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume katika siku kama leo. Imam AS amesema:"Mja bora zaidi ni yule ambaye kila anapofanya jema hufurahia, na kila anapokosea huomba msamaha, inapomfikia neema hushukuru, anapokumbana na masaibu husubiri na wakati anapoghadhibika husamehe".

Siku kama ya leo miaka 362 iliyopita, alizawa Edmond Halley, mtaalamu wa nyota wa nchini Uingereza. Halley alisoma katika kitengo cha Queen kilicho chini ya chuo kikuu cha Oxford nchini humo na kuanza kujishughulisha na masuala ya utafiti wa nyota akiwa kijana mdogo. Edmond Halley alichukua muda mwingi katika kutalii na kuchunguza nyota na kuelewa kwamba, kama ilivyo kwa sayari, nyota nazo zina mzingo na mzunguko wake maalumu. Mwaka 1704 alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Oxford na mwaka 1720 aliarifishwa kama mtaalamu wa masuala ya nyota. Halley alifariki dunia mwaka 1742 wakati akijishughulisha na masuala ya nyota.

Edmond Halley

Siku kama ya leo miaka 344 iliyopita, alifariki dunia John Milton, malenga wa Kiingereza. Kazi za kwanza za ushairi za John Milton zilijulikana kwa majina ya Roho na Huzuni na Roho ya Furaha. Diwani nyingine ya John Milton ni ile aliyoipa jina la Paradise Lost. Malenga Milton alikuwa akitetea suala la kutenganishwa serikali na kanisa, kuweko uhuru wa kuabudu na wakati huo huo aliunga mkono uchujaji wa taarifa uliokuwa ukifanywa na serikali.

John Milton

Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita sawa na tarehe 8 Novemba mwaka 1895, miale ya X iligunduliwa na Wilhem Conrad Rontgen, mwanafizikia na mwanasayansi maarufu wa Ujerumani. Mtaalamu huyo mwaka 1901 alitunukiwa tuzo ya Nobel kwa kufanikiwa kugundua miale hiyo. Kwa kuwa hakutambua miale aliyoigundua, Rontgen aliamua kuipa jina la X. Miale hiyo hupenya kwa urahisi katika mwili wa mwanadamu na kwa ajili hiyo ni njia nzuri zaidi ya kuchukua taswira ya viungo au picha ya X-ray inayotumiwa kujua sehemu za ndani ya mwili zilizodhurika au kuvunjika.

Wilhem Conrad Rontgen

Na siku kama ya leo miaka 118 iliyopita alizaliwa Bi Margaret Mitchell mwandishi wa Kimarekani huko Atlanta katika jimbo la Georgia. Baba yake Bi Mitchell alikuwa wakili wa mahakama. Kwa muda fulani alisomea taaluma ya udaktari lakini baadaye alilazimika kukatisha masomo hayo kutokana na majonzi aliyokuwa nayo kufuatia kifo cha baba yake. Margaret allianza kazi ya uandishi akiwa na umri wa miaka 22. Alizidi kupata umashuhuri baada ya kuchapisha riwaya yake aliyoipa jina la "Gone with The Wind." 

Bi Margaret Mitchell